Image

Wagonjwa wa Saratani ya Uume (Penile Cancer)  Huweza Kushiriki Tendo Ndoa?

Watafiti kutoka kampasi ya chuo cha Gustave Roussy Cancer Campus cha nchini Ufaransa wamesema ya kwamba matibabu ya saratani ya uume kwa kutumia brachytherapy (mionzi) husaidia wagonjwa wa saratani hii kuwa na uwezo wa kushiriki katika tendo la ndoa hata baada ya matibabu.

Katika utafiti wao uliwahusisha wagonjwa 201 wenye saratani ya uume (penile cancer) na wenye umri zaidi ya miaka 45, asilimia 79 ya wagonjwa wote walichagua tiba ya mionzi (brachytherapy) na hivyo kuweza kuishi kwa angalau miaka kumi baada ya kufanyiwa matibabu haya.Chama cha  saratani (American Cancer Society)  nchini Marekani kinasema, ni aslimia 85 tu ya wagonjwa wote wa saratani ya uume wanaotibiwa kwa njia ya upasuaji  ambao huweza kuishi kwa angalau miaka kumi baada ya kufanyiwa upasuaji.

Utafiti huu uliofanyika nchini Ufaransa, ulifanyika kwa  wagonjwa wote 201 kutahiriwa kwanza na baadae kutibiwa kwa brachytherapy.Tiba hii ya brachytherapy hufanywa kwa mgonjwa kuwekewa kipande cha waya chenye kutoa mionzi kwa dozi ndogo kwenye uvimbe wa saratani au karibu na saratani yenyewe na hivyo kufanikiwa kuua chembechembe za saratani katika sehemu husika.

Uwezekano wa mgonjwa kuishi (survival rate) na uume wake kamili, miaka mitano baada ya matibabu ni asilimia 85.Kwa ujumla, ni asilimia 79 tu ya wagonjwa ambao waliweza kuishi kwa miaka kumi baada ya matibabu na kati yao, aslimia 82 hawakupata tena saratani hii ya uume.

Wagonjwa 8 walilazimika kuondolewa dhakari (penis) zao kabisa na 18 wengine waliondolewa baadhi ya sehemu za dhakari zao.

Wagonjwa wa saratani ya uume ambao wapo kwenye hatari ya kupata saratani hii tena baada ya matibabu ni wale ambao kabla ya kupatiwa matibabu, saratani yao ilikuwa tayari imeshasambaa kwenye mafundo fundo (lymph nodes) yaliyopo kwenye nyonga.

Kati ya wale waiotibiwa, wagonjwa 13 (asilimia 6) walihitaji tiba ya upasuaji ili kuondoa madhara  ya saratani hii ambayo yalikuwa ni vidonda venye kuambatana na maumivu makali.

Hata hivyo, ilionekana ya kwamba wagonjwa waliokuwa na  uvimbe wa saratani  wenye upana wa zaidi ya 4cm kabla ya matibabu, ndio walikuwa kwenye hatari zaidi ya kupata tena saratani hii ya uume.

Matokeo ya utafiti huu yameonyesha ya kwamba matibabu ya mionzi (brachytherapy)ni tiba nzuri kwa wagonjwa wa saratani ya uume ambayo haijasambaa kwenye eneo la uume linalojulikana kama corpus cavernosum.Tiba hii ya mionzi mbali na kutibu saratani hii husaidia wagonjwa kubakiwa na dhakari zao (intact penis).Na iwapo maambukizi ya saratani ya uume yatajirudia, basi yanaweza kutibiwa tena kwa tiba hii ya mionzi au kutumia tiba ya upasuaji pasipo kuwa na hofu ya kufariki kwa mgonjwa.

Hii inamaanisha ya kwamba, wanaume wanaotibiwa kwa kutumia tiba ya mionzi, wanakuwa ni watu wenye kujiamini kwa kuwa bado wanamiliki sehemu muhimu ya mwili wao (uume) hivyo  bado kuwa na uwezo  wa kushiriki tendo la ndoa pamoja na kutoa mkojo kupitia sehemu hii husika.

Saratani hii ya uume (penile cancer) huonekana sana katika nchi zinazoendelea kama nchi za Paraguay, Uruguay,Uganda na Brazil ambapo katika nchi ya Uganda, huathiri watu 4.4 kwa kila watu 100,000.

Visabababishi vya saratani hii ni pamoja na ugonjwa wa HIV, virusi vya Human Papilloma Virus, Genital Warts, uchafu kwenye uume, matumizi ya tumbaku, kuwepo kwa uchafu mweupe kwenye ngozi ya uume hasa kwa wale ambao hawajatahiriwa.

Tiba ya saratani hii ya uume ni pamoja na tiba ya upasuaji (inayoweza kuondoa baadhi ya sehemu tu ya uume au kuondoa uume wote kwa ujumla) na tiba ya mionzi.

Imesomwa mara 21253 Imehaririwa Jumatatu, 11 Juni 2018 13:02
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.