Image

Matibabu ya Mzizi wa Jino (Root Canal Treatment)

Haya ni matibabu ambayo hutolewa kwa jino ambalo sehemu ya uhai wake imeharibika kiasi kwamba haliwezi kutibika kwa kuziba tu, kwa maneno mengine hii ndiyo njia mbadala ya kutibu jino bila kung’oa.

Matibabu uhusisha kutoboa jino hadi sehemu ya uhai wa jino yenye mishipa ya damu na ile ya fahamu na chembechembe za meno na kuviondoa nikimaanisha kuondoa mishipa ya fahamu, ya damu na chembe pamoja na ugonjwa na baadae kuijaza sehemu hii na vitu maalumu vinavyokubaliana na mwili (biocompatible).

Aina za matibabu ya mzizi wa jino

Kuna aina kuu mbili za matibabu ya mzizi wa jino

Njia ya kawaida (conventional root canal treatment)
Njia hii ni kama nilivyoeleza hapo juu, kuingia kwenye kiini cha jino na kuondoa kila kitu kilichomo na kisha kujaza uwazi uliobaki na vitu maalumu vinavyokubaliana na mwili

Matibabu ya mzizi wa jino yanayohusisha upasuaji
kwa njia hii mbali na kutumia njia ya kwanza, upasuaji hufanyika pia ili kondoa mfupa uliofunika ncha ya mzizi wa jino kusafisha eneo lililozunguka ncha ya mzizi na baadaye kukata ncha husika kisha kuziba kutokea kwa nyuma (retro grade filling).

Njia hii hutumika pale njia ya kawaida inaposhindwa kuondoa tatizo au inapoonekana kabisa kuwa haitaweza kuondoa tatizo. Huu ni upasuaji mdogo, unaofanyika kwa ganzi ndogo ya eneo husika (local anaesthesia). Mafanikio ya matibabu haya ni makubwa sana.

Ni meno yapi yanahitaji matibabu hayo?

•    Meno yaliyooza hadi uoza kufikia kiini cha jino (dental pulp) - sehemu ya uhai wa jino.
•    Meno yaliyopata ajali na kupasuka na kuacha kiini cha jino kikiwa wazi (traumatic pulp exposure)
•    Meno yaliyopata ajali na kusababisha mishipa ya damu kukatika au kupasuka na kuvunjika ndani ya jino, kitu ambacho hupelekea jino kufa (pulp necrosis) na baadaye kusabisha jipu au kubadilika rangi
•    Wakati mwingine japo ni mara chache, ni pale tunapokuwa tunataka kuliweka sawa jino/meno ambalo/ambayo hayapo kwenye mstari sawa ili yaendane na meno mengine.
•    Pia wakati mwingine, tunapo lisaga jino ili liweze kubeba meno bandia ya daraja (bridge) huku tukiwa na mashaka na uhai wake.

Nini dalili zinazoashiria jino kuhitaji matibabu haya?

•    Jino linalouma - kuuma kwa jino kunashiria ugonjwa kuwa umeingia ndani ya kiini cha jino na au hata kupitiliza na kuingia kwenye mfupa ulioshikilia jino
•    Jino lililooza na kusababisha uvimbe, liwe linauma au haliumi
•    Jino lililokatika na kupoteza zaidi ya nusu ya kichwa cha jino (crown) kukatika kuwe kwa ajali au kuoza au vyote kwa pamoja
•    Jino linalobadilika rangi huku kukiwa na historia ya kuligonga mahali au kuchapwa ngumi usoni, hapa jino linaweza kuanza kubadilika rangi miezi sita tangu siku ya ajali mpaka wakati mwingine hadi miaka ishirini wakati mgonjwa alishasahau hata ajali yenyewe.

Meno yasiyofaa kwa matibabu haya

•    Meno yaliyoharibika vibaya kiasi kwamba hayatibiki tena japo ni machache, kwani hata kama jino limebaki mzizi tu, ukiwa bado imara twaweza fanya matibabu haya na baadae kujenga kichwa (crown)
•    Meno yaliyolegea sana kutokana na magonjwa ya fizi ambayo hayawezi kuimarishwa tena.
•    Magego ya mwisho (wisdom teeth) kwa kawaida meno haya huwa yana maumbile yasiyotabirika kiasi kwamba hata mafanikio ya matibabu huwa hayatabiriki, hii ikiambatana na kuwa yako nyuma sana kiasi cha kuwa vigumu kuyafikia kwa ufasaha na vifaa vyetu na pia yana mchango kidogo kwa usagaji chakula (2%)
•    Meno ambayo mifereji ya mizizi ambayo hupitisha mishipa ya fahamu na damu imeziba (calcified root canals)

Mafanikio ya matibabu haya

Kiwango cha mafanikio ya matibabu haya ni kati ya asilimia sabini na saba hadi tisini na nane (77-98%). Haya ni mafanikio ya hali ya juu kwa matibabu ya aina yeyote ile, mafanikio huongezeka zaidi pale tabibu anapotumia vifaa vya kumuongezea uwezo wa kuona kama dental loops na operating microscope.

Kutokufanikiwa kwa matibabu haya

Ziko sababu mbali mbali zinazoweza kusababisha matibabu haya yasifanikiwe, baadhi zikitokana na udhaifu wa tabibu na zingine kutokana na jino lenyewe lilivyo (internal tooth morphology).

Tabibu

Iwapo tabibu hakusafisha jino vizuri na kuliziba sawasawa upo uwezekano mkubwa wa matibabu haya kutokufanikiwa. Pia ikiwa tabibu hafahamu vizuri maumbile ya ndani ya jino, kuna uwezekano sehemu zingine kuachwa bila kusafishwa.

Meno

Meno mengine yana maumbile yasiyo ya kawaida, mfano katika hali ya kawaida meno ya mbele yana mfereji mmoja wa kupitisha mishipa ya fahamu na damu, lakini kuna jino lingine linakuwa na mifereji miwili au mitatu, hapa kwa mazoea na kwa kukosa vifaa vya kisasa ni rahisi kusafisha mfereji mmoja na kuacha mingine, vivyo hivyo kwa magego ambayo kwa kawaida yana mifereji mitatu hadi mine, lakini mengine mitano, sita, saba hata utafiti fulani huko China umegundua baadhi ya magego kuwa na matundu nane. Meno ya namna hii ni vigumu kufanikiwa.

Nini kifanyike ili kupunguza uwezekano wa matibabu kutofanikiwa?

Tabibu lazima ajikumbushe maumbile ya ndani ya jino analotaka kulitibu kabla ya kuanza matibabu na pia ajue kwamba jino laweza kuwa na mifereji ya ziada hivyo ajitahidi kuitafuta. Matumizi ya vifaa vya kusaidia kuona ni muhimu na hata matumizi ya x-ray za kisasa kama 3-dimensional digital x-ray ili kuweza kuona pande tatu za jino.

Kwanini meno yanaendelea kutolewa wakati matibabu haya yapo?

•    Matibabu haya ni gharama ukilinganisha na kung’oa jino hii ikiendana pamoja na umaskini wa wananchi walio wengi ambao hushindwa kugharamia na hivyo kuchagua kung’oa.
•    Baadhi ya hospitali hazina wataalamu au vifaa vya matibabu haya au vyote kwa pamoja
•    Mwamko mdogo wa wananchi kuhusu matibabu ya meno, hii inachangiwa pia na tabibu wa meno kutokuelezea matibabu mbadala zaidi ya kung’oa. Tafiti zimeonesha baadhi ya tabibu wa meno hutoa maelezo kwa yale matibabu wanayoyaweza tu, badala ya kuwaeleza pia upatikanaji wa matibabu mbadala katika sehemu zingine.
•    Watu kuchelewa kufika hospitalini, wakija baadhi yao matibabu pekee yanayokuwa yamebaki ni kung’oa tu, hapa napo kuna mchango wa umaskini na uelewa mdogo
•    Imani potofu kuwa tiba ya kudumu ya jino ni kuling’oa
•    Uzoefu wa zamani, kwa mtu ambaye aliwahi kuziba jino na likauma tena, ukimwambia matibabu haya ni vigumu kuyakubali

Hitimisho

•    Jali meno yako kama unavyojali viungo vingine vya mwili wako
•    Kungoa jino kama tiba ya ugonjwa wa jino, ni pale tu ambapo jino hilo haliwezi tibika kwa njia mbadala kama hii ya mzizi wa jino au pale inapobainika kuwa jino husika kuendelea kubaki pale hata likiwa limetibika linaweza kuwa chanzo cha kuleta madhara makubwa mwilini kama uoto mpya n.k.

Imesomwa mara 24542 Imehaririwa Ijumaa, 05 Mai 2017 16:03
Dr. Augustine Rukoma

Dr Dr. Augustine Rukoma ni daktari na mtaalamu wa meno, anapenda kutumia muda wake wa ziada kuandika makala na kubadilishana mawazo juu ya afya ya kinywa na Meno.

rukomadentalanswers.blogspot.com | Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana