Image

Unywaji wa Chai ya kijani (Green tea) waweza Kupunguza Ongezeko la VVU

Katika hali inayoweza kutafsiriwa kuwa ni hatua nzuri katika vita dhidi ya VVU, tafiti zilizofanywa na watafiti huko Marekani na Uingereza zimeonesha kuwa unywaji wa chai ya kijani (green tea) waweza kuwa na manufaa makubwa katika kuzuia maambukizi dhidi ya VVU.

Matokeo ya awali ya tafiti hizo ambayo yamechapishwa katika jarida la tafiti lijulikanalo kama Journal of Allergy and Clinical Immunology yameonesha kuwa chai ya kijani ina kiasili ambacho kina uwezo wa kuzuia VVU kuzaliana kwa wingi ndani ya damu ya muathirika.

Utafiti wa awali uliofanywa katika maabara umeonesha kuwa kiasili hicho kijulikanacho kitaalamu kama Epigallocatechin gallate (EGCG) kina uwezo wa kunata katika chembe chembe nyeupe za damu zijulikanazo kama CD4 ambazo kwa kawaida hutumiwa na VVU kuzaliana na hivyo kuzuia uwezekano wa VVU kuingia ndani ya chembe chembe hizo na hivyo kupunguza kasi yao ya kuzaliana.

Mmojawapo wa watafiti hao, Profesa Mike Williamson wa Chuo Kikuu cha Sheffield cha nchini Uingereza alisema katika mahojiano kuwa, utafiti wao umeonesha kuwa unywaji wa chai ya kijani unaweza kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya VVU na pia kupunguza uwezekano wa VVU kuzaliana na kuongezeka katika damu ya muathirika.

Hata hivyo watafiti hao wameonya kuwa ni mapema mno kwa jamii kuanza kuyatumia matokeo ya utafiti huo na kwamba tafiti zaidi hususani zinazohusisha binadamu au wanyama zinapaswa kufanywa ili kuyapa matokeo ya utafiti huo uzito unaostahili.

Waliongeza kuwa imeonekana mara nyingi viasili vinavyoweza kuonesha matokeo mazuri katika maabara, vinaweza visilete matokeo yanayokusudiwa kama utafiti huohuo utafanywa kwa binadamu ama wanyama.

Hawakusita kuonesha kuwa matokeo ya utafiti wao yasichukuliwe kuwa chai ya kijani ni tiba au njia ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU badala yake inaweza kutumika kama njia nyongeza ya kusaidia dawa za kupambana na VVU na hivyo kupunguza kasi ya kuzaliana kwa VVU.

Imesomwa mara 7052 Imehaririwa Jumapili, 08 Agosti 2021 22:21
Dr Fabian P. Mghanga

Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.