Image

Hakuna ubaya wowote kwa mtu kutaka kupendeza. Swala la kuonekana mzuri au kuwa mtanashati limekuwa sehemu muhimu kwa maisha ya binadamu hususani upande wa dada zetu. Si kitu cha ajabu maana tangu enzi za mababu , tunasoma katika historia jinsi mwanamke alivyosifiwa kwa uzuri na urembo wake.

Swala la uzuri na urembo wa mwanamke linajadiliwa mara nyingi katika aya mbalimbali za misahafu ya dini zetu, kuonesha ni jinsi gani ambavyo hata Mungu mwenyewe anavyouthamini uzuri na urembo wa mwanamke. Si ajabu kuona jinsi ambavyo makampuni makubwa yanayojishughulisha na utengenezaji wa vipodozi na nguo, vitu ambavyo vinachangia sana katika kumfanya mwanamke aonekane mzuri na mrembo, yanavyotengeneza faida kubwa.

 Sikatai kwamba kuna uzuri wa kuzaliwa, la hasha. Ni dhahiri kabisa wapo watu waliojaliwa kuwa na muonekano mzuri ambao wamezaliwa nao. Na mtakubaliana na mimi kwamba kuna baadhi ya vitu katika miili yetu ambavyo hatuwezi kuvibadilisha hata kama hatuvipendi, lakini habari njema ni kwamba asilimia kubwa ya muonekano wa sura na miili yetu waweza kubadilishwa, na kuendana na matakwa yetu.

Siongelei wala sishauri utumiaji wa madawa au njia nyingine zenye madhara katika mwili wa binadamu. Bali naongelea jinsi ambavyo mfumo wa maisha waweza kukusaidia kupata muonekano unaoupenda bila kuwa na madhara yeyote ya kiafya katika mwili. Usifikirie sana, hapa naongelea vitu vya kawaida kabisa katika maisha yetu ya kila siku visivyo kuwa na gharama yeyote zaidi ya muda. Naongelea mazoezi na lishe bora.