- Jinsia: Ingawa, saratani ya matiti huweza kutokea kwa wote wanawake na wanaume, imeonekana kuwa wanawake ni waathirika wakubwa zaidi wa saratani hii ikilinganishwa na wanaume.
- Umri: Uwezekano wa kupata saratani hii huendana na umri wa mtu. Kadiri umri wa mtu unavyoongezeka ndivyo pia uwezekano wa kupata saratani hii unavyozidi kuwa mkubwa. Wanawake walio na umri wa kuanzia miaka 50 wapo kwenye hatari kubwa (mara 2 au 3 zaidi) kuliko walio na umri wa miaka 45.
- Uasili wa mtu (ethnicity): Saratani ya matiti hutokea zaidi kwa wanawake wazungu kuliko wanawake wa kiafrika au wenye asili ya afrika (weusi).
- Uzazi: Wanawake ambao hawajazaa au kunyonyesha wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti. Wanawake wanaopata ujauzito kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 nao pia wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii.
- Historia ya ugonjwa huu katika familia: Wanawake walio katika familia zenye historia ya ugonjwa huu wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale ambao hawana historia ya ugonjwa huu katika familia zao. Kwa mwanamke aliye na ndugu (mama, dada au mtoto) ambaye aliwahi kupata saratani hii kabla ya umri wa miaka 50, uwezekano wa mwanamke huyu kupata ugonjwa huu ni mara mbili ya yule ambaye hana historia hii.
- Umri wa kuvunja ungo: Wanawake wanaovunja ungo (kupata hedhi) kabla ya umri wa miaka 12 wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.
- Kuacha kupata hedhi: Kwa kawaida wanawake huacha kupata hedhi wafikapo miaka 45, hali ambayo kitaalamu hujulikana kama menopause. Wanawake wanaochelewa kuacha kupata hedhi, kwa mfano wale wanaoendelea kupata hedhi wakiwa na zaidi ya miaka 45, wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya matiti.
- Historia ya saratani ya matiti: Wanawake ambao wamewahi kupata ugonjwa huu kwenye titi la upande mmoja hapo kabla, wana uwezekano mkubwa wa kupata tena saratani kwenye titi la upande mwingine hapo siku za usoni.
- Ulaji wa vyakula venye mafuta mengi: Tafiti zinaonesha kuwa, wanawake wanaopendelea kula vyakula vyenye mafuta mengi wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.
- Kuongezeka uzito: Tafiti nyingine zimeonesha kuwa, wanawake wanene wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale wa uzito mdogo au wa kati.
- Uvutaji sigara: Kuna matokeo yenye kukinzana kuhusu uhusiano wa uvutaji sigara na hatari ya kupata saratani ya matiti. Wakati baadhi ya tafiti zinaonesha uhusiano wa karibu kati ya uvutaji sigara na uwezekano wa kupata saratani ya matiti, tafiti nyingine zinaonesha majibu yenye kutofautiana kuhusu uhusiano wa uvutaji wa sigara na saratani ya matiti. Hata hivyo, kwa ujumla, wanawake wanaojizuia kuvuta sigara wanakuwa na afya njema zaidi kuliko wale wanaovuta sigara.
- Unywaji pombe: Imeonekana kuwa wanawake wanaokunywa pombe zaidi ya chupa moja kwa siku wana uwezekano wa kupata saratani ya matiti kwa asilimia zaidi ya ishirini.
- Historia ya tiba ya mionzi: Wanawake ambao wamewahi kupata tiba ya mionzi hususani wakati wa ukuaji wa matiti, wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu. Hali hii husababishwa na ukweli kuwa mojawapo ya madhara ya mionzi ni kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya aina yoyote.
- Matumizi ya dawa za kupanga uzazi: Kuna ushahidi kuwa saratani ya matiti ina uhusiano na matumizi ya muda mrefu ya vidonge vya kupanga uzazi.
- Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni mwilini: Kwa wale wanaotumia tiba ya homoni inayojulikana kama hormone replacement therapy, kwa sababu nyingine yeyote ile, au wale wenye kiwango kikubwa cha homoni kama vile oestrogen na progesterone mwilini mwao wapo kwenye hatari zaidi ya kuugua saratani ya matiti.
- Kuwa na matiti makubwa: Wanawake wenye matiti makubwa (dense breast tissue) wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti. Hali hii hutokana na ukweli kuwa wakati mwingine ni vigumu sana kwa madaktari kutambua kama wana saratani au la kutokana na ukubwa wa matiti yao.
Saratani husambaa vipi?
Kwa kawaida saratani husambaa kwa njia tatu zifuatazo
- Kupitia tishu - Saratani husambaa kwenye tishu za kawaida ambazo zimezunguka eneo la saratani.
- Kupitia mfumo wa limfu (lymphatic system) - Saratani huvamia mfumo wa lymph na kufuata mishipa yake hadi sehemu nyingine za mwili.
- Kupitia damu - Saratani inaweza kusambaa kupitia damu kwa kuvamia mishipa ya damu ya vena na capillaries (veins and capillaries) na kusafiri kutumia damu hadi sehemu nyingine za mwili.
Dalili za Saratani ya Matiti
Dalili ya awali inayoweza kutambulisha saratani ya matiti ni kuwepo kwa uvimbe kwenye titi ambao huwa na hali tofauti na sehemu nyingine za titi. Hata hivyo, si kila uvimbe kwenye titi unaashiria uwepo wa saratani ya matiti. Uvimbe huu huwa mgumu, unaochezacheza kwenye titi, ambapo wakati mwingine unaweza kuwa na maumivu makali au kusiwe na maumivu yeyote. Uvimbe huu huwepo zaidi ya mzunguko mmoja wa hedhi kwa wale ambao hawajaacha kupata hedhi.
Dalili nyingine ni pamoja na
Kuwepo kwa uvimbe kwenye sehemu za kwapa
- Sehemu ya titi kuingia ndani inayoashiria uvimbe usioonekana au usioweza kuhisiwa
- Mabadiliko kwenye chuchu, kama vile chuchu kuzama ndani au kuwa na nundu ndogo ndogo, chuchu kuwasha, kuhisi kama kuchoma, kidonda kwenye chuchu au chuchu kuwa na kovu ambalo huashiria saratani ya sehemu hiyo
- Kubadilika kwa umbo la titi, ngozi ya titi kuwa kama ganda la chungwa (peu de orange), ngozi kuwa na rangi nyekundu, na kuongezeka kwa joto kwenye titi. Dalili hizi huashiria kusambaa kwa saratani mwilini.
- Dalili nyingine ni chuchu kutoa maji yasiyo ya kawaida ambayo hayana rangi. Aidha wakati mwingine, chuchu hutokwa damu au majimaji yenye rangi nyingine tofauti.
Ugunduzi wa Saratani ya Matiti
- Pamoja na mgonjwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na wataalamu wa afya kuweza kutambua uwepo wa tatizo hili, anaweza pia kufanyiwa vipimo vifuatavyo ili kusaidia kutambua ugonjwa huu.
- X-ray ya matiti au Mammogram ambayo ina uwezo wa kuonesha ulipo uvimbe kwenye matiti
- Ultra-Sonography ni kipimo kinachosaidia kutambua iwapo uvimbe uliopo ndani ya matiti umejaa maji ama la ili ufanyiwe vipimo zaidi
- Kipimo kinachofanywa kwa kuchukua sehemu ya uvimbe (Aspiration) kwa kutumia aina fulani ya sindano (fine needle) na kisha kupeleka maabara sehemu iliyochukuliwa kwa ajili ya kutafitiwa zaidi ili kugundua uwepo wa saratani. Kwa kitabibu kipimo hiki hujulikana kama Fine Needle Aspiration and Cytology (FNAC)
- Kipimo kingine ni upasuaji mdogo unaofanywa kwenye titi lililoathirika kwa ajili ya kuchukua sehemu ya titi (surgical biopsy) na kisha kuipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
- Sentinal lymph node biopsy - Kipimo hiki hufanywa ili kujua kama saratani imesambaa hadi kwenye tezi.
Aidha kwa nchi zilizopiga hatua ya kimaendeleo, mgonjwa anaweza pia kufanyiwa vipimo kama
- PET Scan: Hii ni aina mpya ya kipimo ambacho kinahusisha CT Scan na PET kwa pamoja. Kipimo hiki kina uwezo wa kutambua uwepo wa saratani ya matiti, iwapo saratani hiyo imesambaa ama bado, na kama itakuwa imeshasambaa, basi ni sehemu gani ya mwili iliyoathirika.
Aidha kipimo hiki, kina uwezo wa kutofautisha tezi au lymph nodes zilizovimba zina uhusiano na saratani (Metastatic lymph nodes) au hazina uhusiano na saratani (Benign lymph nodes).
Baadhi ya matabibu hupata taabu kutofautisha kati ya kuvimba kwa tezi kunakosababishwa na saratani na kule kunakosababishwa na vitu vingine tofauti na saratani. Hali hii hutokea kwa wagonjwa wa saratani wenye tezi zilizovimba ambao hudhani kuwa kuvimba huko ni sababu ya saratani (metastatic lymph nodes).
Kipimo hiki pia husaidia madaktari kuwatibu wagonjwa wa saratani kwa kutumia mionzi kwa usahihi zaidi ( Precise Radiotherapy) au kutumia mionzi inayolekezwa na kipimo hiki (PET Scan guided radiotherapy). Aidha, PET Scan huweza pia kutumika kuonesha maendeleo ya mgonjwa wa saratani baada ya kupata tiba ya mionzi (Radiotherapy) au dawa za kutibu saratani (Chemotherapy).
- Kipimo kingine hujulikana kama DCE MRI (Dynamic contrast MRI). Hiki nacho ni kipimo kipya kwenye ugunduzi na tiba ya saratani. Aina ya kipimo hiki hutofautina na kipimo cha MRI ya kawaida kwani DCE MRI ina uwezo wa kutoa maelezo ya ziada namna uvimbe wa saratani unavyopata damu yake kupitia mishipa ya damu (blood vessels of the tumor) na hivyo kukua na kuongezeka zaidi. Uwezo mwingine wa DCE MRI ni kutoa maelezo mengine sawa na PET Scan.
Hata hivyo, vipimo hivi vya PET Scan na DCE MRI kwa sasa havipatikani nchini Tanzania.
Tiba ya saratani ya matiti
Upasuaji
Lengo kuu la upasuaji ni kuondoa saratani kwenye titi pamoja na tezi (lymph nodes). Zipo aina kadhaa za upasuaji unaoweza kufanywa kwenye titi lililogundulika kuwa na saratani. Aina hizo ni pamoja na
- Lumpectomy: Huu ni upasuaji unaofanywa kuondoa sehemu ya saratani pamoja na sehemu ya titi ambayo haijaathirika kwa saratani. Hii hufuatiwa na tiba ya mionzi (radiotherapy) kwa muda wa kati ya wiki 6 au 7. Mgonjwa anayefanyiwa aina hii ya upasuaji anakuwa na uwezekano wa kuishi muda mrefu sawa na anayefanyiwa upasuaji wa kuondoa titi lote lililoathirika.
- Simple ama Total mastectomy: Ni aina ya upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika kwa ugonjwa wa saratani.
- Radical mastectomy: Aina hii ya upasuaji uhusisha uondoaji wa titi lote na kundi la tezi liloathirika kwa saratani, pamoja na misuli ya sehemu za kifua (chest wall muscles). Hata hivyo, upasuaji wa aina hii ni nadra sana kutumika siku hizi.
- Modified radical mastectomy: Ni aina ya upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika pamoja na kundi lote la tezi (lymph nodes) chini ya mkono (axilla) bila kuhusisha uondoaji wa misuli ya kifua.
Kwa ujumla, lumpectomy na mastectomy, zote zinahusisha uondoaji wa kundi la tezi ambalo lipo karibu na uvimbe wa saratani (regional lymph nodes).
Tiba ya mionzi
Mionzi inaweza kutumika kuharibu seli za saratani zilizobaki kwenye matiti, kifua (chest wall), au/na eneo la chini ya mkono mara baada ya upasuaji kufanyika. Mionzi pia inaweza kutumika kupunguza ukubwa wa uvimbe wa saratani kabla ya kufanyika kwa upasuaji.
Tiba ya saratani kwa njia ya dawa (Systemic therapy)
Tiba ya aina hii inahusisha matumizi ya kemikali maalum za kutibu saratani (chemotherapy) pamoja na matumizi ya homoni (hormonal therapy).
Tiba kwa kutumia homoni (Adjuvant hormonal therapy) hutumika ili kuua seli za saratani ambazo hazikugundulika hapo awali na ambazo yawezekana zimesambaa sehemu nyingine za mwili. Tiba hii hutolewa baada ya kufanyika kwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa saratani.
Aina hii ya tiba hutegemea na ukubwa wa uvimbe, matokeo ya vipimo vya kimaabara vya saratani (histological results), na iwapo saratani imesambaa hadi kwenye tezi za kwenye kwapa la mgonjwa ama la. Tiba hii pia yaweza kutolewa kwa mgonjwa ambaye saratani imeshasambaa mwilini kwake kwa muda mrefu, na ambaye hawezi kufanyiwa upasuaji. Baadhi ya kemikali zinazotumika kutibu saratani ya matiti ni cyclophosphamide, methotrexate, na flouracil. Kwa kawaida dawa hizi hutolewa kwa kujumuisha dawa 2 au 3 kwa wakati mmoja.
Ieleweke pia kuwa, kama ilivyo kwa dawa nyingine za kutibu magonjwa mengine tofauti na saratani, kemikali (dawa) hizi za saratani pia zina madhara mbalimbali kwa mtumiaji. Madhara haya huletwa na ukweli kuwa, pamoja na kuwa kazi kuu ya kemikali hizi ni kuua seli zenye saratani, hutokea pia kuua na kuathiri seli za kawaida yaani zisizo na ugonjwa wa saratani kama vile seli zilizo kwenye mdomo, nywele, pua, kucha, utumbo na hata sehemu za siri za mwanamke.
Hata hivyo, tofauti na seli za saratani, seli za kawaida huwa na uwezo wa kujizaa tena, kukua na kurudi katika hali yake ya kawaida wakati zile za saratani hazina uwezo huo. Madhara ya dawa hutofautiana kati ya mgonjwa mmoja na mwingine.
Dalili za saratani kusambaa mwilini
- Maumivu ya mifupa
- Maumivu kwenye titi
- Vidonda kwenye ngozi
- Kuvimba mkono karibu na eneo la saratani
- Kupungua uzito.