Image

Tatizo la Kutokwa na usaha Wakati wa Kukojoa

Ushawishi wa kuandika makala hii ya tatizo la kutokwa usaha wakati wa kukojoa umetokana na swali la msomaji wetu ambaye aliuliza hivi kwenye tovuti hii na hapa na mnukuu,

 " Dr khamisi samahani sana mi nasumbuliwa nikikojoa mwisho wa mkojo unatoka kama usaha na sina dalili ya kaswende ambazo umezizungumzia nakuomba unisaidie’’.

Bila shaka wapo wengi ambao wana tatizo kama hili na ambao wamewakilishwa kupitia swali hili lililoulizwa na msomaji wetu huyu. Naomba tuwe pamoja kwenye makala hii ili ujifunze kuhusu tatizo la mtu kutokwa usaha wakati wa kukojoa.

Tatizo la Kuwepo kwa chembechembe za usaha au usaha kwenye mkojo hujulikana kama pyuria ambapo linaweza kuonekana kwa kutumia hadubini (microscope) au kama tatizo ni kubwa linaweza kuonekana kwa macho.

Visababishi vya tatizo la Kutokwa Usaha Wakati wa Kukojoa ni nini?

Visababishi vya tatizo hili ni kama vifuatavyo;

  • Ugonjwa wa mfumo wa mkojo (UTI)-Maambukizi kwenye figo, kwenye mrija wa mkojo na kwenye kibofu cha mkojo (cystitis- amabayo huonekana sana)
  • Magonjwa ya Zinaa-Kama ugonjwa wa kisonono au ‘’gono’’ kama wengi wanavyoita, ugonjwa wa Chlamydia na Trichomoniasis
  • Sumu inayotokana na kemikali (Chemical poisoning) kama 4-Aminodiphenyl inayotumika kwenye maabara na kwa ajili ya tafiti
  • Tatizo linajulikana kama Reiter’s syndrome
  • Pyelonephritis-Maambukizi ya bakteria kwenye sehemu za figo zinazojulikana kama calyces, renal pelvis na tishu za figo
  • Madhara ya pyelonephritis ambayo husabababisha ugonjwa unaojulikana kama renal abscess
  • Maambukizi kwenye tezi dume-Prostatitis (Kwa wanaume)
  • Upungufu wa kinga mwilini
  • Mcharuko (Inflammation) kutokana kuwa na mawe kwenye kibofu cha mkojo au kwenye figo
  • Mzio (Allergy) au kuota uvimbe sehemu yoyote ya mfumo wa mkojo

Viashiria vya tatizo hili ni;

  • Maumivu makali ya kuchoma (Painful burning sensation) wakati wa kukojoa
  • Maumivu chini ya kitovu
  • Homa
  • Kutapika

Tatizo hii likidumu kwa muda mrefu husababisha kupungua uzito kwa mgonjwa

Vipimo vya uchunguzi

  • Urinalysis – Kipimo cha mkojo
  • Urine for culture and sensitivity - Kipimo cha kuangalia bakteria kwenye mkojo
  • Complete blood count – Kipimo cha kuangalia wingi wa damu na chembechembe za damu (husaidia  kuonyesha kama kuna maambukizi kwenye mwili)
  • Blood culture - Kuangalia kama kuna maambukizi kwenye damu
  • Prostate –Specific Antigen (PSA) Test-Kipimo cha tezi dume
  • Kipimo cha mionzi ya X-ray - Huonyesha kama tatizo ni kubwa sana
  • Kipimo cha ultrasound
  • Kipimo cha CT scan au MRI - Husaidia kuonyesha kama tatizo hili lipo ndani ya tishu za figo  (Intra-renal abscess) au nje ya tishu za figo (Extra-renal abscess)

Vichagizi vya Tatizo la Kutokwa Usaha Wakati wa  Kukojoa (Predisposing Factors)

Vichagizi vya tatizo hili ni;

  • Kutosafisha vizuri sehemu za siri baada ya kujisaidia haja ndogo
  • Kujamiana na mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa wowote wa zinaa
  • Ugonjwa wa kisukari
  • Madhara yanayotokana na kutumia mpira wa mkojo - Kwa wale wote waliowekewa mpira huu wa mkojo (catheter)
  • Saratani ya kwenye mfumo wa mkojo au sehemu za siri
  • Matumizi ya dawa za jamii aina ya Non-steoridal anti-inflammatory drugs (NSAIDS) au madawa yanayopunguza kinga mwilini (Immuno-suppressant medications) kwa muda mrefu
  • Kuvimba kwa tezi dume

Matibabu

  • Tiba hutegemea na chanzo cha tatizo hili
  • Dawa za kutibu vimelea (antibiotics)
  • Matibabu ya mawe kwenye kibofu cha mkojo au kwenye figo
  • Kunywa maji kwa wingi mara kwa mara ili kusaidia kutoa chembechembe za usaha kupitia njia ya haja ndogo-Ikumbukwe ya kwamba maji sio tiba

DOKEZO-MGONJWA ATAHITAJI KUMUONA DAKTARI ILI APATE TIBA STAHIKI  KULINGANA NA CHANZO CHA TATIZO LA KUTOKA  USAHA  WAKATI WA KUKOJOA

Imesomwa mara 17811 Imehaririwa Jumatatu, 18 Januari 2021 15:20
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana