Image

Dawa za Kuongeza Makalio: Urembo wenye Ukakasi

Dawa za kuongeza makalio ni kitu kilichopata umaarufu wa ghafla miongoni mwa kina dada wengi duniani na hata katika jamii yetu. Siku hizi haishangazi kusikia dada mwenye makalio makubwa au yenye umbo duara akiambiwa kuwa anatumia dawa za kunenepesha makalio au ‘wowowo’ au 'zigo' kama wanavyopenda kuita vijana kwa kiswahili cha mtaani. Aidha matangazo juu ya dawa hizi nayo yamekuwa yakiongezeka kila kukicha. Leo hii ukienda kwenye mitandao ya kijamii kuna matangazo mengi sana ya dawa zenye kuongeza makalio na matiti. Pamoja na kwamba kuna simulizi tofauti juu ya faida na madhara ya matumizi yake, idadi ya watumiaji inazidi kuongezeka siku hadi siku.

Lakini dawa za kuongeza makalio ni nini hasa? Kwa ujumla hizi ni dawa zitumiwazo na akina dada na mama kwa ajili ya kunenepesha na kuongeza ukubwa wa makalio yao na kuyafanya yawe na umbo wanalodhani linawavutia wao au/na wapenzi wao. Ukisoma maelezo ya dawa hizi, nyingi hudai kuwa na uwezo wa kuboresha umbo la makalio kwa kuyafanya yawe na muonekano wa ujana zaidi, duara, laini na yenye mvuto.

Wanawake karibu dunia nzima huamini maelezo kuwa dawa hizi zina uwezo wa kuwajengea maumbo wanayoyatamani. Wengi, kuanzia watu mashuhuri (celebrities) mpaka watu wa kawaida, wanataka makalio makubwa; yale maumbo madogo na makalio ‘yasiyojazia’ hayana nafasi tena. Wanaamini kuwa makalio ‘yaliyojazia’ yanafanya hata nguo kukaa vema mwilini, huwafanya wanaume kugeuza shingo kuwashangaa (labda kuwatamani pia) na wengine hudai yanasaidia kuongeza mvuto wa ngono kwa wapenzi wao.

 wowo-kubwa

Pamoja na kuwepo njia nyingine za kuongeza makalio, ikiwemo upasuaji, njia hii ya kutumia dawa inaonekana kupendwa zaidi kwa vile haina gharama sana ukilinganisha na ile ya upasuaji. Hata hivyo tofauti na upasuaji, matumizi ya dawa yanahitaji uvumilivu kwani huchukua muda kwa matokeo kuonekana. Kwa mfano zipo baadhi ya dawa zinazodaiwa kuonesha mafanikio ndani ya muda wa wiki mbili mpaka miezi mitatu wakati nyingine huchukua mpaka miezi 11.

Lakini cha kushangaza ni kuwa, nyingi ya dawa hizi hazijathibitishwa na mamlaka za chakula na madawa (FDA) za nchi zinaposemekana kutengenezwa kutokana na ama kutengenezwa kwa kificho (black market) au kutokidhi masharti yanayotakiwa katika utengenezaji wake.

Lakini dawa hizi zinafanyaje kazi?

Pamoja na kwamba dawa hizi ni maarufu karibu dunia nzima, ni dawa chache sana kati ya hizi ambazo zina maelezo ya waziwazi ya namna zinavyofanya kazi. Hali hii inatia shaka sana kuhusu ukweli wa uwezo wake katika kuongeza ukubwa wa makalio au hata madhara ambayo mtumiaji anaweza kuyapata kutokana na matumizi yake.

Zipo baadhi ya dawa ambazo hudaiwa kuwa na uwezo wa kunenepesha makalio kwa kuongeza zaidi utando (layer) wa mafuta katika maeneo hayo bila kuongeza mafuta sehemu nyingine ya mwili. Zaidi, ufanyaji kazi hutofautiana pia kutokana na mfumo (formulation) ya dawa husika ilivyo. Kuna aina nyingi ya dawa hizi, kuanzia za kupaka (creams), vidonge (pills) mpaka za sindano (injections).

Misuli na nyama za makalio zinapopoteza collagen na elastin (aina fulani ya mishipa ambayo husaidia kushikilia nyama na misuli katika ngozi), husababisha makalio kupoteza umbo lake, kuwa na mikunjo na pengine ‘kuanguka’. Baadhi ya dawa hizi zinadaiwa kuwa na uwezo wa kupenya utando wa juu wa ngozi (epidermis) mpaka kwenye utando wa pili (dermis) ambapo 

hufanya kazi ya kukarabati collagen na elastin zilizoharibika/kupotea. Aidha dawa za namna hii huaminika kuwa na uwezo wa kupenya hata kufikia utando wa chini kabisa wa ngozi. Dawa zinazofanya kazi kwa njia hii hufanya kazi sehemu ile tu ilipopakwa iwe kwenye makalio au mapaja (hips) na hudaiwa kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa kasi zaidi kuliko zile za vidonge au za sindano.

Njia nyingine ambayo inasemekana dawa hizi hufanya kazi ni kwa kupitia hormones. Hormones ni aina ya vichocheo fulani katika mwili ambavyo huufanya mwili kutekeleza kazi mbalimbali. Mojawapo ya hormones zinazosemekana kutumiwa katika mengi ya madawa haya ni ile iitwayo Phytoestrogen. Kuna njia mbalimbali ambazo phytoestrogen hufanya kazi katika mwili wa binadamu.

Kwa vile hormones hizi zinafanana sana kiumbo na homoni za kike za estrogen, phytoestrogen hufanya kazi kama estrogen (iwapo zikitumika katika kiwango kidogo) na huzuia kazi ya estrogen (kama zikitumika katika kiwango kikubwa).

Estrogen hufanya kazi ya kuupa mwili wa mwanamke mabadiliko na tabia za kike kama vile kuongezeka kwa ukubwa wa matiti, kukua kwa makalio, kuwa na ngozi nyororo na ya kuvutia, kuwa na sauti nyembamba n.k. Hivyo basi phytoestrogen hufanya kazi kama zile zinazofanywa na estrogen ikiwemo ya kuongeza ukubwa wa makalio na kuyafanya yawe na umbo la kuvutia.

bigbooty1

Njia nyingine ya ufanyaji kazi wa dawa hizi ni kuongeza hamu ya kula kwa mtumiaji. Matumizi ya vidonge vijulikanavyo kama chicken pills na vile vya vitamini vya Ectoplan husababisha mtumiaji kupata hamu ya kula na hivyo kula kupita kiasi hali inayomfanya kunenepa siyo tu makalio bali sehemu mbali mbali za mwili.

Dawa nyingine hudaiwa kuwa na vitu vyenye uwezo wa kulainisha ngozi na seli za misuli na hivyo kutanua mishipa ya damu hali inayosaidia kuongeza mtiririko wa damu kwenda kwenye maeneo ya makalio na hivyo kusaidia ukuaji wa seli za maeneo hayo.

Baadhi ya dawa hizi hudaiwa kufanya kazi kwa kutawanya misuli na tishu za mafuta katika maeneo ya kuzunguka mapaja, hips pamoja na misuli ya makalio yaani gluteus muscles. Pia baadhi ya dawa zenye vitamini E, kwa mfano, hudaiwa kufanya kazi kwa kuimarisha seli za makalio na kufanya ngozi ya maeneo hayo kuwa imara, laini na yenye kushika zaidi collagen (firm) na hivyo kuyapa makalio umbo la duara.

Sindano za silicone oil hufanya kazi kwa kusisimua seli za mwili zipambanazo na vijidudu kufanya mcharuko mwili (inflammation). Kinachotokea ni kuwa, mara baada ya mtu kuchoma sindano ya silicone oil, seli za mwili hujikusanya kwa lengo la kushambulia silicone zilizoingia mwilini.

Seli hizi hujaribu kuvunja vunja chembe chembe za silicone kwa kuzimeza na kuzisafirisha kutoka seli moja kwenda nyingine kwa lengo la kuzitoa nje ya mwili. Kwa vile silicone haziwezi kuvunjwa na seli hizi, hubaki zikizungukwa na seli zaidi na zaidi za mwili pamoja na collagen na hatimaye sehemu iliyochomwa sindano huongezeka ukubwa kwa vile collagen zaidi na zaidi kulundikana kuzunguka silicone hizi.  Kwa hiyo kumbuka kuwa, kuongezeka kwa makalio hakutokani na wingi wa silicone iliyochomwa bali tabia ya mwili wa mtumiaji kulundika collagen kuzunguka silicone hizo.

Nini madhara ya dawa hizi?

Ili kuweza kufahamu madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kuongeza makalio, ni vema pia tuangalie ni aina gani ya vitu vilivyomo kwenye dawa hizi.

Kama tulivyoona hapo awali kuwa aina nyingi ya dawa hizi zina hormones za phytoestrogen. Phytoestrogen hupatikana katika mimea ya aina nyingi sana (takribani 300 hivi) kama vile soya, maharage, zikiwa katika mfumo wa kemikali za aina tatu za isoflavonoid, lignans au coumestans.  Pamoja na faida nyingi za phytoestrogen, hormone hii ina tabia ya kushindana na hormone ya estrogen katika vipokeo (receptors) vyake. Kwa maana nyingine ni kuwa phytoestrogen huingilia utendaji kazi wa estrogen ambayo inahusika na uzazi na afya ya moyo na mifupa ya mwanamke.

Aidha kuna matokeo yanayokinzana ya tafiti mbalimbali kuhusu uwezekano wa phytoestrogen kusababisha saratani ya matiti wakati nyingine zikionesha uwezo wake katika kumlinda mtumiaji dhidi ya uwezekano wa kupata saratani hiyo iwapo zitatumika kwa usahihi (kwa kiwango kidogo).

Iwapo phytoestrogen inasababisha saratani ya ukuta wa kizazi (endometrial carcinoma) au la bado haijathibitishwa. Matumizi yasiyofuata maelekezo yanaweza kusababisha uwiano usio sawa wa hormone (hormonal imbalance) hali ambayo inaweza kumsababishia madhara mtumiaji.

Madhara mengine ya kawaida kama vile kutoka majimaji katika matiti (kama maziwa), kutapika, kutoka damu ukeni, kujaa na kuumwa matiti, kiungulia, kujihisi usingizi, kichefuchefu na maumivu ya misuli nayo yameripotiwa kuhusishwa na phyoestrogen.

Pamoja na kwamba phytoestrogens inaweza kuonekana kuwa ni salama lakini kitu chochote kinachohusisha muingiliano wa utendaji kazi wa hormone hakina budi kuchukuliwa kwa uangaliafu mkubwa.

Inasemekana kuwa vidonge vya chicken pills vina madini ya Arsenic. Kwa kawaida madini haya huchochea kuku kuwa na hamu ya kula kupita kiasi na hivyo kuongezeka ukubwa kwa muda mfupi. Binadamu anapotumia dawa zenye madini haya anajiweka katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali kama vile matatizo katika mfumo wa neva (ganzi), kuharisha na hata saratani ya ngozi na ini. Hii ni kutokana na mlundikano wa Arsenic mwilini.

Matumizi ya sindano za silicone oil yamehusishwa na kutokea kwa uvimbe katika maeneo ya makalio (granulomas), kusambaa kwa chembe chembe za silicone katika mitoki (lymph nodes), kuziba kwa mishipa la damu kwa sababu ya silicone (silicone embolism), kufa kwa seli za makalio (necrosis) na hata uwezekano wa kutokea kwa kansa ya ngozi.

Hitimisho

Pamoja na kwamba maelezo mengi ya watengenezaji wa madawa haya ama hayatoshelezi au hayaelezi madhara yake, jamii haina budi kuwa makini sana na matumizi yake. Aidha, kitendo cha dawa nyingi za aina hii kutokuwa na maelezo ya nini kilichomo (ingredients) inatia shaka sana. Hali kadhalika kukosekana kwa maelezo ya kina ya namna dawa hizo zinavyofanya kazi kunazidi kuongeza mashaka zaidi juu uwezo na usalama wa dawa hizo.

Ni wajibu wa mtumiaji kuchunguza kwa kupata maelezo ya kutosha juu ya aina ya dawa, nini kilichomo, zinafanyaje kazi, iwapo zimethibitishwa na athari zake kabla ya kuamua kutumia ama la.

Imesomwa mara 10400 Imehaririwa Jumatano, 26 Mai 2021 21:49
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.