Image

ARV , makundi yake na jinsi inavyofanya kazi

Tangu kuingia kwa dawa za kuvubaza VVU (ARVs) kumeripotiwa kuwepo kwa mafanikio makubwa katika kuboresha afya za watu wanaoishi na VVU kwa kusaidia kupunguza idadi ya VVU na kuongeza idadi ya chembe nyeupe za CD4 zinazosaidia mwili kujilinda na maradhi. Lakini ARVs ni nini? Kuna makundi mangapi ya dawa hizi, zinafanyaje kazi, je zina madhara (side effects) yeyote katika mwili wa binadamu? Katika kujibu maswali haya, mwandishi wako Dk. Fabian P. Mghanga anatuletea makala ifuatayo.

Dk. Robert Kisanga aliegesha gari yake katika eneo la kuegesha magari la kituo kinachojishughulisha na huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI kilichopo wilaya moja ya jiji la Dar es Salaam. Kama ilivyo kawaida ya kazi zake za kila siku, ratiba ya shughuli zake za leo inaonesha ana jukumu la kutoa mada kwa baadhi ya wateja wapya walioandikishwa kwa ajili ya kuanza matibabu ya dawa za kurefusha maisha kwa waathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi maarufu kama ARVs.

Katika umri wake wa miaka ya mwanzo ya thelathini, Dk. Kisanga amejipatia umaarufu sana miongoni mwa wateja wake kwa sababu ya upole, ucheshi, utu na uchapakazi wake. Ni aghalabu kumkuta akiwa amekunja uso au kutoa maneno yasiyofaa na yenye maudhi kwa wale wanaomzunguka. Sifa na tabia hizi zimemfanya awe kipenzi hata kwa wafanyakazi wenzake.

Baada ya kumaliza taratibu nyingine za kikazi asubuhi ile, alielekea chumba cha mkutano, eneo ambalo lilikuwa na wateja wapya takribani thelathini wakimsubiri kwa hamu. Somo la leo lilihusu dawa za ARVs, aina, namna zinavyofanya kazi, faida na athari zake.

Kwa kuanza somo, Dk. Kisanga alitoa ufafanuzi wa nini maana ya ARVs au kama zinavyojulikana kwa jina jingine la HAART.

Alisema, “ARVs au Antiretroviral drugs ni kundi la dawa zinazotumika kwa ajili ya kutibu maambukizi yanayosababishwa na virus wa jamii ya retroviruses, hususani HIV.’

Na ikiwa dawa kadhaa kati ya hizo, tuchukulie dawa tatu au nne, zitatumika kwa pamoja kwa ajili ya lengo hilo basi mkusanyiko huo huitwa Highly Active Antiretroviral Therapy au kwa kifupi HAART.

ARVs zimegawanyika katika makundi kadhaa kutokana na jinsi zinavyofanya kazi na hii ni kulingana na hatua mbalimbali katika mzunguko wa maisha wa kirusi cha Ukimwi (HIV life-cycle). Ndiyo kusema kuwa, dawa hizi zimetengenezwa kwa kuzingatia uwezo wake katika kushambulia hatua mbalimbali za maisha ya VVU tangu vinapoingia katika mzunguko wa damu wa muathirika.

Muundo na umbo la HIV

virus

 

Dk. Kisanga anasema ili tuweze kujibu swali kuhusu mzunguko wa maisha ya HIV katika mwili wa binadamu ni vema kwanza tuangalie umbo la kirusi cha HIV na pia aina ya chembe nyeupe za damu au CD4 ambazo HIV huzitumia kwa ajili ya kuzaliana.

Anasema, ‘HIV kikiwa nje ya seli ya binadamu kina umbo duara linalofanana kiasi na kitufe kidogo ambacho kitaalamu huitwa virion (wingi ni virions). Sura ya virion imezungukwa na ncha zinazofanana na miba midogo midogo au spikes.

Kitufe cha HIV kina kipenyo chenye ukubwa wa takribani 0.1 microns ambayo ni sawa na sehemu bilioni 100 mpaka 150 za mita moja (yaani igawe mita moja katika sehemu ndogo ndogo bilioni 100 au 150), au sawa na moja ya saba ya ukubwa wa seli ya CD4 ya binadamu. Kwa sababu ya udogo huu, si rahisi kuweza kuona HIV kwa kutumia darubini ya kawaida isipokuwa kwa kutumia darubini iitwayo electron microscope.

HIV imezungukwa kwa nje na utando wa mafuta unaojulikana kama envelope (au membrane). Ncha ndogo takribani 72 zijulikanazo kama spikes zinaonekana kuchomoza juu ya utando huu. Ncha hizi zimeundwa kwa kutumia aina mbili maalum ya proteini zinazoitwa gp120 na gp41. Aina hizi za proteini ni muhimu mno katika mzunguko wa maisha ya HIV kama tutakavyoona hapo baadaye. Chini kidogo ya utando huu (envelope) kuna utando mwingine uitwao matrix ambao unaundwa na aina nyingine ya protein ijulikanayo kama p17.

Ndani ya utando wa matrix kuna kiini cha HIV kujulikanacho kama capsid ambacho kina umbo kama la risasi na kimeundwa na aina ya proteini ijulikanayo kama p24. Ndani kabisa ya kiini au capsid kuna aina tatu tofauti za vimeng’enyo au enzymes ambavyo ni muhimu mno kwa ajili ya uzalianaji wa HIV. Vimeng’enyo hivyo hujulikana kama reverse transcriptase, integrase na protease. Pamoja na vimeng’enyo hivyo, capsid pia ina nyuzi mbili za vinasaba vya RNA ambavyo husaidia kurithisha tabia za kinasaba za HIV kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

Ikilinganishwa na makundi mengine ya viumbe hai yenye vinasaba vingi, HIV ina vinasaba vya aina tisa tu. Vinasaba vitatu viitwavyo gag, pol na env hufanya kazi ya kubeba taarifa inayohitajika kuunda protein muhimu kwa ajili ya virusi wapya watakaozaliwa. Vinasaba sita vilivyobaki vinavyojulikana kama tat, rev, nef, vif, vpr na vpu hufanya kazi ya kubeba taarifa ya kuthibiti uzalishaji wa protein inayohusika na kuthibiti uwezo wa HIV kushambulia seli mpya za binadamu, kuzaa virusi wapya au kusababisha ugonjwa kwa binadamu.”

Dk. Kisanga pia aliendelea kuichambua CD4 akisema,” CD ni kifupi cha maneno ya kingereza ya cluster of differentiation. Hii ni aina mojawapo ya kiasili kilichoundwa kwa proteini na mafuta (yaani glycoprotein) ambacho kinapatikana juu ya uso wa seli nyeupe za damu zijulikanazo kama T helper cells, regulatory T cells, monocytes, macrophages, na dendritic cells ambazo kazi yake kubwa ni kupambana na maradhi mbalimbali. Zimepewa jina la CD4 kuonesha kuwa ni aina ya nne katika kundi la viasili vya CD. Vilipewa jina hilo kwenye mwaka 1984 ingawa hasa hasa viligunduliwa mwishoni mwa miaka ya sabini.

Kazi kubwa za CD4 ni kusaidia baadhi ya chembe nyeupe za damu kupambana na wadudu waenezao maradhi mbambali katika mwili wa binadamu.

Kwa kutumia kajisehemu chake ambacho kipo ndani ya seli za T cell, CD4 husaidia kukuza na kupitisha taarifa kutoka kenye vipokeo vilivyopo kwenye T Cell. Taarifa hii huzitaadharisha chembe nyeupe za damu kujiandaa kupambana na vidudu vilivyo vamia mwili kwa kutumia njia mbalimbali. Aina hii chembe nyeupe za damu inayopambana na uvamizi wa mwili huitwa T-lymphocytes.

Wakati akiendelea na mada yake, mteja mmoja alimuuliza swali, “Je HIV huingiaje katika seli za mwili wa binadamu?”

Dk. Kisanga alijibu, “ili tuweze kujibu swali lako hilo, ni vema basi tuangalie kwanza mzunguko wa maisha wa HIV.”

Mzunguko wa maisha wa HIV (HIV-lfe cycle)

mzungungo-wa-hiv

 

Ili kuweza kuingia ndani ya seli za binadamu na kuzaliana, HIV hutumia kiasili cha CD4 kama njia ya kupita. Katika kufanikisha hilo, kuna hatua kuu sita katika mzunguko wake wa maisha. Baada ya mtu kupata maambukizi ya VVU kwa njia yeyote ile na VVU kuingia ndani ya mzunguko wa damu wa mwanadamu, hatua ya kwanza katika mzunguko wa maisha wa HIV ni kunata na kujiunganisha na CD4 au Binding na Fusion.

HIV huanza maisha yake kwa kuunganisha ncha za proteini zilizojitokeza kwenye utando wake zijulikanazo kama gp120 kwenye vipokeo (receptors) vya CD4. Muunganiko huu wa CD4 na gp 120 hubadilisha kabisa umbo la gp120 hali ambayo huruhusu HIV kujipachika katika vipokeo visaidizi (co-receptors) vilivyoko kwenye utando wa juu wa seli ya binadamu.

Vipokeo hivi visaidizi hujulikana kama chemokine receptors CCR5 au CXCR. Kuhusu ni aina gani kati ya vipokeo hivi visaidizi hutumika wakati wa uambukizi wa HIV, inategemea ni aina gani ya seli nyeupe kati ya macrophage au T-helper cell inayoshambuliwa wakati huo.

Baada ya hapo, aina nyingine ya ncha za proteini zilizo kwenye utando wa nje wa HIV ziitwazo gp41 nazo hubadilika umbo lake, na hivyo kuwezesha HIV kuachia aina nyingine ya proteini inayoitwa fusion peptide kwenye seli nyeupe ya damu. Protein hii huwezesha utando wa juu wa HIV kuungana na utando (cell membrane) wa seli nyeupe inayoshambuliwa.

Hatua ya pili ni HIV kupenya na kuingia ndani ya seli nyeupe ya binadamu kitendo kinachojulikana kama Viral Penetration/Fusion. Kitendo cha kuungana kwa utando wa juu wa HIV na ule wa seli nyeupe husababisha kutokea kwa tundu katika utando wa seli nyeupe. Kitendo hiki huwezesha kibeba vinasaba cha HIV au capsid kusukumwa moja kwa moja mpaka ndani ya seli nyeupe ya binadamu kupitia kwenye tundu hilo.

Hatua ya tatu ni kujivua gamba kwa HIV. Hatua hii kwa jina lingine hujulikana kama uncoating. Kujivua gamba huku husaidia kuruhusu vinasaba vya HIV pamoja na vimeng’enyo muhimu kwa ajili ya kubadilisha vinasaba vya RNA kwenda DNA, hatua ambayo ni muhimu sana kwa uzalianaji wa virusi wapya.

Hatua ya nne ni ubadilishaji wa RNA ya virusi kuwa DNA ya virusi kwa kutumia kimeng’enyo cha reverse transcriptase. Kitendo hiki hujulikana kitaalamu kama reverse transcription kwa sababu hutokea kinyume na vile kinavyotakiwa kutokea kwa viumbe hai wengine. Kwa kawaida, kitendo cha transcription hufanyika kwa kubadilisha DNA kuwa RNA na si kinyume kama chake.

Baada ya DNA hii ya virusi kutengenezwa ndani ya ute wa seli ya binadamu, hubadilishwa kuwa aina fulani ya RNA iitwayo messenger RNA, yenye uwezo ya kuamrisha seli kufanya kazi mbalimbali kulingana na mahitaji ya mwili. Kisha aina hii ya RNA yenye uzi mmoja hubadilishwa tena kuwa DNA ya virusi yenye nyuzi mbili. Matukio haya yote hufanyika ndani ya ute (cell cytoplasm) wa seli nyeupe ya damu.

Hatua ya tano huitwa integration. Baada ya HIV kufanikiwa kubadilisha RNA yake kuwa DNA, ni lazima sasa HIV aingize DNA yake hii mpya kuingia kwenye DNA ya seli ya binadamu ili aweze kuthibiti kikamilifu na kuamrisha matendo na kazi zote za seli nyeupe ya binadamu ili seli hiyo iweze kufanya inavyotaka HIV.

Kitendo hiki huitwa integration na hufanyika ndani ya kiinitete (nucleus) cha seli ya binadamu kwa kutumia kimeng’enyo cha HIV kiitwacho integrase.”
Baada ya kusema hayo, miguno na vicheko vilisikika ukumbini, huku baadhi ya washiriki wakistaajabia uwezo huu wa VVU katika kuvamia na kuthibiti seli za binadamu.

Baada ya sekunde kadhaa Dk. Kisanga akaendelea kusema, “Hatua ya sita inahusika na uzalishaji wa protini na virusi wengine wapya au kitaalamu tunaita protein synthesis na viral latency. Katika hatua hii, seli ya binadamu kwa sasa tunaweza sema imeshaambukizwa VVU. Aina hii ya seli ya binadamu yenye DNA wa HIV ndani yake huitwa pia pro-virus yaani Virusi wa awali ambaye anasubiri kuchagizwa tu kidogo na mfumo wa kinga ya mwili.

Baada ya seli hiyo kuchagizwa na mfumo wa kinga ya mwili, viruis huyu wa awali huamka na kuanza kutoa maelekezo katika seli ya binadamu ya kuzalisha viungo vingine kadhaa vya HIV ambavyo vitakuja kutumika kwa ajili ya virui wapya watakaozaliwa. Kutoka katika DNA hii, nyuzi mbili za RNA hutengenezwa na kusafirishwa kuingia kwenye ute wa seli.

Uzi mmoja hubadilishwa kuwa vipande vidogo vidogo vya vimeng’enyo vya protease, reverse transcriptase, na integrase, na pia protini zitakazohusika kuunda umbo la virusi wapya, wakati uzi mwingine hutengeneza vinasaba kwa ajili ya virusi wapya. 

Imesomwa mara 9001 Imehaririwa Jumatatu, 21 Januari 2019 14:41
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana