Image

Kichocho ni zaidi ya kukojoa.Unaambukizwaje na namna gani unaweza kujilinda nao?

Bila shaka umewahi kuusikia ugonjwa uitwao kichocho (bilharzia/schistosomiasis). Je unajua kuwa kichocho ni zaidi ya kukojoa damu tu? Unajua unaambukizwaje na namna gani unaweza kujilinda nao?

Katika makala hii tutajifunza kwa undani kuhusu Kichocho, jinsi kinavyoenezwa, dalili, tiba, madhara ya muda mrefu na jinsi ya kujilinda usiupate.

Kichocho ni nini?

Kichocho ni ugonjwa wa vimelea unaosababishwa na minyoo (trematoda) inayojulikana kama schistosoma.

 Kwa makadirio takribani watu milioni 230 duniani kote wameambukizwa na Schistosoma. (Colley, 2014, )

Kichocho ni chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo kwa nchi zinazoendelea.

 

 Baada ya malaria, huenda ikawa maambukizi ya vimelea yanayoathiri binadamu kwa uzito zaidi, ikiwa ni endemiki katika takriban nchi 78 na inaathiri takriban watu milioni 240 kila mwaka barani Afrika, Asia, Amerika Kusini, na visiwa vya Karibiani. (Editors of encyclopaedia Britannica ,2024)

 Aina za kichocho

Kuna aina kuu mbili za kichocho:

  1. Kichocho cha utumbo ( intestinal schistosomiasis)

 

  1. Kichocho cha mfumo wa mkojo na mfumo wa uzazi ( urogenital schistosomiasis)

Schistosomiasis ya mfumo wa uzazi kwa wanawake ni moja ya magonjwa ya uzazi ambao ni matokeo ya maambukizi ya vimelea vya Schistosoma haematobium na unaathiri angalau wanawake milioni 40, hasa katika Afrika ya Kusini mwa Sahara.(Mazigo HD ,2022)

Maambukizi ya kichocho

Kichocho kwa kawaida huambukizwa kwa kufanya kazi, kuoga, au kuogelea katika maji yenye konokono wanaobeba minyoo ya schistosoma. Minyoo hiyo hupenya kwenye ngozi ya binadamu na kuingia mwilini ambapo hukua kua minyoo wakubwa.Minyoo ya schistosoma  hukaa kwenye mishipa ya damu ya binadamu kwa miaka mingi, ikiweza kuiepuka mifumo ya kinga za mwili wakati huo wote minyoo hiyo hutoa mamia hadi maelfu ya mayai kila siku, baadhi ya mayai hutolewa nje ya mwili kupitia kinyesi au mkojo ili kuendeleza mzunguko wa maisha ya vimelea. Mayai mengine yanakwama kwenye sehemu mbalimbali za mwili, na kusababisha mwitikio wa kinga za mwili na kusababisha uharibifu wa viungo vya mwili.

                   

FIG: Mzunguko wa maisha ya minyoo ya schistosoma.

Dalili za kichocho

  1. Dalili za awali / Acute (katayama fever/syndrome)

Hatua hii husababishwa na mzio (allergic reaction) inayosababishwa na minyoo na/au mayai yao. Dalili hutokea kuanzia wiki 2 hadi 8 baada ya kukutana na maji yaliyoathiriwa.

 Dalili zinaweza kujumlisha:

  1. Maumivu ya tumbo
  2. kikohozi,
  3.  Homa hasa wakati wa  jioni/usiku
  4. Upele na kuwashwa ngozi (cercarial dermatitis/ swimmer's itch)
  5.  Maumivu ya ini.( sehemu ya tumbo ya juu kulia)
  6. Damu katika kinyesi na mkojo katika hatua kali zaidi.

 

2) Dalili za kichocho sugu / chronic

Wagonjwa wenye schistosomiasis sugu huweza kuanza kuonyesha dalili miezi mpaka miaka baada ya kukutana na maji yaliyo athiriwa na minyoo ya schistosoma. Dalili zake hutegemeana na sehemu ya mwili zilizo athirika.

  1. Dalili za ujumla
  • Uchovu wa mwili
  • Maumivu ya tumbo
  • Kuharisha / kuharisha damu
  1. Dalili za mfumo wa mkojo
  • Maumivu wakati wa kukojoa
  • Kukojoa mara kwa mara
  • Kukojoa mkojo wenye damu hasa wakati wa kumaliza kukojoa.
  1. Dalili za Mfumo wa kizazi (kwa wanawake)
  • Kutokwa na damu baada ya kujamiana
  • Vidonda vya ukeni
  • Hedhi isiyo ya kawaida ( irregular)
  • Maumivu ya nyonga
  • Dalili za moyo na mapafu

                              -  Kikohozi au/na kukohoa damu

                              - Kubanwa kifua

                              - Homa

                              - Kuchoka haraka na mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida

                              - Kupumua kwa shida wakati wa kufanya kazi

  • Dalili za ubongo na mishipa ya fahamu
  • Maumivu ya kichwa
  • kizunguzungu
  • Degedege
  • kupooza kutokana na mayai kuathiri uti wa mgongo

                 

Vipimo na Tiba

Vipimo vya kichocho vinategemea na dalili na aina ya kichocho, vinaweza kua :

  1. Kipimo cha mkojo au/na choo kikubwa (kinyesi) ili kuangalia mayai ya minyoo hiyo
  2. Kipimo cha damu ( full blood picture)
  3. Ultrasound ( tumbo, pelvic)
  4. X-ray ( tumbo, kifua)
  5. Uchunguzi wa kibofu cha mkojo kwa kutumia cystoscope
  6. CT scan , MRI kwa ajili ya kugundua maambukizi ya ubongo na uti wa mgongo

Matibabu makuu ya kichocho ni dawa ya kuua vimelea mwili ambayo ni dozi ya mara moja, lakini unaweza kupewa dawa zingine kuligana na dalili zako.

Mfano: dawa za allergy, dawa za kushusha homa, dawa za kuzuia degedege n.k

Madhara ya  kichocho

  1. Kifafa au degedege
  2. Tumbo kujaa maji(ascites) na kutapika damu (  husababishwa na  portal hypertension)
  3. Saratani ya Kibofu cha mkojo
  4. Kuvuja damu katika mfumo wa chakula ( gastrointestinal bleeding)
  5. Ugonjwa wa mapafu na moyo unaoweza kupelekea moyo kushindwa kufanya kazi vizuri
  6. Kupooza
  7. Schistosomiasis sugu ya mfumo wa uzazi imehusishwa na ugumba, ujauzito wa nje ya mfuko wa uzazi ( ectopic), kuharibika kwa mimba, kujifungua kabla ya wakati, na uzito mdogo wa watoto wachanga.(Mazigo HD ,2022)
  8.  Zaidi ya hayo, ushahidi unaoongezeka unaonyesha kwamba Schistosomiasis ya mfumo wa uzazi kwa  Wanawake huongeza hatari ya kupata virusi vya ukimwi (HIV) na HPV/Saratani ya shingo ya kizazi.(Mazigo HD ,2022)

Hitimisho

Tunaweza kuepuka kuugua kichocho kwa

  1. kuepuka kuogelea au kuoga katika mabwawa, mito, maziwa na madimbwi.
  2. Lakini pia watu wote wanaofanya kazi katika vyanzo vya maji baridi au maji yaliyo tuama ( wavuvi, wakulima wa mpunga nk) watumie nyenzo za kujikinga kama gloves na boots.
  1. Watu wanaotumia maji ya mto / ziwa kufanyia shughuli mbalimbali (kama kufua, usafi wa majumbani,kuoga,) watibu maji hayo kabla ya kutumia ( kuchemsha au kwa dawa)

Pata matibabu mapema unapokuwa na dalili za kichocho na tumia dawa kama utakavyoelekezwa na mtoa huduma wa afya ili kuepuka kichocho sugu na madhara yanayotokana na kichocho.

Marejeleo

  1. Medscape
  2. Human schistosomiasis
    Colley, Daniel G et al.
    The Lancet, Volume 383, Issue 9936, 2253 - 2264
  3. Britannica, T. Editors of Encyclopaedia (2024, August 6). schistosomiasis. Encyclopedia Britannica. https://www.britannica.com/science/schistosomiasis
  4.  Mazigo HD, Samson A, Lambert VJ, Kosia AL, Ngoma DD, Murphy R, et al. (2022) “Female genital schistosomiasis is a sexually transmitted disease”: Gaps in healthcare workers’ knowledge about female genital schistosomiasis in Tanzania. PLOS Glob Public Health 2(3): e0000059. https://doi.org/10.1371/journal.pgph.0000059
Imesomwa mara 383 Imehaririwa Jumanne, 20 Agosti 2024 14:23
Dr Ladina Msigwa

Distinguished medical doctor and acclaimed author with a passion for enhancing healthcare and sharing knowledge through the written word.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana