Image

Tekinolojia, ni ufanisi au chanzo cha ugoigoi kwenye afya?

 Nikiwa kama mjukuu kipenzi wa bibi yangu, huwa napenda sana kutumia muda wangu wa mapumziko kujadiliana naye mambo mbalimbali yanayohusu jamii, iwe yaliyokuwa yanatokea hapo awali au yanayoendelea kutokea. Ilikuwa ni siku ya jumapili baada ya kutoka kwenye mihangaiko, niliingia ndani na kumuita bibi kwa jina lake la utani ‘Nyaksi’ ili twende nje tukapunge upepo na mazungumzo ya hapa na pale.

Nikipata Ushauri wa Afya toka kwa Dk Mayala

   Kama ilivyo ada yangu, huwa napenda sana kutafiti mambo mbalimbali, nikamuuliza bibi, eti bibi nimewahi kusikia kuwa wakati wa enzi zenu mlikuwa hamruhusiwi kula mayai wakati wa ujauzito kwa kuwa mtoto atazaliwa bila nywele? Bibi Nyaksi huku akitabasamu akanigeukia na kusema, "umeshaanza, kwanza usikumbushe enzi zile bado nipo mbichi" akimaanisha wakati yupo msichana. Wote tukatabasamu kwa pamoja. Nyaksi akaendelea kusema sio mayai tu, bali vyakula vyote nyenye virutubisho kwa wingi ambavyo ninyi vijana wa leo mnaviita ‘purotini’, akiitamka protini kwa lafudhi ya kizee. Nyaksi alisema tulizuiliwa kula vyakula hivyo kwa mlengo wa mwiko, akaendela kusema, unajua Babu (jina langu alilopenda sana kuniita Nyaksi) wazee walitumia mwiko ili kututisha lakini ukweli ni kuwa wakati ule hakukuwa na tekenolojia (akimaanisha teknolojia) hivyo kama utakula vyakula vyenye virutubisho sana vitamfanya mtoto awe mkubwa, na hivyo kama utashindwa kujifungua kwa njia ya kawaida basi hakutakuwa na njia nyingine ya kukusaidia. Nyaksi akaendelea ninyi vijana wa siku hizi mna raha, hospitali nyingi, madaktari wengi huku mna njia nyingi mbadala ikiwemo ya upasuaji na nyinginezo. 

   Nilimuacha Bibi Nyaksi amalizie maneno yake, halafu nikamuuliza, kama sisi tuna teknolojia na njia nyingi za kisasa, sasa inakuwaje urefu wa maisha wa vizazi vyetu unazidi kupungua kadri teknolojia inavyozidi kukua? Nyaksi alicheka sana, huku akipigapiga makofi ili kuvuta hisia alisema " hakuna kizuri kisicho na kasoro". Baada ya hapo tukaacha kuongelea masuala ya afya na kuketi chini ili kupunga upepo uliokuwa ukivuma kwa kasi kutokea Kinyanyiko. 

   Kipindi chote naburudika na upepo uliokuwa unavuma ukitokea kwenye mabonde ya Kinyanyiko nilikuwa natafakari mambo mengi kuhusu maneno ya Nyaksi. Misemo yake ilikuwa inazungukazunguka kichwani kwangu , huku maneno "Hakuna kizuri kisicho na kasoro " na " ninyi mnaishi kwenye ulimwengu wenye tekinolojia" vikijitokeza mara kwa mara. Lakini je, hizi teknolojia zinatunufaisha vipi? Zipi faida na hasara zake? Hivyo nikawa nachorachora chini nikiainisha viambatanishi vyote vya hii tunayoiita teknolojia, nikarudi haraka nyumbani na kuchukua iPad yangu kuanza kuandika makala hii ambapo tutaiangalia teknolojia kwa mapana na jinsi gani teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi katika medani ya afya. 

Teknolojia ni nini?

   Teknolojia ni utengenezaji,matumizi,maarifaya vifaa,machine,mitambo,uashi ili kutatua tatizo au ketenda kazi husika, iwe ni kwenye matibabu au kwenye michezo. Katika makala yetu ya leo tutaangalia sana hii teknolojia ya mawasiliano ya mtandao yaani ICT. Kwa wale maveterani kama mimi mtakumbuka teknolojia hii ilianza kuibukia kwa kasi sana nyumbani katika miaka ya tisini, katika wakati huo teknolojia hii siyo tu ilionekana kuwa ni kitu cha anasa bali pia ni kwa wenye nazo tu. Teknolojia hii ilihusishwa na viashiria chungu mzima kama kwenda na wakati, usomi, umjini n.k. kitu ambacho kimetufikisha hapa tulipo. 

 

Mtazamo wa jamii juu ya teknolojia

   Kama nilivyoelezea hapo juu, asili na historia juu ya ujio wa teknolojia hii ya mawasiliano ya mtandao inachangia sana katika ujengekaji wake, kwa mfano hapa kwetu wengi bado wana mtazamo hasi kuwa teknolojia hii ni kwa ajili ya wasomi au wenye uwezo, ingawa dhana hii inaendelea kubadirika siku hadi siku, lakini tatizo bado lipo. Nani wa kulaumiwa? Ni wanajamii au sisi wana mawasiliano? Jibu ni fupi. Hakuna wa kulaumiwa bali hatuna budi kutafakari juu ya namna ya kuliboresha na kulihalisisha kwa jamii yetu. 

Muundo wa teknolojia kwenye karne ya 21

   Katika makala yake ya sababu za watoto wachanga kulia, Dk Paul Mwanyika amefafanua kwa undani hatua ambazo mtoto hupitia katika ukuaji, kwa muktadha huohuo nami naufananisha ukuaji wa teknolojia na ule wa mtoto. Kwa ufupi, teknolojia imepitia hatua nyingi. Kwa mfano hapo zamani teknolojia ilikuwa ni kwa ajili ya kurahisisha kazi au utendaji, lakini leo hii teknolojia imegeuzwa kuwa sehemu ya kazi na siyo tena kitendea au kirahisisha kazi. 

   Si kitu cha kushangaza kusikia mtu anauza madawa mtandaoni (online) bila kuwa na duka nje ya mtandao (brick shop). Aidha leo hii madaktari wanaweza kupata muongozo au kushiriki kwenye upasuaji bila kizuizi cha umbali. Huu ndiyo muundo wa teknolojia ya sasa, tunatumia teknolojia kama huduma/kazi (Technology As A Service) na siyo tu kitendea kazi. 

Faida/Matumizi za teknolojia kwenye Afya

   Lengo la makala hii ni kuwaamsha (kumbusha) wanajamii umuhimu au njia mahususi za kutumia teknolojia katika kujenga afya bora. Msukumo wa makala hii umekuja kutokana na matokea ya utafiti

niliyofanya kwenye tovuti ya TanzMED.com. Ndani ya tovuti hii kuna sehemu ambayo mtumiaji anaweza kujisajiri akawa anapokea taarifa mbalimbali kuhusiana na afya (milisho ya afya). Nilichogundua ni kuwa uwiano wa wanaojisajili kwa wanaotembelea ni chini ya 1%. Baada ya kuwauliza watembeleaji wengi kwanini hawajisajili, karibu 20% walisema hawafahamu jinsi ya kutumia njia hiyo, wengine 20% hawajui uwepo wa programu hii na waliobaki ni kutotambua umuhimu wa kufanya hivyo. Hii ni sehemu ndogo tu ambayo matumizi ya teknolojia yanaweza kukurahisishia kujenga afya bora. 

Hivyo tuangalie kwa kila kundi ni jinsi gani linaweza kunufaika na teknolojia. 

 

Munonekano wa Application ya TanzMED


Madaktari
 

   Wakiwa ndio watendaji wakuu, ni dhahiri kuwa madaktari ni moja ya watu wenye heshima kubwa sana kwenye jamii yetu. Wengi tumekuwa tukiwaamini na kuwakubali madaktari kwa kiwango kikubwa zaidi. Leo hii kuna mitandao jamii kama Facebook, Twitter na hata TanzMED.co.tz, kwa kutumia mtandao jamii daktari anaweza kuwasiliana na wanajamii akawapa mustakabali wa masuala ya afya, kwa mfano nimewahi kuona vipachiko kadhaa vya Dk Fabian Mghanga kwenye Facebook, akiwa anapachika mambo yaliyo motomoto kwenye jamii yetu kwa sasa, wanajumuiya wote wanaomfuata huweza kuona vipachiko vyake na kubadilishana naye mawazo au kutolea maoni.

Si hayo tu daktari pia anaweza kutumia programu za mawasiliano kubadilishana mawazo (kuchat) na wagonjwa walioruhusiwa ili kufuatilia hali zao na kuwafariji. Vilevile daktari anaweza kutumia simu kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa wagonjwa walio hospitali akiwakumbusha kunywa dawa na kufanya mazoezi ya asubuhi au jioni. Wagonjwa watafarijika sana endapo wanapokea ujumbe toka kwa daktari unaomsisitizia jambo fulani. Hivyo muda umefika sasa kwa madaktari wetu kubadirika na kuanza kutumia fursa hizi ambazo zinawezekana na kupatikana kwenye mazingira yetu ya Tanzania. 

 Chukulia mfano, kwanini mahospitali yasichukue namba za simu za wagonjwa wote na kuzipanga kulingana na aina ya magonjwa yao halafu wakawa wanawatumia ujumbe au taarifa mbalimbali zinazohusu maendeleo au tahadhari muhimu juu ya magonjwa yao? 

Vyombo vya habari

   Hii ni moja ya sehemu ambazo zina ushawishi na upenzi mkubwa mno kwenye jamii. Katika baadhi ya nchi zilizoendelea, unaweza kukuta uwepo wa televisheni au redio zinazohusu masuala ya afya pekee. Kwa nchi kama Tanzania wamiliki wa hizi televisheni, magazeti au redio wanaweza kutumia vituo vyao kufikisha maarifa, ufahamu na hata ujumbe juu ya afya. Kwa kushirikiana na watu maarufu na wasanii dhana hii inaweza kukubalika na kufika mbali zaidi. 

Makampuni ya teknolojia

   Makampuni yanayojihusisha na mawasiliano ya mtandao, kuanzia makampuni ya simu, watengeneza programu nk, yanatakiwa kushirikiana na wadau wa medani ya afya katika kuhakikisha wanainufaisha jamii. Kwa mfano kampuni ya Dudumizi Solutions imejiunga na kundi la madaktari na kuanzisha mtandao wa Afya ujulikanao kama www.tanzmed.co.tz. Hii ni chachu na changamoto kwa wadau kuonesha kuwa sasa teknolojia ni sehemu ya jamii hivyo tunatakiwa kujihusisha zaidi, tubadilishe utendaji au mfumo wa teknolojia.

Kwa mfano makampuni ya simu yanaweza kuja na programu ambazo zitawawezesha wanajamii kutuma namba fulani halafu wakapata elimu au taarifa fupi za masuala ya afya (kama ile inayofanya kwa mama wajawazito). Aidha wataalamu wa programu wanaweza kuja na programu inayoweza kutumika kwenye simu kumuwezesha mtu kukokotoa afya yake (BMI Calculator), kujua siku ya kujifungua nk, hii ni mifano michache ambayo wadau wa ICT wanaweza kuitumia kujenga jamii yenye afya njema. Nimeongelea kwa ufinyu wake kutokana na hali halisi ya maendeleo ya ICT kwa nchi yetu ingawa tunaweza kwenda mbali zaidi ya hapo. 

Wanajamii

   Wakiwa ndio walengwa namba moja, wanajamii wanatakiwa kuanza kutumia teknolojia kama sehemu ya kujenga afya yao. Kwa mfano unaweza jiunga kwenye milisho (Subscription) ya tovuti mbalimbali za afya ambapo utakuwa unapokea taarifa mbalimbali za afya kama; mabadiriko ya hali ya hewa, magonjwa ya milipuko, kinga na mengineyo. Mara nyingi makala hizi huwa zinachujwa kuhakikisha unatumia taarifa inayojieleza. Hivyo jijengee mazoea ya kutumia teknolojia kwa ajili ya afya yako, iwe kuuliza maswali juu ya afya au kusoma dalili na kinga za magonjwa mbalimbali. Mtandao wa www.tanzmed.co.tz una yote haya kwa ajili ya afya yako. 

   Nilipomaliza kuainisha baadhi ya faida za teknolojia, kuna maneno ya Bibi Nyaksi yakawa yaniumiza," Hakuna kizuri kisicho na kasoro". Hivyo tuangalie athari za hii teknolojia. 

Kuvunja maadili na mipaka ya teknolojia

   Kutokana na ujio wake, wengi wamekuwa wakitumia teknolojia bila mipaka. Maadili ya teknolojia yamepigwa kumbo. Kwa mwandishi wa TanzMED Dk Fabian Mghanga ameeleza jinsi gani dawa za kuongeza makalio zinavyoshabikiwa, huku zikiwa hazina maelezo ya kuridhisha juu ya matumizi na namna zinavyofanya kazi. Ushabiki huu pia huchochewa sana na matumizi ya mitandao jamii kama vile Facebook, ambapo baadhi ya watu hutuma matangazo au picha zenye mvuto na kuwafanya akina dada wengi wahamasike kwa kutaka kuwa na mvuto kama waliouona kwenye picha.

Si hayo tu, tumeona pia jinsi mwandishi Dk Henry Mayala alivyotuelezea jinsi vumbi la viwandani linavyoweza kukusababishia pumu au magonjwa ya mfumo wa hewa, haya yote ni kwa sababu ya kuvukwa kwa mipaka ya maadili ya teknolojia kwa watoa huduma. Uvukaji wa mipaka siyo tu kwa watengenezaji (watoa huduma) za teknolojia bali pia kwa wanajamii. Kwa mfano katika makala yake ya kupungua kwa hamu ya kufanya mapenzi Dk Khamisi Bakari amesema sababu mojawapo ni matumizi ya intaneti kwa muda mrefu, hii ni inatuonesha mifano dhahiri ya athari zinazosababishwa na utokaji nje ya maadili ya teknolojia kwa mtumiaji. Hivyo maadili ya teknolojia ni lazima yaheshimiwe.

 

Maadili na mipaka ya kazi

   Nakumbuka kuna wimbo mmoja wa wanamuziki wa kizazi kipya wanaoitwa Wagosi wa Kaya uitwao wauguzi kuna kipande cha mstari kinasema; "...nesi anaongea kwa simu na bwana wa kizigua". Hii ni moja ya athari za teknolojia. Kuna wakati unatamani hata upigane, maana unaenda hospitalini huku kuna foleni kubwa inasubiri kumuona daktari, lakini yeye yupo bize kwenye simu akicheka kuhusu matokeo ya mpira wa jana. Hapo sizungumzii muda wanaotumia kuangalia picha na maoni kwenye Facebook au kuchat kwenye Yahoo na rafiki yake aliye Wuhan. Idara husika lazima iweke mipaka na maadili ya kazi yatakayomuongoza muhusika katika matumizi ya teknolojia. Tukumbuke kuwa teknolojia sasa imekuwa ni kazi na maisha hivyo haiepukiki. 

   Wakati namalizia haya maneno ya mwisho chaji nayo ikawa imeisha kwenye iPad yangu, ni bahati mbaya kwamba jana sikuichaji kutokana kukatika kwa umeme. Sasa basi inanibidi kusubiri umeme urudi ili niweze kuichaji na kumalizia makala hii ambayo nitaituma kwenye jarida lijalo, makala ambayo itazungumzia mambo ambayo ningependa kuishauri jamii/serikali ifanye ili kujenga na kudumisha afya bora kwenye karne hii ya teknolojia.

Imesomwa mara 7197 Imehaririwa Alhamisi, 08 Novemba 2018 16:56
Mkata Nyoni

Mkata Nyoni ni mtaalamu wa masuala ya Uchumi na Biashara ya Teknohama. (Information Economics & IT Management). Ni muanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya Dudumizi Technologies LTD inayojishughulisha na masuala yautengenezaji wa Website, Web Systems na Applications za simu.

https://www.dudumizi.com | Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.