Gauti (Gout) ni aina ya ugonjwa unaoathiri viungo vya mwili unaosababishwa na kuwepo kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida cha tindikali ya Urea (uric acid) katika damu.
Ongezeko la uric acid husababisha madhara katika jointi (joint) (joint ni sehemu ya mwili inapokutana/ inapoungana mifupa miwili). Gauti inaweza kutokea ghafla (acute gout) au ikawa sugu (chronic gout). Gauti inayotokea ghafla huwa na maumivu makali na mara nyingi huathiri jointi moja tu wakati gauti sugu inaweza kuathiri jointi zaidi ya moja na huambatana na hali ya kujirudia ya maumivu na uvimbe kwenye jointi.
Visababishi
Gauti husababishwa na kuwepo kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida cha uric acid katika damu. Hali hutokea iwapo mwili wa mgonjwa unatengeneza uric acid nyingi kuliko kawaida au unashindwa kutoa uric acid mwilini kama inavyotakiwa.
Ongezeko hili husababisha mrundikano wa uric acid katika maji maji yanayozunguka jointi yanayoitwa synovial fluid na hatimaye kutengeneza vijiwe vidogo vidogo vya tindikali ya urea yaani uric acid crystals ambavyo husababisha jointi kuvimba na hatimaye kuathirika.
Vihatarishi (risk factors)
Ingawa chanzo hakieleweki vema, ugonjwa wa gauti hutokea kuwapata baadhi ya watu walio katika familia moja. Wanaume huathiriwa zaidi kuliko wanawake ingawa wanawake waliokoma kupata hedhi huathiriwa zaidi kuliko wale wanaoendelea kupata hedhi.
Aidha unywaji pombe unachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa ugonjwa huu pamoja na matumizi ya baadhi ya madawa kama vile dawa za kutoa maji mwilini ambazo kwa ujumla husababisha ongezeko la kiwango cha uric acid katika damu.
Vihatarishi vingine vya gauti ni pamoja na kuwa na ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya figo, unene uliopitiliza, ugonjwa wa sickle cell anemia au aina nyingine za upungufu wa damu, pamoja na saratani ya damu (leukemia).
Hali kadhalika, gauti inaweza kusababishwa na matumizi ya dawa ambazo utendaji wake kazi huingiliana na utoaji wa uric acid mwilini.
Dalili
- Dalili za gauti kwa kawaida uhusisha jointi moja au joint chache. Jointi zinazoathiriwa zaidi ni pamoja na kidole kikubwa ha mguuni, magoti, au kiwiko cha mguu.
- Wagonjwa huwa na maumivu yanayoanza kwa ghafla hususani nyakati za usiku. Mara nyingi mgonjwa hudai anasikia maumivu makali kama kitu kinachokata, kupwita au mifupa inayosagana.
- Jointi hubadilika na kuwa na joto, kuvimba na kuwa na nyekundu (hujionesha zaidi kwa watu wenye ngozi nyeupe). Kwa kawaida mgonjwa hulalamika maumivu makali ikiwa ataguswa kwenye jointi yenye matatizo.
- Shambulio linaweza kudumu kwa siku kadhaa kabla mgonjwa hajapata nafuu, lakini pia laweza kujirudia mara kwa mara.
- Pia mgonjwa anaweza kujihisi homa.
Baadhi ya wagonjwa hupata gauti sugu ambayo huwaletea madhara sugu katika jointi (chronic arthritis) hali ambayo husababisha mgonjwa kujihisi maumivu na muda mwingi kushindwa vizuri kutumia jointi zake. Wagonjwa wenye gauti kwa muda mrefu huwa pia na vinundu chini ya ngozi inayozunguka jointi zilizoathirika. Vinundu hivi kwa kitaalamu huitwa trophy na ni ishara ya muhimu kwa madaktari.
Vipimo
Vipimo vya gauti hujumuisha
- Kiwango cha uric acid katika damu. Hata hivyo, si kila aliye na kiwango kikubwa cha uric acid katika damu huwa na gauti.
- Kiwango cha uric acid katika mkojo
- Uchunguzi wa maji maji yanayozunguka jointi (synovial fluid) kuchunguza vijiwe katika jointi
- X ray ya jointi iliyoathirika
- Uchunguzi wa utando unaozunguka jointi (synovial biopsy)
Matibabu
Matibabu ya gauti hujumuisha matumizi ya dawa, lishe pamoja na mabadiliko katika mfumowa maisha wa mgonjwa.
Dawa hutumika mara tu mgonjwa anapopata shambulio la ghafla. Dawa hizo ni pamoja na
- Dawa za kutuliza maumivu kama vile codeine, paracetamol
- Dawa za kutuliza mcharuko mwili (nonsteroidal anti-inflammatory drugs (NSAIDs) kama vile ibuprofen (brufen), indomethacin (indocid), diclofenac n.k. Pia ni muhimu mgonjwa kumfahamisha daktari wake iwapo ana matatizo yasiyoendana na matumizi ya dawa hizi kama vile vidonda vya tumbo au mzio.
Dawa hizo husaidia kupunguza maumivu, uvimbe, na mcharuko mwili (inflammation). Baadhi ya madaktari huchoma sindano dawa ya corticosteroids kwenye jointi iliyoathirika kwa ajili ya kupunguza maumivu na uvimbe. Kwa kawaida maumivu huondoka saa 12 baada ya kuanza matibabu, na mgonjwa hupata nafuu kamili baada ya saa angalau 48.
Ili kupunguza kiwango cha uric acid katika damu, mgonjwa hupewa dawa za allopurinol au probenecid kila siku. Wagonjwa wanaotumia dawa hizi ni wale ambao hupata mashambulizi ya mara kwa mara ndani ya mwaka au wale ambao hupata mashambulia makali, wagonjwa waliopata madhara mkubwa kwenye jointi, wagonjwa walio na vinundu (trophy) au wagonjwa wenye vijiwe vya uric katika figo.
Lishe na mabadiliko katika mfumo wa maisha husaidia pia kuthibiti na kumuepusha mgonjwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya gauti. Njia hizi ni pamoja na:
- Kuacha kunywa pombe
- Kupunguza ulaji wa vyakula vyenye viasili vya purine (aina ya protini) kama vile nyama ya mbuzi, samaki jamii ya sardines na herring, nyama ya maini au figo, mkate mtamu, maharage yaliyokaushwa, njegere, baadhi ya aina za uyoga, spinachi, n.k.
- Thibiti pia ulaji wa nyama kwa kila mlo unaokula
- Jiepushe na matumizi ya vyakula vya mafuta kama vile ice creams, mayonise au vyakula vya kuokwa
- Kula kiasi kikubwa cha wanga
- Iwapo utaamua kupunguza uzito, hakikisha unapunguza kidogo kidogo kwa sababu upunguzaji wa kasi unaweza kusababisha vijiwe vya uric kujitengeneza katika figo
Matarajio
Wagonjwa wanaofuata masharti na ushauri wa daktari huweza kuishi maisha ya kawaida. Hata hivyo, ni vema kufahamu kuwa mara nyingi gauti ya ghafla hatimaye huwa gauti sugu.
Madhara ya gauti
- Gauti inaweza kusababisha matatizo sugu kwenye jointi (chronic gouty arthritis)
- Vijiwe katika figo
- Mrundikano wa uric acid unaoweza kusababisha ugonjwa sugu wa figo
Kinga
Kwa kawaida gauti haizuiliki, hata hivyo mgonjwa anashauriwa sana kujiepusha na vitu vinavyoweza kuchochea shambulizi na dalili za ugonjwa huu (rejea lishe na mabadiliko katika mfumo wa maisha hapo juu).