- Hatua ya kwanza huwa na GFR ya zaidi ya 90mL/dakika/1.73mita za mraba – mgonjwa huwa na madhara kidogo katika figo, huku figo zake zikiendelea kuchuja uchafu kama kawaida.
- Hatua ya pili ina GFR ya kati ya 60-89 mL/dakika/1.73mita za mraba - katika hatua hii, kiwango cha utendaji kazi cha figo hushuka kwa kiasi kidogo.
- Hatua ya tatu, GFR huwa kati ya 30-59 mL/dakika/1.73mita za mraba. Katika hatua hii utendaji kazi wa figo hupungua zaidi,
- wakati katika hatua ya nne GFR hushuka zaidi na kuwa kati ya 15-29 mL/dakika/1.73mita za mraba. Hapa utendaji kazi wa figo huwa wa chini mno;
- na hatua ya tano mgonjwa huwa na GFR chini ya 15 mL/dakika/1.73mita za mraba. Hatua hii huitwa pia kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo au CRF.
Katika makala tutatumia zaidi kifupisho cha CRF kumaanisha kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo (chronic renal failure).
Ukubwa wa tatizo (epidemiology)
Ugonjwa sugu wa figo ni maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea. Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha uthibiti wa magonjwa cha nchini marekani (CDC), Ugonjwa sugu wa figo ni miongoni mwa matatizo ya kiafya yanayojitokeza kuchukua chati za juu sana nchini humo. Ripoti hiyo ilionesha kuwa karibu asilimia 17 ya watu wazima wenye umri wa miaka 20 na kuendelea wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa figo.
Aidha ripoti hiyo ilionesha kuwa kribu watu nusu milioni wapo katika dialysis au wameshawahi kubadilishiwa figo. Mambo kadhaa yanahusishwa na ongezeko la ugonjwa sugu wa figo, miongoni mwayo ni ugonjwa kisukari, shinikizo la damu, unene na uzee. Aidha mabadiliko katika tabia na namna watu wanavyoishi pia vimeonekana kuchangia ongezeko hili kwa kiasi kikubwa.
Visababishi vya ugonjwa sugu wa figo
Pamoja na kwamba ugonjwa sugu wa figo hutokana na magonjwa kadhaa ambayo kimsingi yanaathiri figo lenyewe, visababishi vikuu vya ugonjwa sugu wa figo ni kisukari na shinikizo la damu.
- Kisukari cha aina ya 1 na ya 2 husababisha hali iitwayo kisukari cha figo au kwa lugha nyingine diabetic nephropathy.
- Shinikizo la damu kama lisipothibitiwa vema, baada ya muda fulani, husababisha madhara katika figo, hali inayoitwa hypertensive nephropathy.
Visababishi vingine vya ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na
- Magonjwa kama vile systemic lupus erythematosus pamoja na maambukizi ya bakteria jamii ya streptococci ambao husababisha madhara katika chujio la glomeruli na kusababisha ugonjwa unaoitwa glomerulonephritis. Glomerulonephritis huathiri mfumo wa uchujaji uchafu katika figo.
- Magonjwa ya kurithi ya figo kama vile Polycystic kidney disease. PKD huambatana na hali ya kuwa na vimbe ndogo ndogo zilizojaa maji (cysts) katika figo. Vimbe hizi hufanya figo ishindwe kufanya kazi zake sawasawa na hivyo kusababisha ugonjwa sugu wa figo.
- Matumizi ya kila siku ya muda mrefu ya baadhi ya madawa ya kutuliza maumivu kama vile ibuprofen (brufen) au acetaminophen yanaweza pia kusababisha ugonjwa sugu wa figo. Hali hii huitwa kitaalamu analgesic nephropathy. Matumi ya baadhi ya madawa kama antibiotiki za aminoglycosides kama gentamicin pia husababisha madhara katika figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo.
- Hali ya mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye figo kuzeeka, kupungua kipenya chake na kuwa migumu kiasi cha kushindwa kutanuka na kusinyaa vyema (atherosclerosis) husababisha upungufu mkubwa wa damu katika figo husika, kwa kitaalamu ischemic nephropathy, hali ambayo inaweza pia kusababisha madhara zaidi kwa figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo na hata CRF.
- Magonjwa kama vijiwe figo (kidney stones), kuvimba kwa tezi dume (BPH), kuziba kwa njia ya mkojo (urethra stricture) pamoja na saratani, vyote vinaweza pia kusababisha madhara katika figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo.
Vyanzo vingine vya ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na
- Maambukizi ya VVU ambayo husababisha hali inayoitwa HIV nephropathy
- Ugonjwa wa sickle cell ambao unaweza kusababisha kuziba kwa mirija inayosambaza damu kwenye figo au upungufu wa damu kwenye figo (renal tubula necrosis)
- Matumizi ya madawa ya kulevya
- Maambukizi sugu katika figo, na
- Saratani za figo.
Vihatarishi (Risk factors) vya Ugonjwa Sugu wa Figo
Mtu aliye na mojawapo ya vitu/magonjwa haya ana hatari kubwa ya kupata ugonjwa sugu wa figo hatimaye CRF. Wenye matatizo haya, hawana budi kuhakikisha kuwa figo zao zinafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kuangalia utendaji kazi wake.
- Kisukari aina zote mbili
- Shinikizo la damu
- Kiwango cha juu cha lehemu katika damu (hypercholesteraemia)
- Magonjwa ya moyo
- Magonjwa ya ini
- Magonjwa yanayohusiana na aina mbaya ya protini (Amyloidosis)
- Ugonjwa wa seli mundu (Sickle cell disease)
- Ugonjwa wa mzio/mcharuko mwili wa lupus (Systemic Lupus erythematosus)
- Magonjwa ya mishipa ya damu kama vile magonjwa ya mzio katika artery (arteritis) au vasculitis
- Matatizo katika njia ya mkojo ambapo mkojo badala ya kutoka nje (kushuka chini) hupanda kurudi ndani ya figo (Vesicoureteral reflux)
- Matumizi ya mara kwa mara ya madawa ya kutuliza mcharuko mwili/mzio
- Kuwa na historia ya magonjwa ya figo katika familia
Dalili za ugonjwa sugu wa figo
Figo zina uwezo wa ajabu wa kukabiliana na hali ngumu na matatizo katika utendaji kazi wake kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo basi, mgonjwa sugu wa figo anaweza kudumu katika hali yake kwa muda mrefu bila kuonesha dalili zozote zile.
Dalili za ugonjwa sugu wa figo hujitokeza pale utendaji kazi wa figo unapokuwa umeshuka na kufikia kiwango cha chini zaidi. Dalili hizo ni kama vile
- kukojoa sana hasa wakati wa usiku (nocturia)
- kuvimba uso na macho (facial puffiness)
- Kuvimba miguu (pedal oedema)
- Ongezeko la shinikizo la damu
- Uchovu na udhaifu wa mwili kutokana na upungufu wa damu au kurundikana kwa uchafu na sumu mwilini
- Kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika
- Mwili kuwasha, kupata michubuko kirahisi katika ngozi, na ngozi kuwa nyeupe (kwa sababu ya upungufu wa damu
- Kupumua kwa tabu kutokana na mrundikano wa maji katika mapafu
- Kichwa kuuma, kujihisi ganzi miguuni na/au mikononi (peripheral neuropathy), kupata shida ya kupata usingizi au kulala usingizi wa mang’amung’amu
- Mabadiliko katika uwezo wa utambuzi kwa sababu ya mdhara katika ubongo yanayosababishwa na mrundikano wa uchafu na sumu za urea
- Maumivu ya kifua kwa sababu ya mzio katika gamba la juu la moyo
- Kutokwa damu (kwa sababu ya ukosefu wa chembe sahani zinazosaidia damu kuganda)
- Maumivu ya mifupa na kuvunjika kirahisi, na
- Kukosa hamu ya tendo la ngono na kwa wanaume uhanithi (uume kushindwa kusimama)
Vipimo na Uchunguzi
Inashauriwa kwa watu wote wenye hatari ya kupata ugonjwa sugu wa figo, ni vema wafanye vipimo vifuatavyo ili kuchunguza maendeleo ya utendaji wa figo zao. Vipimo hivi ni pamoja na damu (FBP, pamoja na madini (electrolytes)), kipimo cha utendaji kazi figo (Renal function tests), mkojo, X-ray pamoja na Ultrasound. Vipimo hivi vinaweza kufanyika bila ya mgonjwa kuhitaji kulazwa hospitali.
Vipimo vinavyohusu mkojo
- Urinalysis: uchunguzi wa mkojo (urinalysis) husaidia kutoa picha ya utendaji kazi wa figo. Urinalysis husaidia kuchunguza kiwango cha protini katika mkojo pamoja na vitu vingine. Kwa kawaida mkojo huwa na kiasi kidogo mno cha protini (albumin), kwa hiyo kuwepo kwa protin kupita kawaida katika mkojo kunaweza kuashiria tatizo katika figo. Aidha mkojo pia huchunguzwa kwenye hadubini ili kuangalia uwepo wa vitu kama chembe nyekundu au nyeupe za damu, casts pamoja na vijiwe (crystals) kwenye mkojo.
- Kipimo cha mkojo uliokusanywa kwa masaa 24 (Twenty-four hour urine tests): Katika kipimo hiki, mkojo uliokusanywa kwa masaa 24 mfululizo huchunguzwa ili kuangalia uwepo wa protini, urea nitogen pamoja na creatinine. Uwepo wa protini kwenye mkojo huashiria matatizo katika figo wakati kiasi cha creatinine na urea husaidia kufahamu GFR ya figo za mgonjwa.
- Glomerular filtration rate (GFR): GFR ni kiwango kilichokubalika kitabibu katika kuelezea uwezo wa utendaji kazi wa figo. Kiwango cha kawaida cha GFR ni kati ya 100-140 mL/dakika kwa mita za mraba 1.73 kwa wanaume na 85-115 mL/dakika kwa wanawake. Kama tulivyoona hapo awali, kadiri jinsi figo zinavyozidi kudhurika, ndivyo GFR inavyozidi kupungua, hivyo kufahamu GFR ya mgonjwa husaidia kufahamu hatua mgonjwa aliyofikia na jinsi ya kumtibu.
Vipimo vinavyohusu damu
- Kiasi cha creatinine na urea nitrogen katika damu (BUN): Hivi ni vipimo vinavyotumiwa sana na madaktari wengi kuchunguza uwezo wa figo kutenda kazi zake. Creatinine inatokana na kuvunjika vunjika kwa kawaida kwa misuli ya mwili wakati urea ni zao chafu la kuvunjika kwa protini mwilini. Kwa vile zote huchujwa na figo, ongezeko lake mwilini huashiria kushindwa kufanya kazi kwa figo.
- Kiwango cha madini (Electrolytes) na uwiano wa tindikali na nyongo: Kushindwa kufanya kazi kwa figo husababisha uwiano usio sawa katika kiwango cha madini mwilini hususani madini ya potasium, phosphorus na calcium. Kwa mantiki hiyo hata uwiano wa tindikali na alkali huvurugika pia. Kiwango kikubwa cha madini ya potasium mwilini ni jambo la hatari zaidi kwa vile linaweza kusababisha shambulio la moyo na hatimaye kifo cha ghafla cha mgonjwa.
Kwa upande mwingine, kupungua kwa uzalishaji wa vitamini D katika figo husababisha kupungua kwa kiwango cha madini ya calcium katika damu, wakati kushindwa kutoa phosphorus nje ya mwili husababisha kiwango chake kuongezeka katika damu. Aidha, kiwango cha homoni za kiume au za kike kinaweza pia kuathirika kutokana na matatizo katika figo.
- FBP: Ugonjwa sugu wa figo husababisha mvurugiko katika uzalishaji wa chembe za damu pamoja na kufupisha maisha ya chembe nyekundu za damu kwa kuzifanya zivunjike kwa urahisi. Matokeo yake ni mgonjwa kuwa ni upungufu mkubwa wa damu pamoja na chembe nyeupe na chembe sahani. Baadhi ya wagonjwa huwa na kiwango kidogo cha madini ya chuma kwa sababu madini mengi hupotea kutokana na mgonjwa kutoka damu hususani katika kuta za utumbo wake.
Vipimo vingine
- Ultrasound: Kwa ujumla, ultrsound ya figo za mtu mwenye ugonjwa sugu wa figo huonesha figo ndogo zilizosinyaa, ingawa zinaweza kuwa na ukubwa wa kawaida ua kuongezeka kulingana na chanzo cha tatizo. Ultrasound ni kipimo cha muhimu sana katika kuchunguza matatizo kwenye figo kwa sababu, mbali na kuchunguza ukubwa wa figo, inaweza pia kusaidia kuonesha iwapo njia ya mkojo imeziba, uwepo wa vijiwe figo na pia kuonesha mtiririko wa damu kwenda kwenye figo.
- Biopsy: Hiki ni kipimo kinachofanywa kwa kuchukua kinyama kidogo cha figo na kukichunguza katika maabara. Kipimo hiki hufanywa iwapo chanzo halisi cha tatizo katika figo hakieleweki sawa sawa.
- MRI
- CT scan
- PET/SPECT/CT
Matibabu
Matibabu ya ugonjwa sugu wa figo yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu, yale yanayohitaji dawa, yasiyohitaji dawa na upasuaji.
Matibabu yasiyohitaji dawa (matibabu ya lishe)
Ni muhimu kwa mgonjwa kuzingatia yafuatayo:
- Kupunguza kiwango cha protini anachokula ili kupunguza kasi ya ugonjwa na kuharibika kwa figo.
- Kuthibiti matumizi ya chumvi katika chakula ili kuepusha mrundikano wa maji mwilini na kusaidia kuthibiti shinikizo la damu. Kiasi cha chumvi kinachoshauriwa ni kati ya gramu 4 mpaka 6 kwa siku.
- Kupunguza kiasi cha maji au vinjywaji unavyokunywa ili kusaidia kupunguza mrundikano wa maji mwilini.
- Kupunguza na kuepuka vyakula vyote vyenye madini ya Potassium kwa wingi. Vyakula kama ndizi, maji ya madafu, nyanya, karanga na machungwa.
- Kupunguza na kuepuka vyakula vyote vyenye madini ya Phosphorus kama vile mayai, maharage, vinywaji vyote vya jamii ya cola, na mazao yote ya maziwa, mtindi, jibini, siagi na jamaa zao. Hii husaidia kuilinda mifupa isizidi kuathirika.
- Acha uvutaji wa sigara
- Kama ni mnene, jitahidi kupunguza uzito kadiri itakavyoshauriwa na daktari
- Epuka kutumia madawa bila kushauriwa na daktari.
Matibabu yanayohitaji dawa
Bahati mbaya hakuna dawa inayoweza kutibu na kuponyesha ugonjwa sugu wa figo. Dawa hutumika kwa malengo ya kupunguza kasi ya ugonjwa, kutibu chanzo cha ugonjwa na viambata vyake, kutibu madhara yaletwayo na ugonjwa na kusaidia kurudisha kazi za figo.
Dawa/njia za kuthibiti na kupunguza kasi ya ugonjwa na kutibu chanzo chake ni pamoja na:
- Uthibiti wa kiwango cha sukari
- Uthibiti wa shinikizo la damu kwa kutumia dawa za jamii ya angiotensin converting enzyme (ACE) inhibitors kwa mfano captopril au zile za jamii ya angiotensin receptor blockers (ARB) husaidia zaidi.
Njia za kutibu madhara yaletwayo na ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na
- Kupunguza mrundikano wa maji mwilini kwa kutumia dawa za kutoa maji (diuretics) kama vile frusemide.
- Kutibu upungufu wa damu mwilini kwa kutumia dawa zinazosisimua kiasili cha erytropietin na hivyo kuchochea uzalishaji wa chembe za damu, kwa kumpatia mgonjwa madini ya chuma.
- Kuthibiti magonjwa ya mifupa kwa kumpatia mgonjwa dawa za kupunguza na kutoa nje madini ya phosphorus na kuongeza vitamini D.
- Kuthibiti utindikali mwilini kwa kutumia dawa za jamii ya alkali kama vile sodium bicarbonate.
Matibabu mengine/Upasuaji
Matibabu mengine ni pamoja na dialysis au kupandikizwa/ kubadilishwa kwa figo kwa njia ya upasuaji (renal transplantation).
Kinga
Katika mazingira mengi, ugonjwa sugu wa figo hauwezi kuzuilika. Mgonjwa anaweza kupunguza kasi ya kudhurika kwa figo zake kwa kuthibiti vyanzo mbalimbali vya ugonjwa huu kama vile kisukari au shinikizo la damu.
Mambo mengine ya kuzingatia ni kuepuka matumizi ya kupitiliza ya madawa na kemikali ambazo zina athari katika figo.