Dalili na viashiria vya saratani ya shingo ya kizazi
Saratani ya shingo ya kizazi katika hatua za awali haina dalili au viashiria vyovyote.
- Kutokwa na damu katika tupu ya mwanamke (vagina) ambayo sio ya kawaida. Damu hii inaweza kuwa matone, au damu inayotoka katikati ya mzunguko wa hedhi (yaani baada ya hedhi kabla ya hedhi inayofuata) au damu itokayo kwa mwanamke ambae ameacha kupata hedhi.
- Kutokwa na damu baada ya kujamiana baada ya tendo la ndoa.
- Maumivu wakati wa kujamiana.
Dalili za saratani iliyosambaa ni kama zifuatavyo
- Kupungua kwa hamu ya kula
- Kupungua uzito
- Kuhisi uchovu
- Maumivu ya nyonga
- Maumivu kwenye mgongo
- Maumivu ya mguu
- Mguu mmoja kuvimba
- Kutokwa na damu nyingi kwenye tupu ya mwanamke
- Kuvunjika mifupa (bone fractures)
- Kutokwa na mkojo au kinyesi kwenye tupu ya mbele ya mwanamke.
Vipimo vya saratani ya shingo ya kizazi
Pap smear
Chembechembe au seli za shingo ya kizazi huchukuliwa na kuchunguzwa kutumia hadubini. Kipimo hiki pia hutumiwa katika uchunguzi wa wanawake ili kujua kama wamepata saratani ya shingo ya kizazi au la. Wanawake wenye zaidi ya miaka 18 au wale wenye upungufu wa kinga mwilini wanashauriwa kufanya kipimo hiki angalau mara moja kwa mwaka ili wajue afya yao.
Cervical Biopsy
Kipimo hiki huhusisha uchukuaji wa nyama kutoka kwenye uvimbe katika shingo ya kizazi na hupelekwa maabara kuchunguzwa kama kuna saratani au la. Kipimo hiki kinathibitisha uwepo wa saratani.
Colposcopy
Hii ni aina ya darubini inayotumiwa kuchunguza shingo ya kizazi ili kuangalia kama kuna tishu ambayo si ya kawaida. Kipimo hiki kinaweza kufanywa na daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama.
Cone Biopsy
Kipimo hiki hufanywa kwa kuchukua nyama kutoka katika shingo ya kizazi mfano wa koni kwa uchunguzi zaidi na hufanywa katika chumba cha upasuaji mgonjwa akiwa amepewa dawa ya nusu kaputi. Hiki kipimo kinaweza kutumiwa kama njia moja ya kutibu saratani ambayo haijaenea na ambayo ni ndogo sana kuondolewa kwa njia hii. Kuna aina mbili ya kufanya kipimo hiki
(a) Kukata nyama kutoka katika shingo ya kizazi kwa kutumia nyaya ya umeme inayojulikana kitaalamu kama loop electrosurgical excision procedure (LEEP) na
(b) Kukata nyama ya shingo ya kizazi kwa kutumia visu maalum vya upasuaji au laser
PET Scan
Kipimo hiki pia huweza kuthibitisha uwepo wa saratani na kuangalia maendeleo ya mgonjwa baada ya kupata tiba
Blood test
Vipimo vya damu, kuangalia wingi wa damu, kwa sababu wagonjwa wengi wanakuwa na upungufu wa damu kutokana na kuvuja damu mara kwa mara.
Picha ya kifua ya X-ray
Kuangalia kama saratani imesambaa kwenye mapafu au la.
CT Scan
Kuangalia kibofu cha mkojo kama kimeathirika au la, na pia kuangalia kama saratani imesambaa kwenye mifupa, ini, figo na sehemu nyingine za mwili.
Makundi ya saratani ya shingo ya kizazi
Saratani ya shingo ya kizazi imegawanywa katika makundi kulingana na TNM ama FGO (Classification) kama ifuatavyo;
Stage 0
Saratani iliyo kwenye chembechembe au seli za aina ya epithelium lakini haifiki kwenye nyama za ndani za shingo ya kizazi, Stage I – Saratani iliyopo kwenye shingo ya kizazi,
Stage II
Saratani iliyosambaa hadi kwenye tupu ya mwanamke sehemu ya juu kwa 2/3,
Stage III
Saratani iliyosambaa hadi kwenye ukuta wa nyonga na sehemu ya chini ya uke kwa 1/3, Hii inaleta madhara katika figo,
Stage IV
Saratani iliyosambaa hadi nje ya tupu ya mwanamke na pia husambaa hadi kwenye sehemu nyingine za mwili kama mapafu, figo, mifupa nk.
Tiba ya saratani ya shingo ya kizazi
Tiba ya saratani hii inategemea na kundi na aina ya saratani mgonjwa aliyonayo.
Tiba ni kama ifuatavyo:
Tiba ya kuchoma (cauterization)
Tiba hii hutolewa kwa wagonjwa wenye matatizo ya shingo ya kizazi kabla hayajakuwa saratani na hutumia joto kali , umeme, na kemikali kuchoma sehemu iliyoathirika.
Tiba ya dawa (Chemotherapy)
Tiba kwa kutumia dawa za saratani ambazo huuwa chembechembe au seli za saratani ya shingo ya kizazi. Dawa hizi hutolewa kwa mgonjwa ambae saratani imeshasambaa mwilini na inahusisha dawa moja pekee au mchanganyiko wa dawa zaidi ya moja ambazo mgonjwa hupewa kwa njia ya dripu au humeza kupitia mdomoni. Dawa hizi hutumiwa zaidi ya mzunguko mmoja na ni za gharama. Dawa hizi zinaweza kutumiwa ili;
- Kutibu saratani
- Kuzuia saratani isisambae sehemu nyingine mwilini
- Kupunguza kasi ya ukuaji wa saratani
- Kupunguza madhara ya saratani
Madhara ya dawa hizi yanatofautiana kulingana na aina ya dawa, muda wa utumiaji, na kiwango cha dawa yenyewe. Madhara yake ni kichefuchefu, uchovu, nywele kunyofyoka (hair loss) nk.
Tiba ya mionzi (radiation therapy)
Tiba ya mionzi kwa kutumia mionzi ya X-ray, gamma na neutrons ambayo huua seli za saratani hii. Mionzi hii haina maumivu na madhara yake ni uchovu, tupu kuwa nyembamba sana (narrowing of vagina) na mgonjwa kupungukiwa na damu.
Tiba ya upasuaji (surgical treatment)
Aina za upasuaji kwa mgonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ni kama zifuatazo:
- Cryosurgery: Mpira maalum (probe) huingiziwa kupitia kwenye tupu hadi kwenye shingo ya kizazi na majimaji ya nitrogen hupitishwa yaliyo na baridi ya -160 0 celsius yenye uwezo wa kugandisha na kuharibu seli za shingo ya kizazi hivyo kuzuia saratani.
- Laser surgery: Aina hii ya upasuaji inatumia mionzi ya laser ambayo huchoma seli za shingo ya kizazi ambazo haziko kwenye hali ya kawaida, mionzi hii haiharibu tishu za pembeni na hutumiwa kwa matatizo ya shingo ya kizazi kabla hayajakuwa saratani.
- Cone biopsy: Kama nilivyoeleza kwenye vipimo hapo juu.
- Simple hysterectomy: Hii inahusisha kuondoa mfuko wa kizazi (uterus) kupitia sehemu ya tumboni au kupitia kwenye tupu ya mwanamke kwa wagonjwa wa kundi I (Stage I). Madhara yake ni ugumba, kuvuja damu, kupata madhara sehemu ya haja ndogo au utumbo na maambukizi kwenye kidonda.
- Radical hysterectomy: Hii inahusiha kuondoa mfuko wa uzazi kupitia kwenye tumbo pamoja na tishu za mfuko wa uzazi, sehemu ya juu ya tupu ya mwanamke, na tezi za kwenye nyonga. Mayai (ovaries) na mirija ya uzazi yanabakizwa. Madhara yake ni kama ya hapo juu pamoja na kuleta karaha na maumivu wakati wa kujamiana.
- Pelvic exenteration: Huhusisha uondoaji wa kibofu cha mkojo, uke, puru (rectum) na sehemu ya utumbo mpana (colon). Upasuaji huu hutumiwa kwa wagonjwa wenye na saratani iliyojirudia.