Je mkanda wa jeshi unaambukizwa?
Hapana ugonjwa huu hauambukizwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine! Lakini iwapo itatokea mtoto au mtu mzima ambaye hajawahi kupatwa na ugonjwa wa tetekuwanga maishani mwake na ambaye pia hajawahi kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo akakutana na mtu mwenye ugonjwa wa mkanda wa jeshi, mtoto au mtu huyo atapatwa na ugonjwa tetekuwanga na siyo mkanda wa jeshi.
Dalili
Dalili ya awali kabisa ya mkanda wa jeshi ni maumivu makali sehemu fulani/ upande mmoja wa mwili yakiambatana na hali ya ganzi na hisia za kuungua kwenye ngozi. Maumivu pamoja na hisia za kuungua huwa makali sana na hutokea kabla ya vipele/michubuko kutokea kwenye ngozi.
Kawaida, vipele au michubuko huusisha eneo fulani la mwili kuanzia kwenye uti wa mgongo kuzunguka kuelekea eneo la tumbo au kifua. Michubuko pia inaweza kutokea kwenye maeneo yanayozunguka uso, macho, mdomo au masikio.
Dalili nyingine ni pamoja na
• Maumivu ya tumbo
• Homa
• Maumivu ya mwili mzima
• Vidonda sehemu za siri
• Maumivu ya kichwa
• Maumivu ya viungo
• Kuvimba kwa mitoki/ matezi
Iwapo neva za maeneo ya uso zitaathiriwa, mgonjwa anaweza kupatwa na matatizo ya kuona, kuonja, au kusikia.
Vipimo
Ni nadra sana kufanya Vipimo maalum kwa ajili ya utambuzi wa ugonjwa huu, isipokuwa kwa nchi zilizoendelea. Kwa ujumla utambuzi wa ugonjwa huu hufanyika kwa kuchukua historia ya mgonjwa na kuchunguza sehemu ya ngozi iliyoathiriwa.
Vipimo vya damu yaani FBP huonesha ongezeko la chembe nyeupe za damu na antibodies dhidi ya virus wa tetekuwanga.
Matibabu
Matibabu ya mkanda wa jeshi hujumuisha matumizi ya dawa kama vile Acyclovir, Famciclovir na Valacyclovir kwa ajili ya kuua virus wanaosababisha ugonwja huu. Dawa hizi husaidia kupunguza maumivu, kuzuia madhara zaidi ya ugonjwa huu na kupunguza muda wa ugonjwa.
Dawa hizi hutolewa angalau saa 72 baada ya mgonjwa kuanza kuhisi maumivu na hali ya kuungua. Ni vema dawa zianze kutumika kabla ya vipele/michubuko kujitokeza.
Jamii ya dawa za corticosteroids kama vile prednisolone husaidia kupunguza maumivu na uvimbe kwa badhi ya wagonjwa. Dawa nyingine zinazofaa kutumika ni pamoja na jamii ya antihistamines kwa ajili ya kupunguza muwasho, dawa za maumivu, calamine lotion kwa ajili ya kupunguza muwasho. Aidha mgonjwa anashauriwa kupata mapumziko ya kutosha
Matarajio
Mkanda wa jeshi kwa kawaida huchukua kati ya wiki mbili hadi tatu kupona wenyewe. Aidha ni nadra sana kwa ugonjwa huu kujirudia tena. Iwapo neva zinazothibiti mwendo katika mwili zitakuwa zimeathirika, mgonjwa anaweza kupatwa na kupooza kwa muda au kwa kudumu kwa sehemu ya mwili iliyoathiriwa. Wakati mwingine, maumivu yanayosababishwa na mkanda wa jeshi yanaweza kudumu kwa miezi mpaka mwaka hata baada ya mgonjwa kupona kabisa. Maumivu haya yanayojulikana kama postherpetic neuralgia kwa kawaida huwakumba wagonjwa wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na husababishwa na uharibifu katika neva za mwili.
Madhara
Madhara ya mkanda wa jeshi ni pamoja na kupatwa na shambulio jingine la ugonjwa huu, maambukizi ya bakteria, upofu iwapo eneo la jicho litahusika, ukiziwi, maambukizi katika utando wa ubongo (encephalitis), uwepo wa vimelea kwenye damu (sepsis) au ugonjwa unaoitwa Ramsay Hunt Syndrome iwapo utahusisha neva za uso.
Kinga
Epuka kabisa kugusa eneo lenye vipele au michubuko kwa mtu mwenye mkanda wa jeshi au tetekuwanga iwapo hujawahi kuugua au kupata chanjo ya tetekuwanga.
Ni vema kupata chanjo dhidi ya virus wa Varicella zoster kama inapatikana katika nchi au eneo ulilopo. Tafiti zimeonesha kuwa, watu wazima wanaopata chanjo hii wana uwezekano mdogo sana wa kupata madhara ya mkanda wa jeshi kuliko wale wasiochanjwa.