Image

Viungo vya Nguruwe Kupandikizwa kwa Binadamu

Watafiti nchini China wana matarajio makubwa kwamba nguruwe wanaozalishwa kijenetikia (Genetic modified cloned piglets) wanaweza kuwa suluhisho la matatizo ya viungo ambavyo vitaweza kupandikizwa kwa binadamu wenye kuhitaji viungo kutokana na viungo vyao kushindwa kufanya kazi baada ya kuathiriwa na magonjwa yasiyotibika.

Mkuu wa kitengo cha utafiti cha Metabolic disease research centre cha  Nanjing University Nchini China bwana Zhao Zijian amesema “Nguruwe hawa wa kijenetikia wanaleta matumaini mapya kwa wagonjwa wanaohitaji viungo ambao wamekosa mtu wa kuwapa”.

Kundi la watafiti hao limekuwa likifanya utafiti kuhusu teknolojia ya GM tokea mwaka 1998 wakiwa na matarajio ya kubadilisha viashiria vya asili (genes) kwa nguruwe vinavyosababisha binadamu kukataa viungo kutoka kwa nguruwe.

‘’ Kama vile binadamu walivyo na makundi tofauti ya damu ambapo mtu  hawezi kupewa damu kutoka kwa mtu mwengine mwenye kundi tofauti ambalo haliendani na damu yake, basi viungo vya nguruwe vilikataliwa na binadamu kabla sijabadilisha chembechembe za sukari na kiasilia cha asili tofauti” alisema bwana Dai Yifan, naibu mkurugenzi katika kitengo hicho cha utafiti.

Bwana Dai ambaye alifanikiwa kuzalisha nguruwe hawa wa kijenetikia kwenye maabara ya Revivicor Inc nchini Marekani na kuchukua chembechembe au seli za hawa nguruwe na kurudi nazo nchini China mwaka jana ambapo anatarajia kuzalisha maelfu ya nguruwe wa aina hiyo nchini humo.

Kundi la kwanza la nguruwe hawa litazaliwa ndani ya miezi mitano au sita katika jiji la Nanjing lililopo katika mkoa wa Jiangsu. Kundi hilo litafanyiwa utafiti zaidi ili kuweza kujua kama kweli  kuna uwezekano wa kutumia viungo vyake kama moyo, figo, ini kwa binadamu bila madhara yoyote.

“Kwa muda huu, wanasanyansi  wanatengeneza sehemu maalum ya kufanyia upasuaji nguruwe hawa ambayo  itakuwa huru kutokana na virusi  ili nguruwe hawa wasipate maradhi ambayo yanaweza kumuambukiza binadamu” alisema bwana Dai.

Wakati huo huo, madaktari wa upasuaji wameonyesha wasiwasi kutokana na utafiti huo kwa sababu,  “Wanasayansi wanaufahamu mdogo kuhusu virusi vya nguruwe hivyo inaweza kuleta janga kubwa kama viungo vya nguruwe vitapandikizwa kwa binadamu” alisema Dr Li Shichun, bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya ini kutoka hospitali ya Beijing YuAn Hospital.

Viungo kutoka kwa nguruwe vimekuwa vikifanyiwa utafiti toka mwaka 2002 nchini Marekani  ambapo vimeweza kurefusha maisha ya ngedere/tumbili kwa muda wa siku 400. Hii inaweza kuwa njia mojawapo ya kurefusha muda wa mgonjwa wakati anasubiri kupatikana kwa mtu ambaye ana viungo sahihi ambavyo vitaweza kupandikizwa kwake.

Wanasayansi kutoka kitengo cha Chinese Academy of Agricultural sciences kwa mara ya kwanza walizalisha nguruwe hawa wa kijenetikia (GM pigs) mwezi wa Novemba 2010.  Utafiti kwa binadamu haujafanyika sehemu yoyote duniani.

“Kutokana na uhaba wa viungo,  ni watu 10,000  tu kati ya milioni moja wenye maradhi ya figo na watu 300,000 wenye maradhi ya ini wanaosubiri viungo ndio wanaobahatika kupata viungo na hivyo kuokoa maisha yao kila mwaka nchini china”, alisema naibu waziri wa afya wa China, mheshimiwa Huang Jiefu.

“Watafiti  wa Nanjing University wanatarajia kuomba kibali cha kufanya utafiti wao kwa binadamu wakati nguruwe hao watakapokuwa wakubwa”, alisema bwana Dai.

Wanasayansi wamesema hawajui kama serikali ya China itatoa kibali cha kuruhusu utafiti wa upandikizwaji wa viungo vya nguruwe kwa binadamu.

Ni matarajio yetu ya kwamba utafiti huu utaleta mageuzi makubwa katika tiba hasa ya magonjwa sugu kwani itakuwa rahisi kupata viungo lakini kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa kina  kuhusu virusi vya nguruwe na pia kujiridhisha na matokeo ya utafiti wenyewe kwa binadamu. Hii ni changamoto pia kwa wanasayansi wa Tanzania kufanya utafiti katika nyanja hizi.

Imesomwa mara 4969 Imehaririwa Jumatano, 13 Machi 2019 16:19
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.