Image

Ugonjwa wa contact dermatitis

Ni tatizo la ngozi ambalo linaifanya ngozi kuwa nyekundu, kuvimba/kuwasha au kupata mcharuko (inflammation) baada ya kugusana na kitu kinachochangia mwili kucharuka au kupata mzio (allergic reaction)

Kuna msomaji mmoja aliuliza swali kwenye tovuti hii, na hapa na nukuu swali lake ‘’ Nina tatizo la kutoka vipele sehemu za siri siku moja baada ya kufanya mapenzi au baada ya "masterbartion". Vipele hukaa siku tatu hadi nne hutumbuka na kutoa maji, kidonda hukauka siku moja hadi mbili bila dawa. Nimepima ukimwi pamoja na kaswende lakini halikuonekana tatizo. Naomba msaada kujua tatizo langu’’ Mwisho wa kunukuu.

Contact dermatitis husababishwa na nini?

Vitu vinavyosababisha mtu kupata mzio (allergy) kama baadhi ya sabuni, mimea kama poison ivy or poison oak, manukato, vito na nk. Baadhi ya kazi pia huchangia mtu kugusana na vitu vinavyomfanya  mtu kupata mcharuko mwili au mzio.

Kuna aina tatu za contact dermatitis

  • Irritant contact dermatitis
  • Allergic contact dermatitis
  • Photocontact dermatitis

Irritant contact dermatitis

Aina hii ndio huonekana sana kwa wagonjwa na husababishwa kugusana na vitu kama

Tindikali

  • Kemikali aina ya alkali kama sabuni za kuogea, sabuni za kufulia aina ya detergents, vilainishi nguo (fabric solvents), na aina mbalimbali za kemikali
  • Sementi, rangi za nywele (Hair dyes), dawa za kuulia magugu, rubber gloves, shampoos, kukaa na pampers kwa muda mrefu hasa watoto.
  • Pombe, turpentine,mafuta ya taa.

Aina hii huonekana sana kwenye mikono  kwa sababu mara nyingi mikono ndio hutumbukizwa kwenye sehemu iliyo na visababishi vya irritant contact dermatitis.

Allergic contact dermatitis

Aina hii husababishwa kwa mtu kugusana na kitu/vitu ambavyo mtu anapata mzio pindi tu anapogusana navyo (sensitive). Vitu hivyo vinavyochangia mtu kupata aina hii ya allergic contact dermatitis ni;

  • Gundi
  • Dawa za antibayotiki kama neomycin pindi itakapogusana na ngozi ya mhusika
  • Aina mbalimbali ya vitambaa na nguo
  • Manukato kwenye sabuni, vipodozi, moisturizers na marashi
  • Virutubisho aina ya balsam of peru vinavyotumika kwenye baadhi ya vyakula na vinywaji
  • Madini aina ya nickel, dhahabu, rangi aina ya chromium, baadhi ya rangi za mafuta kutoka kwenye mimea
  • Baadhi ya madini ya chuma yanayopatikana kwenye vifungo vya nguo, vya brasia, visu vya kuweka mfukoni (pocket knife), mikanda ya saa nk.
  • Baadhi ya mimea kama poison ivy, poison oak na poison sumac
  • Gloves za mipira (rubber gloves), latex gloves au viatu.

Photocontact dermatitis -Husababishwa kwa mhusika kugusana na vitu ambavyo haviathiri mwili wa mtu ila tu baada ya kukumbana na miale ya ultraviolet light (320-400 nm UVA) ndipo sehemu ile hupata mcharuko mwili au mzio.Mara nyingia aina hii ya dermatitis huonekana kwenye sehemu za mwili ambazo hazizibwi na nguo kama vile kwenye mapaja (kwa kina dada wanaopenda kuvaa nguo fupi),sehemu ya miguu chini ya magoti nk.

Dalili za ugonjwa huu ni

  • Vipele vyekundu
  • Malengelenge,wheels au urticaria
  • Ngozi kukauka, kukatika au kuwa na mabaka baka mekundu kama mtu aliyeungua kwa moto
  • Maumivu ya sehemu husika
  • Kuwasha na kuungua kwa ngozi- Irritant contact dermatitis huwa ina maumivu makali sana kuliko muwasho wa sehemu husika wakati allergic contact dermatitis huambatana na kuwashwa kwa sehemu husika.

Kipimo cha uchunguzi

Skin allergy test-Kipimo ambacho hutambua vitu vinavomsababishia mtu kupata mzio.

Tiba ya Contact Dermatitis

Tiba ya ugonjwa huu ni mtu kutafuta kisababishi cha tatizo hili na kukiepuka

Calamine lotion hutumiwa ili kupunguza muwasho na athari za mzio

Dawa za  vidonge za kuzuia mzio kama oral antihistamine zinaweza kutumika

Corticosteroid cream zinaweza kutumika kupunguza athari za mzio

Je, mtu anapopata mzio afanyaje?

Pindi tu utakapopata mzio au mcharuko mwili kutokana na kisababishi unachokijua/kutokujua, osha sehemu husika kwa sabuni na maji baridi ili kupunguza athari yake

Kama umetoka malengelenge, weka kitu  cha baridi/barafu kwenye sehemu husika kwa muda wa nusu saa mara tatu kwa siku ili kupunguza malengelenge.

Epuka kukuna sehemu iliyoathirika kwani kujikuna huchubua/hupasua ngozi na kukasababisha maambukizi ya bakteria

Imesomwa mara 10024 Imehaririwa Alhamisi, 24 Oktoba 2019 13:42
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.