Image

Figo Kushindwa Kufanya Kazi (Renal/Kidney Failure)

Utangulizi

Figo ni miongoni mwa viungo muhimu sana katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu. Kwa kawaida, mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana kama yale ya maharage, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu za chini.

Kazi za figo

Kazi kuu za figo ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu kadhaa katika damu na hivyo kusaidia katika kuhifadhi na kuthibiti kiwango cha maji na madini (electrolytes) mwilini. Katika kutekeleza hayo, figo huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika.

Kazi nyingine za figo ni

  • Kurekebisha na kuthibiti kiasi cha vitu mbalimbali katika damu pamoja na kiasi cha maji katika mwili
  • Husaidia kutengeneza kiasili cha erythropoietin ambacho ni muhimu sana katika utengenezaji wa chembe nyekundu za damu.
  • Husaidia uzalishaji wa vitamini D
  • Husaidia pia katika kuthibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure)

Utengenezaji wa mkojo

Kwa kawaida damu inayozunguka mwilini hatimaye huingia kwenye figo kwa ajili ya kuchujwa, kutoa uchafu pamoja na sumu nyingine zisizohitajika mwilini. Kitendo hiki cha utengenezaji mkojo hufanyika katika hatua kuu zifuatazo;

  • Hatua ya kwanza ni uchujaji. Damu kutoka nje huingia ndani ya mafigo na kupita kwenye glomeruli, lenye umbo kama chekeche/chujio ambalo limeundwa na mishipa mingi midogo ya damu iliyojizungusha pamoja. Vitu mbali mbali, maji pamoja na sumu zilizo katika damu inayopita kwenye vimishipa hivi na kisha kuingia katika mirija mingine mikubwa kwa ajili ya uchujaji zaidi.
  • Mirija inayofuata huendelea kuchuja damu na kunyonya baadhi ya vitu vilivyo chujwa kimakosa kuvirudisha mwilini, mpaka kiasi sahihi cha uchafu kinachotakiwa kuchujwa kinapokuwa kimefikiwa.
  • Mara baada ya mkojo kutengenezwa na kutolewa kwenye figo, husafiri kuingia kwenye kibofu cha mkojo kwa kupita kwenye mirija ijulikanayo kama ureta. Kutoka kwenye kibofu, mkojo hutolewa nje ya mwili kupitia kwenye mrija wa urethra.

Figo kushindwa kufanya kazi (Renal Failure/ Kidney Failure)

Kushindwa kufanya kazi kwa figo hutokea iwapo sehemu ya figo au figo lote litapoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kutoka katika damu na kutengeneza mkojo. Kitendo hiki husababisha kusanyiko la uchafu pamoja na sumu kadhaa katika damu ambazo ni hatari kwa afya ya mhusika.

Aina za figo kushindwa kufanya kazi

Figo kushindwa kufanya kazi kumeganyika katika makundi yafuatayo

  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF) au Acute Kidney Failure (AKF).
  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa kiasi (Mild renal/kidney insufficiency)
  • Tatizo sugu la figo kushindwa kufanya kazi (Chronic renal failure)

Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF)

Hii ni hali inayotokea kwa ghafla, na kudumu kwa saa chache mpaka siku chini ya 14, na kusababisha ongezeko la kiwango cha creatinine na urea katika damu. Hali hii huwapata karibu asilimia 5% ya wagonjwa waliolazwa hospitali kwa sababu ya matatizo mbalimbali. Aidha hali hii hutokea zaidi kwa wagonjwa mahututi na wale wanaohitaji uangalizi wa kipekee, yaani waliolazwa ICU.

Katika makala hii tutatumia zaidi kifupisho cha ARF.

Visababishi na aina za ARF

Visababishi (au aina) vya ARF vinaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu:

  • Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal causes/failure)
  • Matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure)
  • Matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/failure)

Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal causes/failure)

Aina hii hutokea kwa takribani asilimia 60 mpaka 70 ya ARF zote. Katika kundi hili, figo hukosa damu ya kutosha kwa ajili ya kuchuja na hatimaye hushindwa kufanya kazi yake ipasavyo. Mambo yanayoweza kusababisha prerenal failure ni pamoja na:

  • Upungufu wa maji mwili unaosababishwa na kutapika kupita kiasi, kuharisha, au kupoteza damu kupita kiasi (kwa sababu ya ajali au kuumia)
  • Kuvurugika kwa mtiririko wa damu inayoingia kwenye figo kwa sababu ya:
    • Kushuka kwa ghafla kwa shinikizo la damu kwa sababu ya kupoteza damu nyingi wakati wa upasuaji mkubwa, kuumia au kuungua sehemu kubwa ya mwili, au maambukizi katika mfumo wa damu (sepsis) yanayoweza kufanya mishipa ya damu kutanuka na kushusha shinikizo la damu
    • Kuziba au kusinyaa kwa mishipa inayopeleka damu kwenye figo
    • Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) au shambulio la moyo (heart attack) linalosababisha kushuka kwa shinikizo la damu 
    • Ini kushindwa kufanya kazi (liver failure) kunakoweza kusababisha mabadiliko katika mfumo wa homoni zinazoathiri shinikizo la damu pamoja na mtiririko wa damu kwenda kwenye figo.

Mwanzoni kabisa mwa pre-renal failure huwa hakuna athari yoyote inayotokea kwenye figo, na mara nyingi, figo laweza kurudi katika hali yake ya kawaida iwapo chanzo cha tatizo kitagunduliwa na kushughulikiwa ipasavyo.

Matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure)

Mambo yanayosababisha madhara katika figo husababaisha karibu asilimia 25 mpaka 40 ya vyanzo vyote vya ARF. Visababishi vilivyo katika kundi hili hujumuisha vile vinavyoathiri uchujaji, mtiririko wa damu ndani ya figo na seli za figo zinazoshughulika na uchujaji na ufyonzaji wa chumvi na maji.

Visababishi hivyo ni pamoja na:

  • Magonjwa katika mishipa ya damu 
  • Kuwepo kwa damu iliyoganda ndani ya mishipa ya damu inayopita katika figo
  • Ajali/Kuharibika kwa tishu na seli za figo
  • Magonjwa ya mzio katika glomeruli na figo kwa ujumla (glomerulonephritis). Magonjwa yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na maambukizi (infection) ya bacteria jamii ya streptococci.
  • Magonjwa ya mzio katika nyama za figo (acute interstitial nepthritis). Mambo yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na matumizi ya baadhi ya madawa kama vile Aspirin, Ibuprofen (Brufen), baadhi ya antibiotics, na baadhi ya dawa za kutoa maji mwilini (antidiuretics); magonjwa kama vile saratani ya damu (leukemia), lupus na lymphoma. Magonjwa ya mzio katika nyama za figo husababisha madhara katika seli zinazohusika na uchujaji na ufynzaji wa chumvi na maji.
  • Magonjwa ya ukosefu wa damu katika mirija ya figo (acute tubular necrosis) ambayo hufanya seli na tishu za mirija hii kufa na hivyo mirija kushindwa kufyonza chumvi na maji kuyarudisha mwilini. Mambo yanayosababisha hali hii ni pamoja na shock (upungufu wa damu kuingia kwenye figo), matumizi ya madawa kama vile baadhi ya antibiotiki, sumu, dawa zinazotumika viwandani na kwenye x-rays na baadhi ya madawa yanayotumika kutibu saratani.

Matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/failure)

Mambo yanayosababisha hali hii huchangia kati ya silimia 5 mpaka 10 ya vyanzo vyote vya ARF. Postrenal failure wakati mwingine huitwa pia obstructive renal failure kwa sababu husababishwa na mambo yanayozuia utoaji wa mkojo nje ya figo.

Kuziba kwa ureta moja ama zote mbili kunaweza kusababishwa na:

  • Vijiwe figo (renal stones)
  • Saratani ya viungo vya njia ya mkojo au viungo vilivyo karibu na njia ya mkojo kiasi cha kuzuia mkojo kutoka nje ya figo
  • Matumizi ya baadhi ya madawa

Kuziba kwa njia ya mkojo katika eneo la kibofu cha mkojo kunaweza kutokana na:

Tafsiri nyingine ya ARF

Wagonjwa wa ARF wanaweza kupata mkojo kidogo sana au wasipate kabisa., au wanaweza kuwa na ongezeko la creatinine kwa kasi ya kutisha au kwa kasi ndogo sana. Hali hizi zinaweza pia kutumika kutoa tafsiri nyingine ya maana ya ARF. 

Mtu anayetoa kiasi cha mkojo chini ya 400mL kwa siku hujulikana kama ana oliguria, na huchukuliwa kuwa ana hali mbaya ya kutoweza kupona. 

Mtu anayetoa mkojo chini ya 100mLkwa siku husemwa ana Anuria, ambayo kama imetokea ghafla, huashiria kuwepo kwa tatizo la kuziba kwa mirija inayotoa mkojo kwenye figo zote mbili, na mara niyingi hali hii ni ya hatari zaidi. Tafsiri hii husaidia sana katika kuamua aina ya matibabu na muda wa kumpatia mgonjwa matibabu ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kumpata.

Dalili za ARF

Katika hatua za mwanzo mwanzo, baadhi ya waathirika wanaweza wasioneshe dalili zozote za tatizo hili. Dalili ni kama 

  • Kupungua kwa uzalishaji mkojo
  • Kuvimba mwili
  • Kupoteza umakini
  • kuchanganyikiwa
  • Uchovu
  • Kulegea mwili
  • Kichefuchefu na kutapika 
  • Kuharisha
  • Maumivu ya tumbo
  • Kuhisi ladha ya chuma na uchachu mdomoni
  • Na katika hatua za mwisho kabisa, mgonjwa anaweza kupata degedege na hatimaye kupoteza fahamu (coma).

Vipimo na uchunguzi

Kama ilivyoainishwa hapo juu kuwa baadhi ya wagonjwa wanaweza wasiwe na dalili zozote za tatizo hili. Hata wale wenye kuonesha dalili, zinaweza zisiwe mahsusi (non-specific). Uchunguzi wa mwili unaweza usioneshe tatizo lolote lile, au kukawa na dalili chache sana ambazo zinaweza zisimsaidie sana daktari kufikia uamuzi. 

Baadhi ya vipimo vinavyoweza kugundua uwepo wa ARF ni pamoja na

  • Kipimo cha utendaji kazi wa figo (Renal function tests) ambacho husaidia kuchunguza kiwango cha urea (blood urea nitrogen (BUN) katika damu. Aidha husaidia pia kuchunguza ongezeko la kiwango cha creatinine katika damu.
  • Uchunguzi wa kiwango cha madini mbalimbali katika damu (blood electrolytes) 
  • Uchunguzi wa damu (Full Blood Picture): Husaidia kuonesha uwepo wa maambukizi ya bacteria na/au upungufu wa damu mwilini (anaemia)
  • Kupima kiasi cha mkojo kinachotolewa na mgonjwa katika masaa 24
  • Uchunguzi wa mkojo (Urine analysis): Rangi ya mkojo, kiasi cha electrolytes, uwepo wa usaha au damu au casts.
  • Ultrasound ya figo na kibofu cha mkojo
  • Renal biopsy.

Matibabu ya ARF

Matibabu ya ARF hutegemea kwanza chanzo chake na pili ukubwa wa tatizo. Kujua chanzo cha tatizo husaidia kufahamu ni aina gani ya matibabu yanayohitajika wakati kufahamu ukubwa wa tatizo huathiri uchaguzi wa aina ya matibabu na hata hitaji la kufanya dialysis. Hata hivyo inashauriwa sana kumpeleka mgonjwa kwa daktari bingwa wa magonjwa ya figo (nephrologist) kwa matibabu zaidi.

Kulingana na chanzo cha ARF, baadhi ya matibabu yanayoweza kufanyika, hutolewa yakiwa na lengo la:

  • Kurekebisha kiasi cha upotevu wa maji mwilini ambapo mgonjwa hupewa i.v fluids pamoja kurekebisha kiasi cha madini (electrolytes) kilichopotea
  • Kupunguza au kuzuia ongezeko la maji kwa wagonjwa ambao figo zao zimeshindwa kabisa kutoa maji nje ya mwili
  • Kuongeza uwezo wa moyo kufanya kazi vizuri au kuongeza shinikizo la damu husaidia kuongeza mtiririko wa damu kwenda kwenye figo
  • Kurekebisha kiasi cha madini mwilini kitendo ambacho husaidia mwili kufanya kazi zake vema

Dialysis

Iwapo pamoja na matibabu hayo, figo za mgonjwa zinaendelea kudorora, mgonjwa hana budi kufanyiwa dialysis. Dialysis ni kitendo cha kutoa uchafu na maji yasiyohitajika katika damu. Kitendo hiki hufanywa kwa kupitia mishipa ya damu iliyo chini ya ngozi (hemodialysis) au kwa kupitia tumboni (peritoneal dialysis). Katika hemodialysis mirija hii huunganiswa kwenye mashine ambayo hufanya kazi kama figo. Damu kutoka kwa mgonjwa huingia katika mashine kisha huchujwa ili kuondoa sumu, uchafu pamoja na maji yasiyohitajika kabla ya kurejeshwa tena mwilini.

Kitendo hiki hufanyika angalau mara mbili mpaka tatu kwa wiki, na kwa kiasi fulani ni ghali na si watu wote wa kipato cha chini wanaoweza kumudu gharama zake.

Katika peritoneal dialysis, uchafu pamoja na maji kutoka katika mzunguko wa damu huingia katika nafasi inayotenganisha tumbo na utando wake (peritoneal space), huchujwa kwenye utando huo kisha hutolewa  kupitia sindano maalum (catheter ) iliyowekwa juu ya ngozi na kuingia ndani ya tumbo (peritoneal cavity).

Matarajio

Wagonjwa wengi wenye ARF hupona bila hata kuhitaji dialysis mara tu chanzo cha tatizo kinapogundulika na kushughuikiwa mapema. Hata hivyo wakati mwingine, pamoja na matibabu, baadhi ya figo hushindwa kurudia kufanya kazi kwa ufanisi wake wa awali. Watu kama hawa hawa wanahitaji kufuatiliwa kwa ukaribu na umakini mkubwa.

Kinga ya ARF

Inashauriwa

  1. kufanya uchunguzi wa figo walau mara moja kila mwaka. Hii husaidia kuchunguza utendaji wa figo na hivyo kuepuka madhara kabla hayajatokea.
  2. Kunywa maji kwa wingi ili kuyafanya mafigo yatende kazi zake kwa ufanisi.
  3. Kuepuka matumizi ya vitu ama madawa yanayoweza kuathiri nyama, seli au tishu za figo. Ni vema kutumia dawa pale tu unaposhauriwa na daktari.
  4. Watu wenye hatari ya kupata tatizo sugu la kushindwa kufanya kazi kwa figo (Chronic Renal Failure) wanashauriwa kufanya vipimo na cuhunguzi mara kwa mara
  5. Muone mtaalamu wa afya mara tu uonapo dalili za kuwepo kwa shida katika kukojoa au uonapo damu katika mkojo

 

Imesomwa mara 16355 Imehaririwa Jumanne, 05 Februari 2019 09:10
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana