4. Kupiga mswaki mara mbili kwa siku kunaepusha kuoza kwa meno
Kupiga mswaki kwa ufanisi walau mara mbili kwa siku huondoa ukoko unaogandiana kinywani na kusababisha kuoza kwa meno. Ukoko huu ni ute laini unaoganda kwenye sehemu mbalimbali za jino/meno huku ukiwa na mamilioni ya vimelea vya magonjwa (bakteria). Matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss) kila siku husaidia kuondosha ukoko maeneo ambako mswaki haufiki, vile vile kuondosha ukoko huu kunasaidia kujikinga na magonjwa ya fizi.
5. Magonjwa ya kinywa na meno husababisha harufu mbaya mdomoni
Takribani asilimia 85 ya watu wenye harufu mbaya kinywani huwa na magonjwa ya kinywa na meno,Ikiwa harufu mbaya kinywani inasababishwa na magonjwa kinywani, dawa za kusafisha kinywa (mouthwash) haziwezi kuondoa tatizo zaidi ya kulifunika kwa muda tu.
Hakuna sababu ya kuona haya kumwambia daktari wa meno kuhusu harufu mbaya kinywani inayokusumbua, kwa vile kumwambia na kujadili tatizo lako ni njia ya kuelekea kwenye tiba ya uhakika. Matumizi ya nyuzi-safishi (dental floss) kila siku, kusafisha meno na ulimi kwa mswaki walau mara mbili kwa siku yaweza kuondoa harufu mbaya kinywani kwa kiasi kikubwa.
6. Chakula bora ni muhimu kwa afya bora ya kinywa na meno
Ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye sukari na visivyo na virutubisho vya mwili vinapochanaganyikana na vimelea vya magonjwa (bakteria) hutengeneza tindikali ambayo hushambulia ukuta wa nje wa jino (dental enamel). Kushambuliwa kwa enameli na tindikali husababisha mashimo kwenye meno na magonjwa ya fizi.
Kudhitibi na kupunguza ulaji wa vyakula vyenye sukari kwa wingi itakuepusha na magonjwa ya kinywa na meno.
7. Bila matibabu, magonjwa ya kinywa na meno hayaponi wala kupata nafuu
Pale daktari wako wa meno anapokupa mpango makakati wa matibabu ya kinywa na meno yako, jukumu lako ni kuzingatia maagizo na maelekezo ya daktari ili upate matokeo mazuri. Inapotokea una mashimo makubwa kwenye meno, bado inawezekana kutibu meno kuanzia kwenye mzizi kabla meno hayajang'olewa.
8. Tiba ya mzizi wa jino haina maumivu
Amini usiamini, sio jambo la kustaajabisha kusikia mgonjwa aking'ang'ania jino ling'olewe kwa madai kuwa matibabu ya jino kuanzia kwenye mzizi wake ni yenye maumivu ya kupindukia, yasiyovumilika.
Ukweli ni kwamba, maendeleo ya teknolojia tiba yamefanya matibabu ya jino kuanzia kwenye mzizi kuwa rafiki na rahisi, tena hayana sifa yoyote ya maumivu makali kupindukia kama ambavyo watu wengi wanaamini, tiba hii ni moja ya tiba rafiki sana kwenye ulimwengu wa matibabu ya kinywa na meno.
9. Badili mswaki mara kwa mara
Umri wa miswaki tunayotumia unapaswa kuwa miezi mitatu (siku 90), baada ya muda huu ufanisi wa mswaki hupotea. Ikiwa unasumbuliwa na magonjwa ya fizi unashauriwa kubadili mswaki kila baada ya majuma manne hadi sita (wiki 4 – 6), kwa sababu vimelea vya magonjwa (bakteria) hijificha kwenye brush za mswaki. Vile vile unashauriwa kuosha mswaki wako kwenye maji ya moto kila baada ya kuutumia na kuubadilisha kila unapopata mashambulizi ya ugonjwa wa fizi.
10. Ni rahisi sana kutunza afya ya kinywa na meno
Watu wengi hifikiri kuwa kuwa na afya bora ya kinywa na meno kunahitaji jitihada za ziada, Ukweli ni kuwa, kumwona daktari wa meno mara kwa mara (walau mara mbili kwa mwaka kila baada ya miezi sita), na kusafisha meno kitaalamu, kupiga mswaki walau mara mbili kwa siku (asubuhi baada ya kupata kifungua kinywa, na usiku kabla ya kulala), kutumia nyuzi-safishi (dental floss), ulaji wa chakula bora chenye virutubisho ni vigezo muhimu sana vya kuwa na afya njema ya kinywa na meno, sasa ugumu upo wapi?