Image

Maambukizi ya Fangasi Sehemu ya Kwanza

Fangasi wapo kila mahali, kwenye miti, mimea, mchanga, ndani majumbani mwetu na hata kwenye ngozi ya binadamu.Aina nyingi ya fangasi hawasababishi madhara yoyote kwa binadamu isipokuwa wachache tu. Kuna aina milioni moja na nusu za wadudu aina ya fangasi wanaotambulika duniani, kati yao ni fangasi 300 tu wanaojulikana kusababisha maambukizi kwa binadamu .1,2 Uvutaji wa hewa iliyochanganyika na  mazalia ya fangasi yanayojulikana kama fungal spores pamoja na uwepo wa uvamizi au ukuaji wa fangasi kwenye ngozi ya binadamu husababisha maambukizi ya fangasi, hivyo basi maambukizi mengi ya fangasi huanza kwenye  mapafu au kwenye ngozi ya mtu.

Takribani watu milioni 984 walipata maambukizi ya fangasi kwenye ngozi  mwaka 2010 na hivyo kufanya maambukizi haya kuwa ugonjwa namba nne katika magonjwa yote kwa mwaka huo 3.

Watu walio kwenye hatari ya kupata maambukizi ya fangasi ni kama wafuatavyo;

  • Wagonjwa wanaotumia dawa za kuua vimelea vya wadudu bila kufuata masharti ya daktari -Dawa aina ya antibayotiki (antibiotics)
  • Wale wenye kinga dhaifu - Wagonjwa wa ukimwi,wagonjwa wa kisukari, wagonjwa wanaotumia dawa za jamii ya steroid, wagonjwa wanaotumia dawa za kutibu saratani (chemotherapy drugs), immunosuppressive drugs, wagonjwa wanaotibiwa kwa mionzi na  wajawazito
  • Watoto wadogo na wazee - Ingawa watu wote wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya fangasi, hatari kubwa ipo kwenye kundi hili la wazee na watoto kutokana kuwa na kinga dhaifu

Aina za maambukizi ya fangasi

  1. Maambukizi ya fangasi nje ya mwili (Superficial mycoses) - Ni fangasi ambao husababisha maambukizi kwenye ngozi, nywele, kucha na hawaishi kwenye tishu mwilini. Fangasi aina hii hujulikana kama Dermatophytes.Fangasi hawa hushambulia sehemu tajwa hapo juu kwa kutoa vimengenyo (Extracellular enzymes) vinavyolainisha protini aina ya keratin inayopatikana katika maeneo hayo.Maambukizi haya ya fangasi yamegawanyika katika
  2. Tinea Corporis - Maambukizi ya fangasi yanayopatikana katika sehemu yoyote ile mwilini.
  3. Tinea Pedis (Athlete’s foot)-Maambukizi ya fangasi katikati ya vidole vya miguuni na kwenye nyao za miguu
  4. Tinea Unguium (Onchomycosis) - Maambukizi haya yanapatikana kwenye kucha za vidole vya miguuni na vya mikononi
  5. Tinea Capitis – Huonekana kwenye kichwa hasa kwa watoto wadogo.Husababisha mapunye kwenye kichwa, nywele kunyofoka, mabaka meusi kwenye kichwa yaliyoambatana na mcharuko (Inflammation), kutokwa na magamba kichwani, kuwashwa na kuvimba vimba  kwenye kichwa
  6. Tinea Cruris – Maambukizi ya fangasi sehemu za siri
  7. Tinea Barbae – Huonekana maeneo yenye ndevu kwenye uso na shingoni
  8. Tinea Vesicolor – Maambukizi ya fangasi kwenye ngozi ya watu wazima.Maambukizi haya hayaonekani kwenye uso ila husababisha ngozi kuwa na mabaka yenye rangi ya kahawia iliyochanganyika na rangi nyekundu (reddish brown).Tinea vesicolor huonekana sana kwenye ngozi ya watu wanaoishi sehemu zenye joto kali au wenye matatizo kwenye vichocheo vya miili yao (hormonal abnormalities) ingawa wote wanaopata maambukizi haya huwa ni watu wenye afya njema.
  9. Subcutaneous Mycoses- Maambukizi ya fangasi kwenye tishu chini ya ngozi zinazojulikana kama dermis, subcutaneous tissue, fascia na kwenye misuli.Fangasi wanaosababisha maambukizi haya hupatikana kwenye mchanga na mimea.Maambukizi haya sugu hutokea pale mtu anapokuwa na kidonda na hivyo kurahisisha fangasi kuvamia mwili.Magonjwa yanayosababishwa na fangasi kwenye tishu chini ya ngozi ni kama yafuatayo;
  • Sporotrichosis
  • Chromoblastomycosus
  • Mycetoma
  • Phaeohypomycosis 

Sporotrichosis

Husababishwa na fangasi aina ya Sporothrix schenckii.Fangasi hawa hupatikana kwenye mimea, miti, nyasi na kwenye maua aina ya waridi. Maambukizi yanayotokea kwenye mikono na miguu ingawa kwa watoto huonekana sana sehemu za usoni.Pia huweza kusambaa kwenye damu kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini. 

Vipimo vya uchunguzi

  • Kipimo cha maabara kwa kutumia hadubini
  • Kipimo cha kuotesha fangasi hawa kwenye medium aina ya mold agar au sabouraud’s agar iliyochanganywa na dawa aina ya chloramphenicol kisha kuwekwa kwenye nyuzi joto kati ya 25-30֯֯C
  • Kipimo cha damu (Serology test)

Tiba ya Sporotrichosis

  • Mara nyingi maambukizi haya hupona yenyewe
  • Tiba ya dawa ya kunywa ya potassium iodide iliyochanganywa na maziwa
  • Dawa ya kutibu fangasi za vidonge

 

Chloroblastomycosis

Husababishwa na aina tano ya fangasi ambao ni;

  • Phialophora verrucosa
  • Fonsecaea pedrosoi
  • Rhinocladiella aquaspersa
  • Fonsecaea compacta
  • Cladophialophora carrionii

Fangasi hawa huvamia mchubuko au kidonda kilichopo kwenye miguu au nyao. Baada ya miezi au miaka kadhaa, mgonjwa hupata viuvimbe vilivyofanana na mboga ya cauliflower, vijipu venye mabaka meusi (black dots) venye kutoa usaha  ambavyo huonekana kwenye ngozi za miguu au kwenye nyao. Mara chache sana husababisha matende kwenye miguu kutokana na kuziba mishipa ya lymphatic (Lymphatic obstruction).

Vipimo vya uchunguzi

  • Sehemu iliyoathirika hukwanguliwa au kuchukuliwa kinyama na kupelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi (Biopsy)
  • Kuoteshwa kwa fangasi maabara (Culturing)
  • Uchunguzi maabara kwa kutumia hadubini

Tiba ya Chloroblastomycosis

  • Tiba ya upasuaji kwa kukatakata na kusafisha sehemu husika (surgical debridement)
  • Tiba ya dawa za saratani pamoja na dawa aina ya Flucytosine and Itraconazole

Phaeohypomycosis

Maambukizi haya husababishwa na fangasi aina ya;

  • Exophiala jeanselmei
  • Phialophora richardsiae
  • Bipolaris spicifera
  • Wangiella dermatitidis

Kielelezo cha maambukizi haya ni uwepo wa tishu zenye mabaka meusi (dark pigmented septate hyphae)

Vipimo vya uchunguzi

  • Kuoteshwa kwa fangasi hawa maabara (Culture) 

Tiba ya Phaeohypomycosis

Dawa za kutibu fangasi hutumika ingawa hazina matokeo mazuri kwa fangasi hawa kwani asilimia 80 ya watu wote wanaopata maambukizi haya hufariki 4.

Mycetoma

Maambukizi hatari ya fangasi kwenye ngozi, fascia na mifupa ya mikono na miguu.Husababishwa na fangasi jamii ya mycelial fungi kutoka kwenye divisheni ya Ascomycota.Fangasi aina hii hupatikana kwenye mchanga na huvamia mwili pindi mtu anapochomwa na mwiba, vipande vya miti (twigs) au hata sehemu ya mwili iliyokatika inapogusana na majani yenye fangasi hawa.Fangasi wanaosababisha mycetoma ni kama wafuatao;

  • Pseudallescheria boydii
  • Madurella mycetomatis
  • Madurella grisea
  • Exophiala jeanselmei
  • Acromonium falciforme

Dalili na viashiria vya mycetoma

  • Kutokea kwa viuvimbe kwenye sehemu zilizoathiriwa na hivyo maambukizi kuendelea kusambaa kwenye sehemu nyingine ya mwili
  • Kuwepo kwa matundu yanayotoa uchafu kwenye misuli (Draining sinuses)
  • Maambukizi kwenye mifupa ambayo huweza kusababisha kilema cha maisha

Vipimo vya uchunguzi

  • Kipimo cha maabara kwa kutumia hadubini (microscope)
  • Kuotesha fangasi maabara

Tiba ya Mycetoma

  • Tiba ya upasuaji ya sehemu husika (Surgical debridement)
  • Dawa za saratani
  • Dawa za kutibu fangasi

Marejeo

  1. National Center for Emerging and Zoonotic Infectious Diseases (NCEZID)
  2. Division of Foodborne, Waterborne, and Environmental Diseases (DFWED)
  3. Hay, Roderick J.; Johns, Nicole E.; Williams, Hywel C.; Bolliger, Ian W.; Dellavalle, Robert P.; Margolis, David J.; Marks, Robin; Naldi, Luigi; Weinstock, Martin A.; Wulf, Sarah K.; Michaud, Catherine; Murray, Christopher J.L.; Naghavi, Mohsen (Oct 28, 2013). "The Global Burden of Skin Disease in 2010: An Analysis of the Prevalence and Impact of Skin Conditions". The Journal of Investigative Dermatology134(6): 1527–34. doi:1038/jid.2013.446PMID 24166134.
  4. Sanjay G.R., J.E. Patterson, D.DA. Sutton, R.Pullen, and M.G. Rinaldi. 2002. Disseminated phaeohyphomycosis : review of an emerging Mycosis. Clinical Infectious Disease 34:467-476.
Imesomwa mara 12388 Imehaririwa Jumatatu, 23 Julai 2018 16:57
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.