Image

Saratani ya Kibofu cha Mkojo

Utangulizi

Kibofu cha mkojo kinapatkana sehemu ya chini ya maeneo ya tumbo na ni kiungo ambacho kina uwazi/tundu ndani yake na kazi yake kubwa ni kukusanya na kuhifadhi mkojo unaotolewa na figo kabla ya kuutoa nje ya mwili wa binadamu. Kibofu cha mkojo kina kuta (layers) aina tatu za tishu ambazo ni;

1.Mucosa layer – Kuta ya ndani kabisa ambayo ndio inayokutana na mkojo wa binadamu. Kuta hii nayo inakuta nyingi sana za seli au chembechembe zinazojulikana kama transitional epithelium cells ambazo pia hupatikana kwenye sehemu ya mirija inayojulikana kama ureters, urethra na kwenye figo. Seli hizi zinazuia uvujaji wa mkojo kwenda kwenye sehemu nyengine ya mwili.

Ureter huingiza mkojo kutoka kwenye figo na urethra hutoa mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kukojoa.

2.Lamina propia – Kuta ya katikati nyembamba sana kati ya kuta  hizi tatu na  ambayo mishipa ya damu na neva inapatikana hapa na ni muhimu sana  wakati wa kupanga makundi ya saratani ya kibofu cha mkojo wakati wa tiba.

3.Muscularis layer -  Kuta ya nje ambayo ndani yake kuna destrusor muscle na ndio kuta nene kati ya hizi tatu. Kazi yake kubwa ni kupumzisha kibofu cha mkojo ili mkojo uingie ndani na ukishajaa basi hukaza kibofu (contracts) na kufanya mkojo kutoka nje.

Nje ya hizi kuta tatu, kibofu cha mkojo kimezungukwa na  mafuta ambayo hukinga kibofu kutokana na mtikisiko wowote na kukitenganisha na viungo vengine. Kuna saratani aina tatu kutokana na kuta hizi tatu nilizotaja hapo juu za kibofu cha mkojo

  • Urothelial carcinoma (transitional cell carcinoma) – Hii ndio aina ya saratani inayotokea kwa wingi na hutokea kwenye seli za transitional epithelium cells. Asilimia 90 – 95 ya saratani zote za kibofu cha mkojo huwa ni aina hii.
  • Squamous cell carcinoma – Aina hii hutokea baada ya maradhi ya kwenye kibofu cha mkojo kwa muda mrefu kama vijiwe vya kibofu cha mkojo (bladder stones) na huchukua asilimia 1- 2 ya saratani zote za  kibofu cha mkojo. Huonekana sana maeneo ya mashariki ya kati na afrika. Aina hii ina uhusiano mkubwa na ugonjwa wa kichocho (schistosomiasis) cha muda mrefu.
  • Adenocarcinoma – Hutokea baada ya inflammation ya kwenye kibofu cha mkojo kwa muda mrefu. Na huchukua asilimia 2 ya saratani zote za kibofu cha mkojo.

Vihatarishi vya saratani ya kibofu cha mkojo

  • Wale wanaofanyakazi kwenye saluni za nywele
  • Wanaofanya kazi ya kupaka rangi
  • Wafanyakazi wa viwanda vya nguo
  • Wanaofanya kazi kwenye viwanda vya ngozi
  • Wafanyakazi wa viwanda vya mipira (rubber)
  • Uvutaji sigara – Wavutaji sigara wako kwenye hatari ya kupata saratani hii mara mbili zaidi ya wale wasiovuta sigara.
  • Asili ya mtu – Saratani hii huonekana zaidi kwa watu weupe kuliko watu weusi. Watu wa mashariki ya kati wanaasilimia ndogo zaidi.
  • Umri – Huonekana zaidi kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 40 lakini huweza kutokea kwenye umri wowote ule.
  • Jinsia – Hutokea sana kwa wanaume  mara mbili au tatu  zaidi kuliko  kwa wanawake
  • Lishe – Watu wanaokula kwa wingi nyama za kukaanga kwa mafuta na kutumia mafuta yatokanayo na wanyama wakati wa kupika wako kwenye hatari kubwa kupata saratani hii. Aristolochia fangchi ni mti wa mitishamba unaotumiwa na watu wa  jamii ya Wachina katika kupunguza uzito kwa wale wenye uzito uliopitiliza na hata kwenye baadhi ya dawa za kichina, watu wanaotumia mti huu au dawa inayotokana nao pia wako kwenye hatari kubwa sana kupata saratani hii.
  • Historia ya matumizi ya dawa za saratani kama za saratani ya matiti nk.
  • Historia ya saratani ya kibofu cha mkojo kwenye familia. Inahusishwa na mabadiliko katika viashiria vya asili au jena (genes) aina ya HRAS, KRAS2, RB1, FGFR3.
  • Madereva wa malori (truck drivers)  – Pia wako kwenye hatari kubwa

Baadhi ya kemikali zinauhusiano na saratani ya kibofu cha mkojo kama

Dalili na viashiria vya saratani ya kibofu cha mkojo

  • Kukojoa damu (gross haematuria) ambayo inaweza kuonekana kwa macho au kwa hadubini (microscopic haematuria)
  • Maumivu wakati wa kukojoa au kichomi wakati wa kukojoa (burning sensation)
  • Kukojoa mara kwa mara (frequency of urination)
  • Maumivu  nyuma ya mgongo
  • Kuhisi bado mtu hajamaliza mkojo baada ya kukojoa awali
  • Kuhisi mkojo ambao hautoki
  • Kushindwa kujizuia kukojoa baada ya kukojoa awali (urgency)
  • Uvimbe wa saratani ndani ya kibofu cha mkojo

Dalili na viashiria vengine ni

  • Maumivu ya tumbo
  • Upungufu wa damu mwilini
  • Uzito kupungua
  • Maumivu ya mifupa
  • Kujikojolea

Baadhi ya dalili na viashiria hivi vinaweza kuonekana kwa wagonjwa wa saratani ya figo, tezi dume na cystitis.

Vipimo vya uchunguzi

  • Cystoscopy – Mpira unaoingiziwa kwenye mrija wa wa kutolea mkojo ambao una kamera mbele na taa ili kuchunguza kama kuna uvimbe wa saratani  ya kibofu cha mkojo na kuchukua nyama kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara zaidi
  • Biopsy – Nyama iliyochukuliwa kwa kipimo hapo juu, huchunguzwa kwenye maabara ili kuthibitisha  kama ni saratani
  • Ultrasound ya tumbo  na nyonga – Kuangalia kama kuna uvimbe kwenye  kibofu cha mkojo au kwenye figo. Inaweza kugundua sababu nyengine ya kukojoa damu kama vijiwe kwenye kibofu cha mkojo (bladder stones)  au uvimbe kwenye tezi dume (prostate enlargement).
  • Kipimo cha mkojo (Urinalysis) – Kinaweza pia kugundua sababu ya kukojoa damu  na kama kuna ugonjwa mwengine wowote wa kibofu cha mkojo
  • Kipimo cha damu (Complete blood count) – Kuangalia wingi wa damu, kundi la damu iwapo mgonjwa atahitaji kuwekewa damu nk.
  • CT scan na MRI – Husaidia katika uchunguzi wa saratani kwani hutoa maelezo mazuri na pia huweza kugundua saratani kama ipo kwenye figo, nyonga na sehemu nyengine mwilini.
  • Pyelography – Hii ni aina ya x-ray ya kibofu cha mkojo ambayo hupigwa mgonjwa baada ya kuchomwa dawa maalum (contrast dye)  kwenye mishipa ya damu (Intravenous pyelography)  au kwenye mrija wa kutoa mkojo (urethtra) na hujulikana kama retrograde pyelography.
  • Bone scan – Kuangalia kama saratani imesambaa hadi kwenye mifupa
  • Picha ya kifua (Chest X-ray) – Kuangalia kama saratani imefika kwenye mapafu.

Makundi ya saratani ya kibofu cha mkojo

Kabla ya mgonjwa kupewa tiba, ni muhimu kwa daktari kwanza kujitahidi kujua kundi (stage)  la saratani aliyonayo mgonjwa. Saratani hii imepangwa katika makundi tofauti kulingana na kama inaweza kutibiwa kwa njia ya upasuaji, kama imeenea hadi kwenye tezi (lymph nodes) na kama saratani imesambaa kwenye sehemu nyengine mwilini.

Umuhimu wa kupanga makundi ya saratani

  • Inasaidia kuchagua tiba sahihi ya saratani ya mgonjwa
  • Saratani iliyo ndani sana inauwezekano mkubwa wa kusambaa kwenye tezi na sehemu nyengine mwilini kuliko ile ambayo ipo juu.
  • Kadri  namba ya kundi inapoongezeka ndio ugonjwa ulivyo mbaya zaidi na asilimia ya kuishi kwa muda mrefu hupungua.
  • Husaidia katika kuwapanga wagonjwa kwenye makundi na hivyo basi kuweza kuwafanyia utafiti kutumia matibabu mapya kwa urahisi  zaidi.

Makundi ya saratani ya kibofu cha mkojo ni kama yafuatavyo

  • Stage 0 – Seli za saratani  zinapatikana kwenye kuta ya ndani ya kibofu cha mkojo tu.
  • Stage I – Seli za saratani zimeenea kutoka kwenye kuta ya ndani ya kibofu cha mkojo lakini hazijafika kwenye nyama (muscles)  ya kibofu cha mkojo
  • Stage II – Seli za saratani zimefika kwenye nyama za kibofu cha mkojo lakini hazijafika kwenye  tishu za  mafuta zilizozunguka kibofu cha mkojo.
  • Stage III – Seli za saratani zimefika kwenye tishu za mafuta zinazozunguka kibofu cha mkojo hadi kwenye tupu ya mwanamke (vagina), tezi dume (prostate), mfuko wa uzazi (uterus) lakini hazijafika kwenye tezi (lymph nodes) au kwenye viungo vengine mwilini.
  • Stage IV – Seli za saratani zimefika kwenye tezi, nyonga, kuta za tumbo (abdominal wall) na viungo vengine mwilini.
  • Recurrent – Saratani imejirudia kwenye kibofu cha mkojo au kwenye viungo vengine baada ya kutibiwa hapo awali.

Saratani ya kibofu cha mkojo inakawaida ya kusambaa kwenye tezi, na kupitia kwenye damu hadi kwenye mapafu, ini, mifupa na sehemu nyengine za mwili.

Tiba ya saratani ya kibofu cha mkojo

Saratani hii ni kati ya saratani zinazojulikana kuwa na asilimia kubwa ya kujirudia baada ya kutibiwa.Saratani ya kibofu cha mkojo ina uwezekano mkubwa wa kutibika kama itagundulika mapema. Tiba hutegemea ;

  • Aina ya saratani
  • Kundi la saratani (stage)
  • Historia ya kutibiwa saratani yoyote hapo awali
  • Umri wa mgonjwa
  • Afya ya mgonjwa (ili kuweza kujua kama mgonjwa atahimili aina ya tiba, kuna wagonjwa wengine huwa wanakuwa wamedhoofika sana).

Tiba imegawanyika kwenye

  • Tiba ya mionzi
  • Tiba ya dawa
  • Tiba ya upasuaji
  • Tiba ya immunotherapy ama biological therapy

Tiba ya mionzi (Radiation therapy)

Mionzi hutumika kuua seli za saratani. Tatizo la tiba hii ni kwamba inaua seli za saratani pamoja na seli za kawaida na hutumika kama njia mbadala ya tiba ya upasuaji. Matumizi yake ni kwenye saratani ndogo zilizoathiri nyama ya kibofu cha mkojo. Tiba hii ipo ya aina mbili;

  • Mionzi inayotolewa kwa kutumia mashine ya mionzi (external radiation)
  • Mionzi inayotolewa kwa kupachika kifaa cha kutolea mionzi ndani ya mwili kwa kukiingiza kupitia kwenye mrija wa kutoa mkojo (urethra) au kupitia upasuaji mdogo kwenye maeneo ya kibofu cha mkojo na kukiweka kifaa hicho ndani ya kibofu cha mkojo (Internal radiation).

Madhara ya tiba ya mionzi ni kama yafuatayo

  • Kujisikia uchovu au kuchoka
  • Kichefuchefu
  • Sehemu ya ngozi ambayo mionzi imepita kuwa kavu,nyeusi au nyekundu na kuwasha
  • Matatizo ya mkojo
  • Kupata maradhi kirahisi kwa kuwa inapunguza kinga mwilini
  • Upungufu wa damu mwilini (anaemia)
  • Tupu kuwa kavu kwa wanawake (vaginal dryness)
  • Kwa wanaume  - Uume au dhakari  kushindwa kusimama au kusimika (impotence)

Tiba ya dawa (Chemotherapy)

Tiba hii inaweza kutumika pekee au pamoja na tiba ya upasuaji au ya mionzi au kutumika pamoja na tiba ya upasuaji na mionzi (kutumika dawa + upasuaji + mionzi). Pia inaweza kutumika kabla ua baada ya tiba nyengine. Dawa za saratani ya kibofu cha mkojo ni Methotrexate (M), Vinblastine (V), Doxorubicin (A) Cisplastin (C) au MVAC. Kwa wale wenya matatizo ya moyo hupewa CMV.

Dawa zinaweza kutumiwa kwa wale wenye saratani iliyosambaa mwilini au wale ambao wapo kwenye makundi kuanzia Stage 0 hadi Stage III baada ya upasuaji ili kupunguza uwezekano wa kujirudia na tiba hii hujulikana kama adjuvant chemotherapy.

Pia dawa hizi zinaweza kutolewa  kabla ya upasuaji ili kuongeza ufanisi wa upasuaji na kupunguza ukubwa wa uvimbe wa saratani na tiba aina hii hujulikana kama neoadjuvant chemotherapy.

Wagonjwa wa Stage 0 na Stage I wanaweza kupewa dawa kupitia mpira unaojulikana kama catheter na dawa hukaa kwa muda (masaa kadhaa) na hutolewa baadae kwa njia ya kukojoa, hii hufanyika mara moja kwa wiki na huendelea kwa muda wa wiki kadhaa.

Madhara ya tiba hii ni pamoja na

  • Kuchoka
  • Kichefuchefu
  • Kutapika
  • Nywele kunyofoka
  • Kupungikiwa na damu mwilini
  • Kupungua hamu ya kula

Madhara hutofautiana kati ya mgonjwa mmoja na mwengine.

Kibofu cha mkojo kwenye maumbile ya mwanamume
Tiba ya Upasuaji

Kuna aina tatu za upasuaji;

  • Transurethral resection with fuguration – Aina hii inahusisha kuondoa uvimbe wa saratani kutoka kwenye kibofu cha mkojo na hutumiwa kwa wagonjwa wa Stage 0 na Stage I na baada ya upasuaji hupewa dawa za saratani.
  • Radical cystectomy – Inahusisha uondoaji wa kibofu chote cha mkojo, tezi pamoja na viungo vengine vya mwili kwa wale ambao saratani imeenea hadi kwenye nyama za kibofu cha mkojo au saratani ambayo haijaingia ndani lakini haipungui au kuleta matokeo mazuri kwa kutumia tiba nyengine.
  1. Kwa wanaume upasuaji huu pia unahusisha kuondoa tezi dume pamoja na mishipa inayopitisha shahawa kutoka kwenye tezi dume kwenda kwenye dhakari au uume (seminal vesicles) na huathiri  ufanyaji mapenzi.
  2. Kwa wanawake, mfuko wa uzazi (uterus), mayai (ovaries), na sehemu ya tupu (part of vagina) pia huondolewa  na hivyo mwanamke kutoweza kupata hedhi   pamoja na kutoshika mimba maishani mwake. Pia huathiri ufanyaji mapenzi na mambo ya mkojo.

Baada ya kuondoa kibofu cha mkojo, mgonjwa anaweza kuwekea mfuko wa kuhifadhia mkojo ambao unakuwa nje ya mwili na atahitaji kuubadilisha mara kwa mara na kuutunza kuwa msafi na kuzuia maambukizi. Mgonjwa huyu atahitaji ushauri nasaha pamoja na kumuona daktari mara kwa mara ili aangalie sehemu iliyowekwa mpira na hali ya mgonjwa mwenyewe. Au sehemu nyengine  ya kuhifadhia mkojo hutengenezwa ndani ya mwili wa mgonjwa zinazojulikana kama ileal conduit na continent urinary reservoir.

  • Segmental or partial cystectomy – Sehemu ya kibofu cha mkojo huondolewa kwa upasuaji hasa kwa wagonjwa wenye saratani ambayo haina hatari kubwa ya kusambaa.

Tiba ya Immunotherapy au Biological therapy

Tiba hii ni ya maji ambayo yamechanganyika na chanjo aina ya BCG, ambayo mgonjwa hupewa kwa kutumia mpira aina ya  catheter  ambao unaingizwa kwenye mrija wa kutoa mkojo (urethra) na huchochea kuamsha kinga ya mwili (stimulate immune system)  ili itoe kemikali zinazosaidia kupambana na chembechembe au seli  za saratani.

Madhara ya tiba ya immunotherapy

  • Kichefuchefu
  • Homa
  • Kuhisi baridi (chills)

Madhara haya ni kwa muda mfupi tu.

Maendeleo ya mgonjwa baada ya kupata tiba

Asilimia 90 ya wagonjwa wenye saratani ambayo bado haijaingia ndani sana huishi zaidi ya miaka mitano baada ya tiba. Asilimia tano ya wale walio na saratani ambayo imesambaa mwilini huishi kwa muda wa miaka miwili baada ya kupata tiba. Saratani inayojirudia ni hatari zaidi na hutoa matokeo mabaya kwa wagonjwa kwani wengi hawaishi muda mrefu baada ya kupata tiba.

Madhara ya saratani ya kibofu cha mkojo

  • Upungufu wa damu mwilini
  • Kushindwa kuzuia mkojo na hivyo kujikojolea
  • Kupungua kwa tundu kwenye mrija wa kutolea mkojo (urethral stricture)
  • Kuvimba kwa ureters kutokana na mkojo kushindwa kwenda kwenye kibofu cha mkojo

Kinga ya saratani  ya kibofu cha mkojo

  • Acha kuvuta sigara
  • Kunywa maji kwa wingi anagalau lita 1 na nusu kwa siku ili kusaidia kuondoa kemikali zinazosababisha saratani mwilini.  ‘’Kumbuka kunywa maji mpaka wakati unapokojoa mkojo unatoka bila rangi yoyote’’.
  • Kwa wale wanaofanya kazi viwandani, saluni, nk,  hakikisha unajikinga kutokana na madhara ya kemikali zinazosababisha saratani.

 

Imesomwa mara 11095 Imehaririwa Jumanne, 07 Agosti 2018 16:53
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana