Image

Ishi kwa kujiamini, kisukari sio mwisho wa Maisha

Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa tishio sana hasa kwa wale wanaougua ugonjwa huu kutokana kuwa na athari nyingi sana kama mgonjwa kupata kiharusi, kupoteza viungo mbalimbali  vya mwili kama vile kukatwa mguu/miguu, kidole/vidole na hata kupoteza uwezo wa kuona (diabetes retinopathy), na athari hizi hutokea endapo ugonjwa  wa kisukari haujadhibitwa vyema.

Ugonjwa huu wa kisukari unaweza usiwe ugonjwa  wa kutisha endapo tu mwenye kisukari ataweza kuishi kwa kujiamini na kujikubali, wataalam wanasema kuwa mtu kuishi na ugonjwa  huu wa kisukari anahitaji mambo makuu manne :-

Kujikubali

 Kujikubali ni jambo  muhimu sana, kutayarisha akili yako na kuikubali hali hiyo ya kuwa na  ugonjwa wa kisukari,na kuiambia akili yako kuwa ugonjwa huu hauponi ni hali ambayo itakuwepo katika umri wa maisha yako yote na kuwa tayari kubadili mfumo wako mzima wa maisha.Hii ni sawa na mtu aliyezaliwa upya.

Kubadili mfumo wa Ulaji

Ukijikubali kuwa una  ugonjwa wa kisukari ni rahisi sana kubadili mfumo wako mzima wa ulaji, hii inamaanisha kuwa mfumo wako wa ulaji unaweza kusababisha kupanda kwa sukari (glucose level) au kushuka kwa sukari. Ulaji wa vyakula vya wanga kwa wingi husababisha sukari kupanda. Kuacha kabisa ulaji na matumizi ya vitu ama vyakula vyenye sukari, kwa mfano soda, keki, barafu za sukari (ice cream), chokoleti n.k.

Pia kupunguza matumizi ya mafuta wakati wa uandaaji  wa chakula na kuacha matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi kwa mafano ulaji wa viazi vya kukaanga (chips), maandazi, vitumbua, n.k. Ulaji wa mboga za majani/salad/kachumbari kwa wingi ni muhimu sana. Sahani ya chakula itawaliwe na mboga za majani,na hii ni kwa kila mlo yaani chakula cha asubuhi,mchana na cha jioni.

Mazoezi ya Viungo

Mazoezi ni muhimu kwa afya, mazoezi huchangamsha mwili,hupunguza mapigo wa moyo na kuyafanya kuwa ya wastani pamoja na kuongeza mzunguko wa damu kwa mtu wenye ugonjwa kisukari (hivyo hupunguza hatari ya kupoteza kiungo cha mwili kwa mgonjwa wa kisukari kutokana kuwa na mzunguko mzuri wa damu kwenye viungo vyake), mazoezi yana nafasi kubwa sana kwa sababu husaidia kuyeyusha lehemu (cholesterol)  mwilini na kuondosha hatari ya kupata tatizo la kiharusi (stroke). Mazoezi yanayohitajika hapa ni yale ya kuchoma mafuta na sio ya kupanua misuli, mazoezi hayo ni kama kukimbia, kuruka kamba,kuogelea,kutembea kwa mwendo kasi. Mazoezi haya yafanyike kwa muda wa nusu saa au saa moja kila siku asubuhi au jioni.

Matumizi ya dawa/Insulin

Wagonjwa wa kisukari hutumia dawa za vidonge za kudhibiti ugonjwa huu  au dawa za sindano aina ya insulin. Ni muhimu kutumia dawa kama daktari alivyoshauri, usiache matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari ili kudhibiti ugonjwa wa kisukari.

Endapo utajiamini na kijitambua basi nakuhakikishia ya kwamba ugonjwa wa  kisukari hautakusumbua.

Ishi kwa kujiamini, kisukari sio mwisho wa maisha!!!

Imesomwa mara 7261 Imehaririwa Alhamisi, 04 Mai 2017 20:05
Lucy Johnbosco

Diabetes Consciousness for Community is focusing on raising Diabetes awareness and healthy lifestyle

https://dicoco.or.tz | Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana