Image

Imani potofu kuhusiana na VVU/Ukimwi

Ukimwi ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa Kinga mwilini, ugonjwa huu husababishwa na virusi vya ukimwi(VVU). Njia kubwa inayopelekea maambukizi ya ugonjwa huu ni ngono, katika makala za awali, tuliangalia njia nyingine za maambukizi ya ugonnjwa huu pamoja na Njia Thabiti Ya Kujikinga Na Maambukizi Ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) .  Hadi sasa, bado hakuna tiba ya ugonjwa wa Ukimwi, lakini kuna dawa zinazotumika kupunguza makali ya ugonjwa huu (ARV), hivyo matumizi ya mapema ya ARV yatakuwezesha kuishi ukiwa na afya njema, na ndiyo sababu tunahimizwa sana kupima afya zetu ili kujitambua na kuchukua hatua mapema.

Ingawa maarifa ya ugonjwa huu ni mengi, ila bado kumeendelea kuwa ni changamoto kubwa katika jamii yetu na nchi nyingine zinazoendelea. MOja ya changamoto hizi ni imani potofu iliyojengeka katika jamii inayopelekea watu ama kuwanyanyapaa wagonjwa wa Ukimwi au kuogopa kupima kwakuwa wakishajulikana watanyanyapaiwa. Hii, hurudisha nyuma harakati za mapambano ya ugonjwa huu.

Leo hii tuangalie imani potofu juu ya ugonjwa wa ukimwi.

Hauwezi kuambukizwa au kumuambukiza mtu virusi vya ukimwi kwa njia zifuatazo

  • Kuumwa na mbu
  • Kwa jasho
  • Kuchangia vyoo, sauna, vifaa vya gym, bwawa la kuogelea
  • Kuchangia taulo
  • Kwenda shule pamoja au kuwa na rafiki mwenye virusi vya ukimwi
  • Kupiga chafya au kukohoa
  • Kushikana mikono, kukumbatia au kupigana busu kavu na mtu mwenye virusi vya ukimwi
  • Kuvuta hewa moja na mtu mwenye virusi vya ukimwi

Imani nyingine potofukatika jamii ni kama

Kupata maambukizi ya ukimwi ndiyo mwisho wa maisha, hii si kweli, kwa kupima na kujitambua mapema na kuanza ARV mapema, kutakupelekea kuishi maisha marefu yenye afya njema.

Unaweza kumtambua muathirika kwa kumuangalia afya yake au muonekano wake kwa macho. Hauwezi kumtambua muathirika kwa kuangalia kwa macho, watu wengi hawana dalili yoyote ya maambukizi ya ukimwi kwa miaka ya awali. Hivyo, njia pekee na ya uhakika kujua kama mwenza wako ana maambukizi au la ni kupima. Na, sasa hivi upimaji wa HIV umerahisishwa zaidi na unatolewa bila gharama yoyote.

Tohara kwa wanaume inazuia kabisa maambukizi ya ukimwi: Ukweli ni kuwa, tohara inapunguza hatari ya maambukizi ya virusi ya ukimwi kwa kiasi kikubwa kama ilivyoandika hapa, lakini si kweli kwa inazuia maambukizi.

Ukimwi unatibika: Hadi sasa bado hakuna tiba ya ugonjwa wa Ukimwi.  ARV husaidia kupunguza makali ya virusi vya ukimwi. Hivyo , matumizi bora ya ARV hupelekea virusi kufubaa na kushindwa kuzaliana hivyo kumuwezesha mtu anayeishi na virusi vya ukimwi kuisha maisha marefu na yenye afya lakini si kweli kwamba zinatibu ugonjwa wa Ukimwi.

Nikiwa nina VVU/Ukimwi sitakiwi kubeba ujauzito: Unao uwezo wa kupata mtoto ili mradi viwango vya virusi (Viral load) ipo chini na imechungwa vyema ndani ya miezi sita. Wenza ambao mmoja wao ana maambukizi na mwingine hana, wanao uwezo wa kutumia njia ya tendo kwa ajili ya kupata ujauzito lakini wanatakiwa kuzingatia viwango vya virusi (viral load). Hivyo, unashauriwa kupima na kuongeza na washauri nasaa (Daktari) watakaofuatilia uwingi wa virudi na kukushauri muda muafaka wa kushika ujauzito.

Photo Credit: (David Bassey/MSU Reporter)  & Avert.org

 

Imesomwa mara 13466 Imehaririwa Jumapili, 08 Agosti 2021 22:21
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.