Bado tupo katika mwendelezo wa Makala yetu kuhusu kisukari na jinsi ya kuishi na kisukari. Katika makala ya kwanza katika mfululizo huu wa makala za kisukari, Ishi kwa kujiamini, kisukari sio mwisho wa Maisha, tulianza kwa kuangazia jinsi ya kuishi na kisukari, pia mambo makuu manne ya kuzingatia kwa wagonjwa wenye kisukari.
Baada ya kupata ufahamu juu ya umuhimu wa kujiamini kwa mtu anayeishi na kisukari,katika makala ya Jinsi ya kula kwa watu wenye Kisukari, tuliangazia suala la jinsi ya kula, maana hapo ndipo tatizo lilipo, watu wengi wenye tatizo la kisukari hawafahamu ni aina gani ya vyakula wanapaswa kula na wengine wanaingia kwenye gharama kubwa kununua vyakula tofauti wakiamini kuwa ni maalum kwa wenye kisukari.
Leo tunaangalia suala zima la udhibiti wa kisukari kwa mtu mwenye kisukari. Lazima ufahamu kuwa wewe mwenye kisukari ni Tabibu wa kwanza wa tatizo lako. Kuna matatibu wengi sana mitaani na wote wana utaalamu tofauti,pia kuna taarifa nyingi mitaani na kwenye mtandao ila ni jukumu lako wewe kujua ni taarifa gani sahihi na inayokufaa.
Unaweza kuambiwa kula aina hii ya chakula, usile aina ile ya chakula,acha kabisa kula aina hii ya chakula,kula sana aina ile ya chakula, mara kula sana aina hii ya matunda,usile aina ile ya matunda. Kwa mfano, wengi wanaambiwa wale ndizi changa kwa wingi,labda na ugali wa uwele,dona au ulezi kwa wingi. Sasa mathalani, umeenda sehemu ambapo hakuna ndizi changa,hakuna dona,ulezi au uwele, unataka kusema hautakula chakula? Utashinda na njaa? La Hasha, utakula tu, mwenye kisukari anakula aina zote za chakula, iwe wali,ndizi za kupika,pilau,biryani,viazi vya aina yote, maboga,sembe,dona n.k, cha msingi ni kujua ni jinsi gani au kwa utaratibu gani unaweza kula vyakula hivyo.
Tusipikiwe au tusitengewe chakula tofauti na cha familia, hapana, tunakosea sana, chakula cha familia ndio na wewe mwenye ugonjwa wa kisukari unaweza kula chakula hicho hicho, hakuna chakula maalum cha mtu mwenye kisukari,isipokuwa tu wewe mwenyewe ni lazima ufahamu ni jinsi gani unatakiwa ule au ni kwa utaratibu gani unatakiwa ule, ndio maana ninasema wewe mwenye kisukari ndiyo tabibu wa kwanza wa kisukari.mimi nitakushauri,mpishi atapika tu na chakula kitawekwa mizani, ila wewe ndiyo utajua jinsi ya kula.Wewe ni Tabibu wa kwanza wa kisukari chako.