Image

Matibabu ya Meno Yaliyojipanga Vibaya (Orthodontic treatment)

Baadhi ya watu wana meno yaliyojipanga visivyo. Katika hali ya kawaida meno yanatakiwa yawe katika mahusiano mazuri kiasi kwamba meno ya juu yaweze kukutana vizuri na yaliyo jirani yakae vizuri pia. Utakuta baadhi ya watu meno ya juu yamechomoza mbele sana kiasi kwamba hata kufunga mdomo ni tatizo, wengine ya chini kuvutika mbele zaidi na kuwa na kidevu kilichochongoka kwenda mbele na wengine yamepandana pandana.

Mpangilio mbaya wa meno unaweza kuwa mbaya zaidi kiasi cha kumughasi mhusika na wakati mwingine meno yenyewe kushindwa kufanya kazi zake vizuri. Tatizo lingine la meno yaliyojipanga vibaya ni vigumu kuyasafisha na hivyo kuyaweka meno katika hatari ya kuoza na kusababisha magonjwa ya fizi.

Nini kinasababisha matatizo haya?

  • Maumbile yatokanayo na vinasaba na urithi
  • Tabia kama kunyonya vidole utotoni hata ukubwani kwa wengine
  • Kuwahi kutoka meno ya utotoni
  • Kuchelewa kutoka kwa meno ya utotoni hivyo kuyafanya ya ukubwani kuota upande
  • Ajali wakati wa kujifungua ambayo inaweza kuathiri maeneo ya kukua kwa taya

Matibabu

Lengo kubwa la matibabu ni kuyaweka meno katika mpangilio unaokubalika, ili kuboresha muonekano, utafunaji na hata utamkaji wa maneno.

Matibabu huusisha kuwekewa nyaya kwenye meno ambazo husaidia kuyavuta na kuyaweka katika mpangilio mzuri. Nyaya zaweza kuwa za kufunga moja kwa moja kwa vifaa maalumu na kuwa vinafanyiwa marekebisho kadri meno yanavyozidi kujipanga (fixed orthodontic appliances); lakini pia nyaya hizi zaweza kuwa za kuvaa na kuondoa kadri mgonjwa anavyotaka (removable orthodontic appliances). Kama mpangilio ni mbaya zaidi, ili kufanikisha matibabu haya, yawezekana baadhi ya meno kuondolewa ili kutoa nafasi kwa yaliyobaki kujipanga.

Muda wa kuvaa nyaya hizi yaweza kuwa miezi sita au zaidi kulingana na ukubwa wa tatizo na wakati mwingine ushirikiano wa mgonjwa.

Muda mzuri wa kufanya matibabu haya ni pale ambapo mtoto bado anakuwa anakua (chini ya miaka 18). Zaidi ya umri huu matibabu huwa magumu, kuchukua muda mrefu na wakati mwingine kutoa matokeo ambayo hayaridhishi.

Kwa wale ambayo matatizo haya yanatokana na mojawapo ya taya kuwa dodo kuliko kawaida au kunyume chake basi upasuaji unatakiwa kupunguza au kuongeza taya husika.

Ni vizuri kuwaangalia watoto wetu mara kwa mara, kwani matibabu ni rahisi yakigundulika mapema.
Msisitizo tembelea kliniki ya meno wewe pamoja na familia yako angalau mara mbili kwa mwaka. Kumbuka matibabu ya meno ni gharama na bima nyingi zinayakimbia. Tiba ya mapema ni sawa na kinga.

Picha hapo chini zinaonyesha mgonjwa kabla, wakati na baada ya matibabu
 

                                            

Kabla ya matibabu
  

     Wakati wa matibabu


  
  Baada ya matibabu

Makala hii imeandikwa na Dr. Augustine Rukoma, daktari bingwa wa magonjwa ya kinywa na meno. Kwa makala zaidi, maswali na ushauri mtembelee kwenye blog yake ya http://rukomadentalanswers.blogspot.com

Imesomwa mara 20834 Imehaririwa Ijumaa, 14 Julai 2017 10:57
Dr. Augustine Rukoma

Dr Dr. Augustine Rukoma ni daktari na mtaalamu wa meno, anapenda kutumia muda wake wa ziada kuandika makala na kubadilishana mawazo juu ya afya ya kinywa na Meno.

rukomadentalanswers.blogspot.com | Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.