Image

Mahanjumati ya Eid

Leo katika mahanjumati ya Eid, tunakuletea mapishi ya biriani ya nyama ya ngombe, biriani na sosi ya nyama ya mbuzi, mandi na nyama, makbuus dajaaj, maandazi, mchuzi wa kima na mayai, nyama ya kukaanga na pilipili manga, juisi ya tikiti maji na embe, juisi ya mabungo na juisi ya mapera na karakara. Wapikie familia yako vyakula vitamu wafurahie sikukuu vizuri.

Biriani Nyama ya Ngombe

Biriani nyama ngombe

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo Vya Masala

Nyama vipande 3 lb (au Kilo moja na nusu)

Mtindi ½ Kopo

Thomu 1½ Kijiko cha supu

Tangawizi 1½ Kijiko cha supu

Nyanya 2

Pilipili mbichi Kiasi

Nyanya kopo 4 Vijiko vya supu

Vidonge supu (Curry cube) 2

Pilipili nyekundu paprika Kiasi

Bizari zote saga 2 Vijiko vya supu

Viazi 4

Mafuta 2 Mug

Samli ½ Kikombe

Vitunguu 6

Namna ya Kutayarisha na Kupika

 • Kwenye sufuria tia nyama, saga nyanya na thomu, pilipili mbichi, tangawizi. Mimina kwenye nyama na mtindi, tia na nyanya kopo, bizari paprika, vidonge vya supu, chumvi kisha changanya vyote pamoja weka motoni.
 • Katika sufuria nyengine tia mafuta na samli kaanga vitunguu mpaka viwe rangi ya hudhurungi toa weka pembeni.
 • Kaanga viazi weka pembeni.
 • Chukua mafuta kidogo uliyokaangia tia kwenye nyama acha katika moto wa kiasi mpaka nyama iive na maji ya punguke.
 • Tia viazi na vitunguu vivunje vunje tia ndani ya nyama acha moto mdogo.

Vipimo Vya Wali

Mchele 5 mug

Maji Kiasi

Chumvi Kiasi

Mafuta uliyokaangia vitunguu Kiasi

Rangi ya biriani ¼ Kijiko cha chai

*Zafarani ½ Kijiko cha chai

*Loweka rangi na zafarani kwenye kikombe na maji ¼ weka pembeni.

Namna ya Kutarisha na Kupika Wali

 • Osha mchele loweka muda wa saa.
 • Chemsha maji kama magi 10 hivi na chumvi tia mchele.
 • Uache uchemke ukishaiva kiini nusu, mwaga maji chuja.
 • Mimina juu ya nyama tia rangi na mafuta kwa juu funika.
 • Acha kidogo katika oveni kwa muda wa dakika 20 hivi kisha epua ikiwa tayari.

Mandi na Nyama (Wali wa Yemen)

Mandi na Nyama

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Mchele 3 Magi

Nyama ya mfupa 2 Ratili ( lb) au Kilo moja

Mafuta ¼ Kikombe

Vitunguu maji kata vikubwa vikubwa 3 Kikubwa

Bizari ya pilau ya unga (cumin) 1 Kijiko cha chakula

Pilipili manga ½ Kijicho cha chai

Hiliki ½ Kijiko cha chai

Karafuu ya unga ¼ Kijiko cha chai

Mdalasini nzima 3 Vijiti

Mdalasini wa unga ½ Kijiko cha chai

Thomu na tangawizi 2 Vijiko vya chakula

Nyanya iliyokatwakatwa 1 Nzima

Kidonge cha supu(Curry cube) 1 au 2

Zafarani (ukipenda) loweka katika maji 1 Kijiko cha chai

Zabibu kavu (ukipenda) ¼ Kikombe

Pilipili mbichi Ukipenda

Chumvi Kiasi

Namna ya Kutayarisha na Kupika

 • Kwenye sufuria katakata nyama na isafishe vizuri kisha tia binzari zote pamoja na vitunguu viwili, nyanya freshi, thomu na tangawizi na chumvi kiasi acha ichemkie huku ukiongeza maji mpaka iive vizuri.
 • Ikishaiva epua nyama zote tia kwenye (tray) treya ya kuchomea kisha ukipenda unaweza kuongezea viungo au hivyohivyo ukaichoma (bake) kwa moto wa 350° C mpaka rangi ibadilike.
 • Ile supu inayobaki ichuje vizuri weka kando kwa ajili ya kupikia wali.
 • Tia mafuta katika sufuria, kisha kaanga tena kitunguu kimoja tia mdalasini kidogo na thomu na tangawizi na kidonge cha supu 1 au 2 acha ikaangike kisha mimina ile supu, ukipenda unaweza kutia rangi ya zafarani au rangi ya biriani acha ichemke, kisia maji kutokana na mchele, kisha mimina mchele upike mpaka uive.
 • Ukishaiva pakua kwenye sahani kisha weka nyama yako juu ya wali tayari kwa kuliwa na saladi au pilipili.

Kidokezo

Ukipenda unaweza kutia zabibu kavu kwenye wali. Tolea na kachumbari yake.

Biriani na Sosi ya Nyama ya Mbuzi

Biriani ya Sosi Nyama ya Mbuzi

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Nyama ya Mbuzi 1 Kilo

Mchele 4 Magi

Vitunguu 3

Nyanya 2

Nyanya kopo 3 Vijiko vya chai

Thomu na tangawizi iliyosagwa 2 Vijiko vya supu

Pilipili mbichi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Garam Masala (mchanganyiko wa bizari) 2 Vijiko vya supu

Hiliki 1 Kijiko cha chai

Chumvi Kiasi

Mafuta ½ Kikombe

Zafarani au rangi za biriani za kijani na manjano/orenji

Namna ya Kutayarisha na Kupika Sosi ya Nyama

 • Changanya nyama na thomu, pilipili, chumvi na nusu ya garam masala. Tia katika treya (tray) ya oveni uipike nyama (Bake) hadi iive. Au iivishe kwa kuichemsha.
 • Katika kisufuria nyengine, tia mafuta (bakisha kidogo ya wali) kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi, kisha tia nyanya, nyanya kopo, bizari zote nyingine zilizobakia.

Namna ya Kupika Wali

Mchele 4 magi

Mdalasini 1 Kijiti

Hiliki 3 Chembe

Kidonge cha supu(Curry cube) 1

Chumvi

 • Osha na loweka mchele wa basmati au pishori.
 • Tia maji katika sufuria uweke jikoni. Tia kidonge cha supu, mdalasini, hiliki na chumvi .
 • Yakichemka maji tia mchele, funika upike hadi nusu kiini kisha uchuje kwa kumwaga maji.
 • Tia mafuta kidogo katika mchele na zaafarani iliyolowekwa au rangi za biriani kisha rudisha mchele katika sufuria ufunike na upike hadi uive.
 • Pakua wali katika sahani kisha mwagia sosi ya nyama juu yake, pambia kwa kukatia nyanya, pilipili mboga na figili mwitu (Celery) au mboga yoyote upendayo.

Makbuus Dajaaj/ Machbuus ya Kuku (U.A.E)

Makbuus Dajaaj

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Mchele wa Basmati/pishori 4 Vikombe

Kuku (mkubwa kiasi) 1 (wa lb 6 -7) au Kilo 3 -3.5kg

Vitunguu vilivyokatwakatwa 3

Samli 4 Vijiko vya supu

Buharaat (bizari ya Machbuus) 2 Vijiko vya supu

Bizari ya manjano (haldi/tumeric) 1 Kijiko cha chai

Nyanya zilizomenywa na kukatwakatwa 3

Thomu iliyosagwa 2 Vijiko vya supu

Loomi (ndimu kavu) au ya unga ½ au ½ Kijiko cha chai

Mdalasini kijiti 1

Karafuu nzima 3

Hililiki nzima 4

*Maji 5 Vikombe

Kotmiri iliyokatwakatwa ½ Kikombe

Chumvi Kiasi

Baharaat – Bizari ya Makbuus

Pilipili Manga ½ Kikombe

Gilgilani (Corriander seeds) ¼ Kikombe

Mdalasini vijiti ¼ Kikombe

Karafuu ¼ Kikombe

Bizari ya pilau (cumin seeds) 1/3 Kikombe

Hiliki 2 Vijiko vya chai

Kungu manga 2

Paprika ya unga( Pilipili nyekundu) ½ Kikombe

Namna ya Kutayarisha Baharaat (bizari)

 • Vunja kungu manga, chambua hiliki utoe kokwa zake, kisha tia vitu vyote katika mashine ya kusagia (grinder) usage hadi iwe unga.
 • Changanya na Paprika bizari ikiwa tayari.
 • Ihifadhi katika chupa yenye mfuniko wa kubana vizuri.

Namna ya Kutayarisha na Kupika Makbuus

 • Osha na loweka mchele kwa muda kiasi.
 • Msafishe kuku, mkate vipande vinne weka kando.
 • Katika sufuria ya kupikia, tia samli, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (brown). Tia baharaat na bizari ya manjano, kaanga kwa dakika moja hivi.
 • Tia vipande vya kuku, chumvi, thomu, punguza moto na umkaange kuku katika masala ya vitunguu.
 • Tia nyanya, karafuu, loomi, mdalasini, hiliki, changanya vizuri na endelea kukaanga.
 • Tia maji (inategemea mchele unaotumia, huenda ukahitaji zaidi). Funika na pika kwa muda wa dakika 20-25.
 • Mwaga mchele maji uliyolowekea, mimina mchele katika supu, tia kotmiri, changanya vizuri, funika uchemke mchele, punguza moto na pika wali kama inavyopikwa pilau ukoroge mara moja au mbili tu.
 • Ukishaiva wali, pakua katika sinia/sahani na weka vipande vya kuku juu katikati ya wali.

Kidokezo

 • Ukipenda badala ya kupika wali katika sufuria baada ya kutia mchele na kukaribia kuiva, na kabla ya kukauka supu yote, mimina katika treya ya jalbosi (Treya ya foil) upike ndani ya oveni (bake) kwa moto wa takriban 400-450º kwa muda wa dakika 20-25.
 • Baharaat hiyo inatumiwa katika vyakula vya nchi za Kiarabu (Gulf States), hivyo unaweza kutumia kupikia machbuus ya vitoweo vingine kama nyama na samaki na vyakula vinginevyo kama michuzi n.k.

Maandazi

Maandazi

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Unga 4 Vikombe vya chai

Sukari 1 Kikombe cha chai

Hamira 1 Kijiko cha chai

Samli 1 Kijiko cha chai

Maziwa au Tui la nazi 1 ½ Kikombe cha chai

Hiliki Kiasi

Mafuta ya kukaangia Kiasi

Namna ya Kutayarisha na Kupika

 • Changanya unga Hamira, Samli, maziwa au tui, kisha vuruga na kanda ukandike kiasi.
 • Kata madonge manane kisha acha uumuke.
 • Ukishaumuka sukuma kila donge ukate vipande vinne.
 • Panga kwenye meza tena yaumuke. Weka mafuta ya kukaangia katika karaii na yakaange kwa moto wa kiasi.
 • Yatoe weka kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Mchuzi wa Kima na Mayai

Mchuzi wa Kima na Mayai

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Nyama ya kusaga 2 lb (Ratili) au Kilo moja

Mayai 6

Vitunguu 4

Thomu na Tangawizi 1 Kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa 1 Kijiko cha chai

Nyanya iliyokatwa katwa 4

Kotmiri ½ Kikombe

Pilipili Manga ¼ Kijiko cha chai

Bizari ya curry ½ Kijiko cha chai

Nyanya ya kopo 3 Vijiko vya supu

Garam masala 1 Kijiko cha supu

Mafuta ya kukaangia Kiasi

Namna ya Kutayarisha na Kupika

 • Chemsha mayai, yakiiva ambua maganda na uweke kando.
 • Katika sufuria weka mafuta yapate moto, Kaanga vitunguu hadi vigeuke na kuwa rangi ya hudhurungi.
 • Halafu tia thomu na tangawizi kaanga kidogo tu, kisha tia bizari zote na pilipili uendelee kukaanga.
 • Kisha weka nyama na uiache motoni huku unakoroga hadi iwe si nyekundu tena.
 • Tia nyanya na chumvi ziache zilainike halafu tia nyanya ya kopo.
 • Ongeza maji kiasi unavyopenda mchuzi wako kuwa mzito au mwepesi.
 • Kisha weka yale mayai ya kuchemsha na iache itokote kidogo kwa moto mdogo.
 • Mwishoe mwagia kotmiri, changanya na umimine katika bakuli na itakuwa tayari kwa kuliwa na wali au mkate upendayo.

Nyama ya Kukaanga na Pilipili Manga

Nyama ya Kukaanga na Pilipili Manga

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Nyama ½ lb au Robo kilo

Kitunguu 1

Kidonge cha supu 1

Chumvi Kiasi

Pilipili manga 1 Kijiko cha chai

Bizari ya pilau (cumin) ½ kijiko cha chai

Mafuta 2 Vijiko vya supu

Thomu 1 Kijiko cha chai

Tangawizi ½ Kijiko cha chai

Namna ya Kutayarisha na Kupika

 • Katika sufuria, kaanga vitunguu mpaka viwe rangi ya hudhurungi
 • Tia thomu, tangawizi, bizari ya pilau, pilipili manga, kidonge cha supu, na nyama.
 • Kaanga kidogo kisha tia maji kiasi tu cha kuivisha nyama.
 • Funika moto mdogo mdogo mpaka iwe kavu, ikiwa haikuiva utaongeza maji kidogo mpaka ikaangike na tayari kwa kuliwa.

Juisi ya Melon na Embe

Juisi ya Melon na Embe

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Tikiti la asali (honey melon) 1

Unga wa embe au embe 1

Tangawizi 1 Kijiko

Ndimu 1

Sukari ¼ Kikombe cha chai

Arki rose 2 Matone

Namna Ya Kutayarisha

 • imenye melon na ulikate kate kisha tia kwenye blender
 • Tia unga wa embe au embe iliyokatwa katwa
 • Kisha tia ndimu iliyokatwa vipande kiasi pamoja na maganda yake
 • Halafu weka sukari
 • Saga vizuri hadi ilainike
 • Mimina kwenye jagi kisha tia matone mawili ya arki rose ukoroge na tayari kwa kunywewa

Kidokezo

Ukiweka ndimu weka na maganda yake unapata ladha nzuri zaidi.

Juisi ya Mabungo

Juisi ya Mabungo

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo Kupata takriban gilasi 6

Mabungo 3

Maji 6 au 7 Gilasi

Sukari Kiasi upendacho

Chumvi Kidogo sana

Namna ya Kutayarisha

 • Kata mabungo na toa nyama yake tia katika mashine ya kusagia.
 • Tia maji, sukari na chumvi usage kidogo tu.
 • Chuja kisha mimina katika jagi uweke katika friji.
 • Mimina katika gilasi.

Juisi ya Mapera na Karakara/pasheni (Passion fruit)

Juisi ya Mapera na Passion

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Mapera 5

Karakara/Pasheni (Passion fruit) 9

Sukari Kiasi

Maji Kiasi

Namna ya Kutayarisha

 • Osha na katakata mapera kisha tia katika mashine ya kusagia (blender) na usage kwa maji kiasi kisha yachuje.
 • Kata karakara/pasheni toa nyama yake kisha saga katika blender kwa maji kiasi.
 • Changanya pamoja na juisi ya mapera na tia sukari kiasi kadiri upendavyo ikiwa tayari.

Credit kwa wavuti ya www.alhidaaya.com

Imehaririwa Jumanne, 09 Juni 2020 11:51
Tagged under
Share
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Makala shabihana