kupitisha damu nje ya moyo (Heart-Lung machine/ Extracorporal Circulation machine au Cardiopulmonary Bypass machine) na kuweza kufanya operesheni kwa kuupasua moyo na kurekebisha kasoro zilizo ndani yake. Hapa ndipo mapinduzi makubwa na maendeleo makubwa katika tiba yalianza kutokea. Hii ilikuwa ni mwaka 1953.
Upasuaji wa moyo wa kisasa ulianza na mabingwa wengi zaidi kujitokeza kama kina Dkt. Lillehei, Denton A. Cooley, Michael De Bakey, John Kirkin, Crafoord, Francis Fontan na wengineo wengi.
Mwaka 1967 operesheni ya kwanza ya ya upasuaji wa moyo duniani kwa kupandikiza/ kuweka moyo wa mtu mwingine (Heart Transplant) ulifanyika huko nchini Afrika Kusini na Dkt. Christian Barnard. Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1968, operesheni ya kwanza duniani ya upasuaji wa moyo kwa kumuwekea mgonjwa moyo wa bandia (Artificial Heart Transplant) ilifanywa na Dkt. Denton Cooley (mwalimu wangu na mwanzilishi wa Texas Heart Institute) mjini Houston, Texas, Marekani.
Kufanyika na kufanikiwa kwa upasuaji huu kulileta changamoto na maendeleo makubwa katika tiba kwa ujumla na hasa katika tiba ya moyo na upasuaji wa moyo. Kwa hivi sasa, sayansi ya tiba ya moyo imekua kiasi kwamba leo hii tupo kwenye upasuaji wa kutumia mirija (catheterization/ Angioplasty), kwa kukata kidogo bila kuharibu mwili au moyo (minimally Invasive Surgery) na kwa kutumia vifaa bandia (Robbotic Surgery).
Lakini pamoja na maendeleo haya duniani, Bara letu la Afrika ikiwemo nchi yetu Tanzania sayansi hii inaonekana ni kama ndoto. Kuna kila haja ya kufanya juhudi za ziada ili bara letu na hasa nchi yetu ya Tanzania iweze kufikia hapo wenzetu walipofikia. Tazama takwimu za upasuaji wa moyo zilizivyo duniani katika karne hii ya 21.
Takwimu za upasuaji moyo duniani
Kama zilivyotolewa na Shirika na Moyo Duniani (World Heart Foundation) mwaka 2002
- Operesheni za moyo 860 kwa kila idadi ya watu milioni moja hufanyika Marekani ya Kaskazini, Australia na Ulaya
- Operesheni zamoyo 60 kwa kila watu milioni moja hufanyika Amerika ya Kusini, Urusi, Asia na Afrika
- Hii inamaanisha kuwa takribani 93% ya watu wanaohitaji huduma ya upasuaji wanaoishi nje ya Amerika, Australia na Ulaya hawapati huduma hii
- Kwa takwimu halisi ni kwamba, watu karibu bilioni 4.5 duniani hawafikiwi na huduma ya upasuaji wa moyo duniani.
Changamoto ya Uwezo wa Upasuaji wa Moyo
Teknolojia hii ina changamoto zake kadhaa zikiwemo
- Ni sayansi ya kisasa zaidi, hivyo
- Ina gharama – vifaa ni aghali sana, na
- Kuna upungufu wa wataalamu, ambao kwa upande fulani husababishwa na
- Kutokana na kukosa mtazamo
- Kuanisha mradi mpya hakuwavutii wafadhili/ wakopeshaji kwa vile faida huchukua muda mrefu zaidi kupatikana kama miaka zaidi ya mitano, na
- Mgongano wa maslahi kama vile kitendo cha kupeleka wagonjwa nje ya nchi huwanufaisha sana baadhi ya watu, lakini pia
- Ni ngumu kwa watu wa kawaida kumudu gharama za tiba ya upasuaji wa magonjwa haya
Dkt. Ferdinand B. Masau ni Daktari Bingwa wa Tiba na Upasuaji wa Moyo katika Taasisi ya Moyo Tanzania (THI). Makala hii inapatikana pia katika kitabu chake cha “Magonjwa ya Moyo, Yajue, Yazuie na Yatibu”.