Image

Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Kutoboa/Kuchorwa (Tattoo) Mwili Wako

Zamani ilikuwa ni kawaida kuona wanawake wanatoboa  masikio, pua, ili kuvaa aina mbalimbali za herini na shemeri. Siku hizi si ajabu kuona wanaume na wanawake wakijitoboa au kuchorwa alama (tattoo) sehemu mbalimbali za miili yao kama kwenye pua, mdomo, ulimi, tumbo, masikio, mikono, miguu, kwenye kichwa, mapaja, mgongo  na hata sehemu za siri yote haya kwa ajili ya urembo, miila au desturi zao, kutaka kujinasibu na tabaka fulani au kutaka kuonyesha ubunifu wao (artistic expression). 

Kutoboa/kuchorwa mwili kama kutafanywa na mtaalamu wa kutoboa/kuchora mwili hakuna madhara yoyote ya kiafya, madhara ya kutoboa/kuchorwa mwili  hupatikana pale tu ambapo kitendo hiki  hufanywa na mtu ambaye si mtaalamu na mjuzi wa fani hii bila kutumia njia salama za kiafya.
 
Katika utafiti uliofanywa nchini Marekani na madaktari bingwa wa ngozi (dermatologists) katika chuo kikuu cha Northwestern University Feinberg School of Medicine na kuchapishwa katika jarida la   American Journal of Clinical Dermatology umesema tatizo kubwa la kutoboa/kuchorwa mwili ni maambukizi (infection) yanayokisiwa kufika asilimia 20 ya kutoboa/kuchorwa sehemu mbalimbali za mwili. Maambukizi haya mara nyingi husababishwa na bakteria na huonekana katika sehemu ya mwili iliyotobolewa/kuchorwa.Madhara mengine ya kutoboa/kuchorwa mwili ni kuvuja damu, mzio/aleji, ngozi kuchanika pamoja  na ngozi kuwa na baka au scarring.

Ni mambo gani ya kuzingatia kabla ya kutoboa/kuchorwa  mwili wako?

  • Unatakiwa kujua  uwezekano wako wa kupata maambukizi - Kama tayari una maambukizi au una kidonda kilichowazi, ni bora ukaacha kutoboa/kuchorwa mwili mpaka utakapopona na kuwa na afya njema. Hatari ya kupata maambukizi ni kubwa kama utatobolewa/kuchorwa na mtu ambaye si mtaalamu na hana ujuzi wa kufanya kazi hii. Hakikisha anayekufanyia  hivi awe anafahamu masuala ya kukinga wateja wake na maambukizi ambayo ni pamoja na kusafisha vifaa vyake kila baada ya kazi, kuvichemsha vifaa hivyo au kuhakikisha vipo salama na havina bakteria wowote kwa kutumia kemikali za kusafishia, kuvifunika vifaa hivyo baada ya kuvisafisha na yeye mwenyewe kuvaa gloves salama (surgical gloves) wakati wa kufanya kazi yake hiyo ili hata kama ana magonjwa ya kuambukiza asiweze kukuambukiza wewe kwani zipo taarifa ambazo watu wameambukizwa ugonjwa wa ukimwi  au wamepata ugonjwa wa tetanus wakati wa kutobolewa/kuchorwa miili yao.
  • Hakikisha huna maradhi yoyote sugu - Kama una maradhi ya kisukari, ni bora ukaepuka kutoboa/kuchorwa mwili kwani kidonda chake kinaweza kisipone haraka na hatari ya maambukizi kwa wagonjwa wa sukari iko juu kupitia kwenye vidonda.
  • Fahamu kuhusu uwezo wako wa kupona - Unatakiwa uwe na ufahamu juu ya uwezo wa mwili wako katika kupona (healing tendencies) kidonda chochote kile. Kuna watu wengine wanapopata mchubuko au kukatika ngozi zao hupona kwa ngozi ile kufanya kama baka na uvimbe unaojulikana kama keloids. Kama wewe ni mmoja wa watu wa aina hii basi unahitaji kuepuka kufanya kitendo hiki cha kutoboa/kuchora mwili wako. Sehemu ambazo huchukua muda mrefu kupona baada ya kutoboa/kuchora mwili ni pamoja na kwenye maeneo ya tumboni, kwenye chuchu na hata sehemu za siri kwa wanawake.
  • Jua maumbile yako-Sio kila ngozi ya mwanadamu inafaa kwenye kuitoboa/kuchora, mfano, wale wenye ngozi  ya kwenye tumbo iliyoenuka ndio hufaa kutoboa sehemu hii, kama unataka kutoga ulimi na ulimi huo ni mfupi kutokana na umbile lako, (Tongue with short frenum) yaani wale wenye mkunjo chini ya ndimi zao  na hivyo kufanya ulimi kuwa mfupi, hawapaswi kutoga ndimi zao
  • Hakikisha unafanyiwa na mtaalamu wa fani hii.Wataalamu wa mambo ya kutoboa/kuchora mwili wana uelewa mkubwa wa maumbile ya mwanadamu na huwa na vifaa vya kuzuia uvujaji wa damu pindi unapotokea. Pia huwa na ufahamu wa jinsi ya kukulinda na maambukizi .
  • Historia yako ya afya- Wataalamu wa kutoboa/kuchora mwili wanatakiwa kuchukua historia ya  afya ya wateja wao inayohusisha magonjwa ya moyo, ugonjwa wa kisukari, mzio/aleji, ugonjwa wa pumu na kadhalika. Kama unatumia dawa za ugonjwa wowote ule ni bora ukamweleza mapema mtaalamu huyo kabla hajaanza kukutoboa/kukuchora mwili wako. Ili kuzuia uvujaji wa damu kwa wingi, unashauriwa kuepuka dawa aina ya aspirin angalau kwa wiki moja kabla ya kutoboa/kuchora mwili  wako, pia epuka dawa jamii ya Non Steroidal Anti-Inflammataory Drugs (NSAIDS) kama ibuprofen, naproxen na kadhalika.
  • Hakikisha vifaa sahihi ndivyo vilivyotumiwa- Hakikisha ya kwamba  vifaa vinavyotumiwa ni vile ambavyo havina   madini ya Nickel, pini zenye ubora na vipachiko vya aina mbalimbali ambavyo ni vya ubora wa hali ya juu. Pini na vipachiko vidogo vinaweza kutoka na kusogea kutoka katika sehemu vilipopachikwa na hivyo kukuletea madhara makubwa. 
  • Mfumo wa maisha- Kipachiko cha katika maeneo ya tumboni (kitovuni, chini ya kitovu nk) huvutia kwa mwanamke wenye umri mdogo wa miaka ya ishirini na huleta picha mbaya kwa wanawake wale waliofikia umri wa miaka thelathini na kuendela. Unatakiwa uangalie  na aina ya taaluma yako  kama inaendana na vitu vya aina hivi, mathalani wewe ni mwanamume unafanya kazi ya mhudumu wa afya, mwalimu, askari,  unafanya kazi kwenye ofisi, muuzaji bidhaa kwa wateja, mtoa huduma za kijamii, halafu unavaa herini kwenye masikio, ha! Watu watakuchukuliaje?Hakuna atakaye kuelewa au kukubali kuhudumiwa na wewe.
  • Pia angalia kama  mila, desturi, dini  yako kama inakubali mambo haya kwani itakuwa jambo la aibu sana kama utatoga mwili wako  bila kuzingatia mazingira unayoishi kwani binadamu tunaishi kulingana na mazingira yetu. Hii sio kwa wanaume tu hata kwa wanawake, kabla ya kutoboa/kuchora  sehemu husika zingatia  taaluma yako, mila, desturi,mazingira,  dini yako nk.
  • Fuata maelekezo vizuri- Fuata maelekezo unayopewa vizuri jinsi ya kujikinga na maambukizi baada ya kutoboa/kuchorwa mwili wako, namna ya kusafisha sehemu husika nk.
  • Fahamu madhara ya kutoboa/kuchorwa sehemu husika- Fahamu kuhusu madhara ya kutoboa/kuchorwa sehemu husika kwanza kabla ya kutoboa/kuchorwa ili uweze kujiepusha na madhara hayo.Pia unatakiwa ujue sehemu hiyo unayotoboa/kuchora, kidonda chake kinapona baada ya muda gani na maumivu yake huchukua siku ngapi kuisha? Hatma ya afya yako ipo mikononi mwako! We are what we are! Tafakari!
  • Imesomwa mara 34563 Imehaririwa Jumanne, 28 Novemba 2017 12:03
    Dr Khamis

    Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

    Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

    Makala shabihana