Image

Mambo ya kuzingatia unapogundulika kuwa na maambuki ya virusi vya ukimwi

Nimekutana na jamii ya watu wengi kwenye utumishi wangu kama daktari ambao wanaamini kuwa ukigundulika una maaambukizi ya VVU/UKIMWI basi maisha yameishia hapo na  hakuna tumaini tena.

Leo nimekuletea habari njema kuwa dhana ya kwamba hakuna maisha baada ya maambukizi ni uongo.

Wapo watu wengi sana wanaofurahia maisha pamoja na familia zao licha ya kwamba wanaishi na maambukizi ya VVU/UKIMWI.

Twende pamoja nami kwenye makala hii ili uweze kutambua mambo ya kuzingatia pindi unapogundulika kuwa umepata  maambukizi ya VVU/UKIMWI. 

HONGERA! Kwa kupima na kujua afya yako.

Jambo la kwanza la kufanya ukingundulika kuwa una maambukizi ni kukubali matokeo au hali halisi ya majibu ya vipimo. Na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mtoa huduma.

Mtoa huduma baada ya kukupa ushauri nasaha  kulingana na miongozo ya matibabu ya VVU/UKIMWI atakuanzisha dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI.

Zingatia!!

Ni muhimu sana kujisajili na kuhudhuria katika kliniki za CTC zilizopo kwenye takribani vituo vyote vya afya ili taarifa zako na maendeleo yako yaweze kuafuatiliwa kwa ukaribu na wahudumu wa afya. Ukijisajili utapewa kadi ya CTC yenye namba yako ya usajili na inayoonyesha mahudhurio, dawa unazotumia, kiwango cha virusi mwilini (viral load) na wingi wa chembechembe nyeupe za damu zinazohusika na kinga ya mwili yaani CD4

Kuwa na mahudhurio mazuri kwenye kliniki za CTC kadri unavyoelekezwa na daktari ni jambo la msingi sana kwani wahudumu wa afya wataweza kufuatilia kwa karibu maendeleo ya afya yako, madhara yatokanayo na dawa za kufubaza virusi vya VVU/UKIMWI na kuangalia kama dawa ulizopewa zinakusaidia kupata nafuu au la nk.

Matumizi sahihi ya dawa ya kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV) -Dawa hizi mgonjwa humeza kila siku kulingana na maelekezo ya daktari.

Kama wewe ni msahaulifu ni vizuri kumtumia mtu wa karibu nawe (mwenza au ndugu katika familia au rafiki) kukusaidia kukukumbusha endapo umesahau kumeza dawa au utumie APP yetu ya Tanzmed ambayo inapatikana kwenye play store ambayo unaweza weka taarifa zako nayo ikakumbusha muda wa kumeza dawa.

Kumbuka kwamba dawa hizi hazitibu virusi vya VVU/UKIMWI bali hufubaza makali ya virusi hivyo, husaidia kuongezeka kwa kinga ya mwili wako, hupunguza au kuondoa kabisa magonjwa nyemelezi na kuboresha hali ya maisha ya  mgonjwa. Ni muhimu sana kwa mgonjwa wa UKIMWI kuzingatia matumizi ya dawa hizi kwa kufuata maelekezo ya daktari  bila kukosa.

Lishe na mazoezi

Madawa ya kufubaza virusi vya UKIMWI yana nguvu sana hivyo huhitaji lishe nzuri na mazoezi. Pia ugonjwa wa UKIMWI  husababisha mwili kudhoofu kwa kupunguza  kinga mwilini na hivyo basi kuongeza mahitaji ya nishati mwilini, hupunguza hamu ya kula chakula, na uduni wa kufyonza virutubisho kwenye mwili.

Hivyo unashauriwa ule mlo kamili wenye virutubisho vyote ile kusaidia kujenga mwili vizuri.

Lishe ya mgonjwa wa UKIMWI  huzingatia  umri wa muhusika, hali ya ujauzito au kama ananyonyesha.Pia lishe hutegemea kama mgonjwa wa UKIMWI ana  magonjwa nyemelezi na hatua ya ugonjwa (stage) na wingi wa virusi vya VVU mwilini (viral load).

Lishe bora kwa wagonjwa wa UKIMWI inahusisha virutubisho kama  wanga, protini,mafuta, vitamin na madini aina mbalimbali.

Tafiti zinasema kama una maambukizi na huna dalili yoyote unatakiwa kutumia lishe  asilimia 10 zaidi ya mtu ambaye hana maambukizi, na kama una dalili inabidi kutumia lishe asilimia 20-30 ya mtu asiye na maambukizi wa rika moja, jinsia moja na shughuli za mwili zinazofanana. Endelea kuwa nasi kupata makala inayohusu lishe na UKIMWI.

Kujiepusha na tabia hatarishi za ugonjwa wa VVU/UKIMWI.

Kuna dhana mtaani kwamba kama nimepata maambukizi ya VVU/UKIMWI basi na mimi nastahili  kuambukiza  wengine. Dhana hii ni potofu sana.

Pindi unapogudulika na maambukizi ya VVU/UKIMWI inabidi uzigatie namna zote za kuzuia kueneza ugojwa huu hatari na kuwa msitari wa mbele kuelimisha na kulinda jamii inayokuzunguka.

Mfano wa tabia hatarishi ni;

Kushiriki ngono zembe bila kinga

Kuwa na wapenzi zaidi mmoja

Kuchangia vitu vyenye incha kali kama sindano, viwembe n.k na

Kutokutumia dawa za kufubaza virusi vya VVU/UKIMWI kama ulivyoelekezwa na dakari.n.k

kama ulikuwa na ulevi wa pombe unashauriwa kuacha mara moja  kwani unywaji wa pombe kupindukia huongeza uwezekano wa  kupata magojwa mbalimbali ikiwemo kifua kikuu,nimonia na homa ya ini na pia huongeza madhara kwenye ubungo kwa watu wenye maambukizi ya VVU/UKIMWI. Kama ni muathirika wa madawa ya kulevya hakikisha unaanza kliniki za methadone kwa ajili ya matibabu na kujiepusha kuchangia kujidunga sindano.

Mama mjauzito

Inawezekana ulikuwa unafikiri kama mimi ni mjamzito JE nafanyaje?

Nikupe hongera kwa sababu sasa unaweza pata mimba na kujifungua mtoto asiye na maambukizi kwa kufuata maelekezo kutoka kwa wahudumu wa afya ukiwa kliniki.

Jambo la kwanza ni kuanza kliniki mapema ambapo vipimo vitarudiwa tena na utaanzishiwa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV) mara tu baada ya kukubali na kupata ushauri nasaha.

Mambo yote tajwa hapo juu ni  muhimu kuyazingatia hata kama ni muathirika wa VVU/UKIMWI ni mjamzito. Matumizi ya madawa ni muhimu sana maana yatafubaza virusi na kupunguza uwezekano wa mtoto kupata maambukizi akiwa kwenye mfuko wa uzazi. Pamoja na hilo inabidi kuzingatia lishe bora kama ambavyo utaelekezwa na dakatri. Kwa maana mahitaji yako ya lishe yako tofauti na makundi mengine.

Pia inabidi kufanya mahudhurio mazuri kliniki na kuhakikisha unajifungulia kwenye kituo cha afya na sio nyumbani ili upate huduma sahihi na salama kwa mtoto wakati wa kujifungua ikiwemo dawa za kumkinga mtoto asipatae maambukizi ya virusi vya VVU/UKIMWI.

Ukizingatia hayo machache na mengi kutoka kwenye vituo vya afya basi utaweza kuishi maisha marefu yenye furaha na kuendelea na shughuli zako kama kawaida.

 

 

 

Imesomwa mara 5917 Imehaririwa Jumapili, 08 Agosti 2021 22:22
TanzMED Admin

TanzMED ni mjumuiko wa wataalamu wa fani mbalimbali za Afya na IT wa kitanzania ambao wamejitoa katika kuhakikisha kuwa jamii ya kitanzania na Afrika kwa ujumla inafaidika kwa kupata habari na ushauri juu ya masuala ya afya yanayozunguka jamii hizo.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.