Wagonjwa wa Ukimwi huathiriwa sana na ugonjwa wa figo. Ugonjwa wa figo unaohusiana na Ukimwi (HIV-Associated Nephropathy au kwa kifupi HIVAN) unaweza kusababishwa na mashambulizi ya moja kwa moja ya VVU kwenye figo au madhara yanayotokana na matumizi ya madawa ya kurefusha maisha (ARVs).
Aidha wagonjwa wengi wa Ukimwi wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya figo kwa sababu ya kupungukiwa na maji mwilini kutokana na kichefuchefu na kutapika mara kwa mara, kupoteza chumvi mwilini, au lishe duni.
Ukubwa wa Tatizo
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Msango, Leonard(1) na wenzake katika hospitali ya Bugando, Mwanza ilionekana kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa walioandikishwa kuanza ARVs hospitalini hapo walikuwa na matatizo ya figo yaliyotokana na VVU. Ilionekana pia kuwa HIVAN iliwaathiri zaidi wanawake kuliko wanaume, wenye uzito mdogo, na wale waliokuwa na CD4 chini ya 200.
Huko nchini Marekani, HIVAN ni maarufu zaidi miongoni mwa wamarekani weusi wenye asili ya Afrika ikilinganishwa na wale wa asili nyingine; na hushika nafasi ya tatu kwa kusababisha magonjwa sugu ya figo (CRF) miongoni mwa watu wa jamii hiyo wenye umri wa kati ya miaka 20-64(2). Kwa ujumla HIVAN huchangia karibu asilimia 1 ya wenye ugonjwa sugu wa figo (CRF) nchini humo kila mwaka.
Kwa ujumla takwimu za dunia zinaonesha kuwa HIVAN huathiri zaidi vijana weusi, na takribani nusu ya wagonjwa wa HIVAN ni watumiaji wa madawa ya kulevya ya kujidunga(3).
Wanaume huathirika zaidi kuliko wanawake katika uwiano wa 10:1, wakati wastani wa umri wa watu wenye HIVAN ni miaka 33(4) ingawa HIVAN huwapata pia watoto(5).
Nini hutokea? (Pathofiziolojia ya ugonjwa)
Watafiti wameonesha uhusiano wa mashambulizi ya moja kwa moja ya VVU-1 kwenye figo. Pia kuna uhusiano mkubwa wa vinasaba na vyanzo vya kimazingira vinavyochochea kutokea kwa tatizo hili, hususani kwa watu weusi zaidi kuliko watu wa asili nyingine.
VVU-1 hushambulia zaidi chujio (glomeruli) pamoja na seli za kuta (epithelium) za mirija yake (renal tubules) kuliko sehemu nyingine yeyote ya figo. Hali hii husababisha kuharibika kwa chujio pamoja na mirija na kufanya kazi ya uchujaji uchafu pamoja na utengenezaji wa mkojo kuvurugika. Matokeo yake mkojo huwa na kiwango kingi cha protini kuliko kawaida (protenuria), chujio huwa na makovu (glomerulosclerosis) hali kadhalika nayo mirija (tubulointerstitial scarring).
Uhusiano wa Vinasaba
Mpaka sasa, haijulikani sababu hasa inayowafanya watu weusi kuathirika zaidi na HIVAN kuliko watu wa asili nyingine. Ifahamike kuwa, kwa ujumla watu weusi wanaongoza kwa kupata magonjwa mengine ya figo kama vile ugonjwa wa figo unaotokana na kisukari (diabetic nephropathy) au unaotokana na mcharuko mwili (systemic lupus erythematosus); hivyo basi kuna uwezekano mkubwa pia wa vinasaba kuchangia katika kufanya watu weusi kupata HIVAN.
Dalili na muonekano wa mgonjwa
Pamoja na kuwa na dalili zote za magonjwa ya figo (rejea makala zilizopita za ARF na CRF), wagonjwa wa HIVAN huwa pia na tabia/dalili zifuatazo
- Muonekano wa mgonjwa: Hupoteza kiwango kingi cha protein katika mkojo (zaidi ya gramu 3.5 kwa siku). Hupoteza pia kiwango kingi cha albumin (aina nyingine muhimu sana ya protini). Aidha huwa na kiwango kingi cha mafuta mwilini (hyperlipidemia). Pamoja na kupoteza sana proteini, wagonjwa wengi wa HIVAN hawana hali ya kuvimba miguu (edema). Huwa na shinikizo la damu la kawaida (tofauti na wagonjwa wa ARF au CRF ambao huwa na ongezeko la shinikizo la damu). Huwa na mrundikano usio wa kawaida wa urea au mazao mengine machafu yanayotokana na Nitrogen katika damu (azotemia).
- Muonekano wa figo katika Ultrasound au CT scan: Tofauti na wale wa CRF iliyosababishwa na vyanzo vingine ambao huwa na figo ndogo zilizosinyaa, wagonjwa wenye HIVAN huwa na figo zilizo na ukubwa wa kawaida au zilizovimba sana (kubwa kuliko kawaida).
- Muonekano wa figo katika biopsy: Figo huwa na makovu makovu katika chujio zake (Focal segmental glomerulosclerosis (FSGS) yanayoonekana katika darubini tu.
- Kiwango cha CD4+ T-cells cha mgonjwa: Kwa kawaida kiwango cha seli za CD4+ kwa wagonjwa wenye HIVAN huwa chini ya 200 cells/µL. Hata hivyo, HIVAN inaweza kutokea hata kwa mgonjwa mwenye kiwango cha juu cha CD4. Wagonjwa wenye CD4 chini ya 50 cells/µL wana hatari zaidi ya kufa mapema kutokana na HIVAN.
Vipimo na uchunguzi
- Kipimo cha mkojo (urinalysis): Pamoja na kuonesha kiwango cha juu cha protini katika mkojo, kipimo hiki pia huonesha damu katika mkojo, chembe nyeupe za damu, vipande vidogo vinavyojulikana kama casts pamoja na chembechembe za mafuta.
- Vipimo vya utendaji kazi wa figo (renal function tests)
- Vipimo vya kuchunguza uwiano wa madini mwilini (electrolytes analysis): Kwa sababu ya mrundikano wa maji mwilini, wagonjwa wenye HIVAN huwa na upungufu wa madini ya sodiam (hyponatremia) na ongezeko la madini ya potassiam (hyperkalemia). Hali hii ni hatari kwa utendaji kazi wa viungo vya mwili hususani moyo kwa vile inaweza kusababisha shambulio la ghafla la moyo na hatimaye kifo kwa mgonjwa.
- FBP kwa ajili ya kuchunguza wingi wa damu, kiwango cha seli mbalimbali za damu na uwepo wa magonjwa mengine yanayomuathiri mgonjwa.
- Kipimo cha Renal Biopsy: Kipimo hiki husaidia kuthibitisha na kutofautisha HIVAN na vyanzo vingine vya CRF. Aidha madaktari wengi hupenda kufanya biopsy kwa wagonjwa wanaopoteza zaidi ya gramu 1 ya protini kwa siku kupitia kwenye mkojo.
Vipimo vingine
- Ultrasound ya figo, mirija pamoja na kibofu cha mkojo
- CT ya figo
- Kiwango cha CD4 pamoja na wingi wa VVU (viral load).
Matibabu
Matibabu ya HIVAN yanajumuisha matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARVs) kwa wale ambao bado hawajaanza kutumia dawa hizo, kurekebisha au kubadilisha aina ya dawa za ARVs kwa wale ambao tayari wamekwisha anza kutumia ili zisimdhuru mtumiaji, na matumizi ya dawa nyingine kama invyoelezwa hapa chini.
- Matumizi ya dawa za jamii ya Angiotensin-converting enzyme (ACE) inhibitors: Baadhi ya tafiti zimeonesha kuwa matumizi ya dawa ya Captopri kwa wagonjwa wa figo husaidia kuongeza muda wa figo kufanya kazi kwa wastani wa kati ya mwezi mmoja mpaka sita(6), wakati dawa ya fosinopril ilisaidia kuongeza muda wa kufanya kazi wa figo kwa wastani wa miezi 16(7).
- Matumizi ya dawa za kupunguza mcharuko mwili na mzio (Corticosteroids): Dawa zinazotumika ni pamoja na predinisolone. Dawa hizi husaidia kupunguza kitendo cha mcharuko mwili/mzio katika nyama za figo na hivyo kuliepusha na madhara zaidi.
Matibabu mengine
Matibabu mengine ni kama yalivyoelezwa kwenye makala ya ugonjwa sugu wa figo.
Matarajio
Ilionekana huko nyuma kuwa, kabla ARVs hazijaanza kutumika rasmi, kasi ya mgonjwa mwenye HIVAN kupata ugonjwa sugu wa figo ilikuwa ni wastani wa miezi miwili na nusu tu. Lakini tangu kuanza kwa matumizi ya dawa hizo, kumekuwepo mabadiliko makubwa na hata kupungua kwa kiasi kikubwa kwa kasi ya HIVAN kuelekea kwenye CRF.
Kasi inapungua zaidi iwapo mgonjwa atatumia ARVs pamoja na dawa za jamii angiotensin-converting enzyme inhibitors (captopril, fosinopril).
Marejeo
- Renal dysfunction among HIV-infected patients starting antiretroviral therapy in Mwanza, Tanzania. Leonard Msango et al.. AIDS 52 Suppl (1):1 (2011)
- Schwartz EJ, Klotman PE. Pathogenesis of human immunodeficiency virus (HIV)-associated nephropathy. Semin Nephrol. Jul 1998;18(4):436-45.
- Rao TK. Human immunodeficiency virus (HIV) associated nephropathy. Annu Rev Med. 1991;42:391-401.
- Carbone L, D'Agati V, Cheng JT, et al. Course and prognosis of human immunodeficiency virus-associated nephropathy. Am J Med. Oct 1989;87(4):389-95.
- Ray PE, Xu L, Rakusan T, et al. A 20-year history of childhood HIV-associated nephropathy. Pediatr Nephrol. Oct 2004;19(10):1075-92.
- Kimmel PL, Mishkin GJ, Umana WO. Captopril and renal survival in patients with human immunodeficiency virus nephropathy. Am J Kidney Dis. Aug 1996;28(2):202-8.
- Wei A, Burns GC, Williams BA. Long-term renal survival in HIV-associated nephropathy with angiotensin-converting enzyme inhibition. Kidney Int. Oct 2003;64(4):1462-71.