Image

Parachichi Kinga ya Sumu Mwilini na Kuzeeka

Kwa muda mrefu sana wanawake wamekuwa wakitumia parachichi kama nyenzo mojawapo ya urembo ima kwa kupaka kwenye uso au nywele bila kuwa na uhakika kama kweli parachichi husaidia katika kurutubisha nywele na ngozi ya kwenye uso.

Swali ni je ni wangapi wanajua faida za parachichi kiafya, hususani faida ya kuukinga mwili dhidhi ya kemikali hatari pamoja na kumfanya mtu kuonekana kijana?

Wanasayansi wa chuo kikuu cha Michoacana de San Nicolas de Hidalgo cha nchini Mexico wamesema ya kwamba parachichi husaidia katika kuukinga mwili dhidhi ya kemikali hatari (free radicals) na hivyo kuweka kinga dhidhi ya magonjwa mengi pamoja na kumfanya mtu kuonekana kijana (fight against ageing). Wanasayansi hao wamesema kwamba mafuta yanayopatikana katika parachichi yanauwezo wa kupenya hadi ndani ya injini inayotengeneza nishati mwilini inayopatikana katika seli inayojulikana kama mitochondria.

Free radicals ni kemikali zinazosababisha magonjwa mengi yakiwemo baadhi ya saratani, huharibu mishipa ya damu ya ateri (arteries), pamoja na kumfanya mtu kuzeeka haraka. Mafuta yanayopatikana katika baadhi ya mboga za majani, matunda na nyanya/tungule (tomatoes) yanauwezo wa kupambana na kemikali hizi hatari lakini mafuta haya hushindwa kuingia ndani ya mitochondria ambapo ndio kuna kemikali hizi hatari kwa wingi.

Mtafiti Christian Cortes-Rojo kutoka chuo kikuu hicho cha Mexico ambaye ndiye alifanya utafiti huu, alisema ‘’Anti-oxidants zinazopatikana katika mboga za majani na matunda mengi haziwezi kupenya ndani ya mitochondria na hivyo kushindwa kudhibiti kemikali hatari ndani ya mitochondria hizo. Hivyo kusababisha kemikali hizo hatari kuendelea kushambulia mitochondria na kuziharibu, matokeo yake ni kuwa nishati haitolewi tena kutoka kwenye mitochondria na seli hushindwa kufanya kazi na kufa.”

Matokeo ya utafiti huu yalitolewa katika kongamano la kila mwaka la chama cha wataalamu wa mambo ya biochemistry na bayolojia ya viumbe hai kutoka nchini Marekani (American society of biochemistry and molecular biology annual conference).

Kemikali hizi hatari ni uchafu (natural waste products) zinaotolewa na mwili wakati wa kusaga chakula (metabolism), na huweza kutolewa kwa wingi kwa mtu anayevuta sigara,mtu anapokumbana na mionzi (radiation) na hata wakati kukiwa na uchafuzi wa mazingira (pollution). Kemikali hizi uharibu mpangilio wa protini katika muundo wa vina saba (DNA structure).

Wanasayansi hao wakati wanafanya utafiti waliweza kuona ya kwamba mafuta ya parachichi yaliwezesha seli za yeast kuishi kwa muda mrefu kwenye madini chuma licha ya kuwekewa kiwango kikubwa cha madini hayo (exposed to high concentration of iron) ambayo ndio hutoa kemikali hizi hatari (free radicals) kwa wingi.

Mtafiti Christian Cortes-Rojo alisema “Tunahitaji kuthibitisha ya kwamba kile tulichoona katika seli za yeast kinaweza kutokea kwenye seli za binadamu”. Katika tafiti ambazo ziliwahi kufanyika huko nyuma nchini Mexico, nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa parachichi duniani, zilionyesha ya kwamba parachichi hupunguza kiwango cha lehemu (blood cholesterol) mwilini na pia hupunguza baadhi ya mafuta yanayohusishwa na ugonjwa wa kisukari.

Mafuta ya parachichi yana virutubisho sawa na mafuta ya olive oil yanayohusishwa kwa kusaidia kupunguza lehemu mwilini pamoja na kinga dhidhi ya magonjwa mengi sugu kama inavyoonekana kwa watu wanaoishi katika nchi za mediteranean ambao ni watumiaji wazuri wa mafuta haya ya olive oil.

Parachichi hupatikana kwa wingi nchini Tanzania katika mikoa ya Tanga (Lushoto), Mbeya hivyo ni muhimu kuboresha kilimo cha matunda haya ili kuweza kuboresha afya za wananchi. Kwa muda mrefu wanasayansi wamekuwa wakiita parachichi kama mfalme wa matunda kutokana na kuwa na virutubisho vingi kuliko tunda jingine lolote duniani.Hivyo, usisahau kula/kutumia parachichi mara kwa mara kwa afya njema.

Imesomwa mara 30223 Imehaririwa Ijumaa, 09 Juni 2017 16:31
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.