Image

Matumizi Ya Vinywaji Nishati Yahusishwa na Unywaji Pombe wa Kupindukia

Unywaji wa vinywaji nishati  au vile vyenye kuongeza nguvu mwilini kwa mfano Red Bull unazidi kupata umaarufu mkubwa hasa miongoni mwa wanafunzi wa elimu ya juu. Wengi wa wanafunzi hawa hudai kuwa, vinywaji hivi huwaongezea nguvu ya kuweza kuwa macho na kujisomea kwa muda mrefu nyakati za usiku bila kuchoka hasa kipindi wanapojiandaa na mitihani yao. Aidha vinywaji hivi vinazidi kupata umaarufu miongoni mwa kundi jingine la vijana ambao mara nyingi hupendelea kuchanganya vinywaji hivi pamoja na pombe.

Kwa mujibu wa utafiti kuhusu unywaji wa vinywaji nishati uliofanywa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu kadhaa vya mjini Maryland na Taasisi moja huko Marekani, na matokeo yake kuchapwa katika jarida la Alcoholism: Clinical & Experimental Research, tabia hii ya unywaji wa vinywaji nishati imeelezwa kuwa inaweza kuwa hatari kwa afya za wanywaji. Matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa hali ya kupunguza uchovu na kutopata usingizi inayosababishwa na vinywaji hivi inaweza kumfanya mnywaji aongeze muda wa unywaji zaidi.

Aidha watafiti hao wameonesha kuwepo kwa ushahidi kuwa vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini hupunguza hisia ya ulevi wakati ambapo kiwango halisi cha ulevi mwilini tayari huwa kipo juu. Hali hii inaweza kuhatarisha zaidi hali ya mnywaji na pia kupelekea mnywaji kuwa mlevi sugu na hivyo kumuweka katika hatari ya kupata madhara makubwa zaidi ya pombe.

Wakiongozwa na tafiti zilizopita kuhusu hatari ya kuchanganya vinywaji nishati na pombe, Dr Arria (ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Afya na Maendeleo ya Vijana katika Chuo Kikuu cha Maryland)  na wenzake walichunguza ni kwa jinsi gani matumizi ya vinywaji nishati inavyoweza kusababisha hatari katika utegemezi wa pombe.

Utafiti huo ambao ulishirikisha jumla ya wanafunzi 1,097 wenye umri wa kati ya miaka 20 – 23 wa mwaka wa nne wa kimoja kikubwa cha Umma mjini Maryland ulifuata kipimo cha unywaji wa pombe kupindukia  kulingana na vigezo vya muongozoo wa ugonjwa wa akili. Aidha iliripotiwa kwamba karibu nusu ya wanafunzi wote walioshiriki kwenye utafiti huo walikuwa  watumiaji wadogo wa vinywaji hivyo, ambao walikuwa wakinywa kati ya siku moja mpaka siku 51 katika mwaka, na karibu asilimia kumi walikuwa watumiaji wakubwa wa vinywaji hivyo, ambao walikuwa wakinywa kwa zaidi ya siku 52.

Vilevile ilionekana kwamba watumiaji wakubwa wa vinywaji hivi, wana tabia pia ya kunywa pombe mara nyingi zaidi (siku 141.6 kwa mwaka kulinganisha na siku 103.1)  na kwa kiasi kikubwa zaidi (mara 6.15 kulinganisha na mara 4.64  kwa siku) ukilinganisha na wenzao wanaokunywa vinywaji nishati kwa kiwango kidogo. Aidha ilionekana kuwa watumiaji wakubwa wa vinywaji hivi walikuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuwa wategemezi wa pombe tofauti na wale ambao hakuwa wakinywa kabisa pombe.

Pamoja na matokeo hayo, hata hivyo utafiti huo ulishindwa kuonesha utofauti wowote wa utegemezi wa pombe kati ya wanywaji wanaokunywa kwa kiasi kidogo na wale wasio watumiaji kabisa wa vinywaji nishati.

Matokeo ya utafiti huu yanatoa picha ya kuwa, kuna umuhimu hasa miongoni mwa vijana wanaopenda kuchanganya vinywaji nishati na pombe au wale wanaotumia vinywaji nishati kupita kiasi kuwa makini katika tabia zao ili kuwaepusha na madhara yake.

Imesomwa mara 6678 Imehaririwa Jumatano, 13 Machi 2019 16:19
Dr. Paul J. Mwanyika

Dr. Paul J. Mwanyika ni Daktari  Bingwa waTiba na Uchunguzi wa Magonjwa ya Watoto (Pediatrics).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana