Image

Je, kunyonyesha husaidia kupunguza maambukizi ya VVU?

Wakati watafiti duniani wakiendelea kutafuta dawa itakayoweza kutibu tatizo la UKIMWI linalosababishwa na VVU, hivi karibuni imebainika kwamba kuna uwezekano mkubwa wa maambukizi ya VVU kupungua kwa mtoto mchanga anayenyonyeshwa zaidi ya miezi 6 kutoka kwa mama mwenye VVU anayetumia dawa. Hii ni kutokana na matokeo ya utafiti iliyofanywa na BAN (Breastfeeding, Antiretroviral and Nutrition) trial na kuchapwa katika mojawapo ya jarida kubwa la afya duniani la Lancet la mwezi Mei mwaka huu.

Hapo awali Shirika la Afya Duniani (WHO) na mashirika mengine ya afya yalipendekeza mama mwenye maambukizi ya VVU kunyonyesha mpaka mtoto atakapofika miezi 6 au chini ya hapo katika nchi maskini na familia zisizokuwa na kipato kikubwa ili kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwenye maziwa ya mama lakini vilevile kuepuka maambukizi ya magonjwa mengine ambayo yanaweza kumpata mtoto.

Faida mojawapo kubwa ya kunyonyesha mtoto ni kumpatia kinga imara kupitia katika maziwa ya mama ili kupambana na vimelea mbalimbali vya magonjwa. Ikumbukwe kwamba kinga ya mtoto mchanga dhidi ya vimelea vya magonjwa mbalimbali ni hafifu, na hii ndio inayosababisha kukawepo aina mbalimbali za chanjo kwa ajili ya watoto.

Hata hivyo, katika hii taarifa mpya ya BAN matokeo yanaonesha kwamba hatari ya maambukizi ya VVU huongezeka mara mtoto anapoacha kunyonya akiwa na miezi 6. Katika kukabiliana na hili, Shirika la Afya Duniani linapendekeza kwa mama mwenye maambukizi ya VVU kuendelea kumnyonyesha mtoto wake mpaka atakapofikisha mwaka 1.

Katika tafiti hii ambayo ilifanyika nchini Malawi katika kipindi cha miaka 7 toka mwaka 2004-2010, Dr. Denise J. Jamieson, kutoka kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa, (CDC) cha huko Atlanta, nchini Marekani na timu ya utafiti ya BAN walikuwa na makundi 3 ya akina mama pamoja na watoto wao wachanga [wajawazito ambao walikuwa kwenye dawa aina 3 za ARV, watoto wachanga waliokuwa kwenye dawa aina ya nevirapine na watoto wachanga ambao hawakuwa kwenye dawa ambao hawa waliitwa kundi thibiti au kwa lugha ya kitafiti control group].

Watoto wachanga walipimwa VVU wakati wa kuzaliwa, wakiwa na wiki 2, 12, 28, na wiki 48. Wale waliobainika kuwa na VVU katika wiki ya 2 walitibiwa na kuondolewa kwenye utafiti kwa vile hawa walishaonekana kuwa wameshapata maambukizi ya VVU kabla ya kuzaliwa na kunyonyeshwa. Akina mama waliambiwa kuanza kuwapatia watoto wao vyakula vya ziada kati ya wiki 24 na 28.

Katika wiki ya 32, wengi wa wanawake, karibu asilimia 96 kutoka katika kundi tafiti au kwa lugha ya kitafiti treatment group na karibu asilimia 88 ya kina mama kutoka kundi thibitiwa yaani control group waliripoti kuacha kunyonyesha.

Hatari ya kuongezeka kwa maambukizi ya VVU katika wiki ya 48 ilikuwa kubwa zaidi katika kundi thibitiwa [control group] kwa silimia 7 ukilinganisha na asilimia 4 katika kundi tafiti [treatment group]. Katika tathmini ya maambukizi ya VVU, asilimia 30 (%) ya maambukizi yalitokea baada ya wiki 28 mtoto alipoachishwa kunyonya maziwa ya mama, wakati asilimia tisa ya maambukizi ilitokea katika kundi la wakina mama wanaotumia ARV, asilimia 13 katika kundi la watoto wachanga wanatumia nevirapine, na asilimia 6 katika kundi thibitiwa [control group]. Aidha, matatizo mengine kama ya kuharisha, malaria, kifua kikuu, ukuaji mbaya na vifo yalijitokeza katika kipindi hiki.

Hitimisho katika tafiti hiyo ilikuwa kwamba kumuachisha mtoto kunyonya maziwa ya mama mapema siyo njia salama na sahihi katika mikakati ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa watoto wadogo.

Imesomwa mara 5273 Imehaririwa Jumamosi, 28 Julai 2018 13:40
Dr. Paul J. Mwanyika

Dr. Paul J. Mwanyika ni Daktari  Bingwa waTiba na Uchunguzi wa Magonjwa ya Watoto (Pediatrics).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana