Image
×

Onyo

JUser: :_load: Haiwezi kupakia mtumiaji aliye na kitambulisho: 797

Maambukizi ya Tezi Dume (Prostatitis) Sehemu ya Kwanza

Prostatitis ni ugonjwa unaosababishwa na maambukizi  ya vimelea vya bakteria katika tezi dume (prostate) kwa wanaume.

Kuna aina kuu nne za ugonjwa huu wa prostatitis

1. Maambukizi ya ghafla ya tezi dume (Acute bacterial prostatitis)

2. Maambukizi sugu ya tezi dume (Chronic bacterial prostatitis)

3. Chronic prostatitis without infection/Chronic pelvic pain syndrome/chronic non bacterial prostatitis

4. Asymptomatic inflammatory prostatitis 

Tuangalie aina moja baada ya nyingine za ugonjwa huu 

Maambukizi ya ghafla ya tezi dume (Acute bacterial prostatitis)

Ni maambukizi ya tezi dume yanayosababishwa na vimelea vya bakteria aina ya E.coli, Klebsiella, Proteus, Pseudomonas, Enterobacter, Staphylococcus aureus, Enterococcus, Serratia na vimelea vinavyosababisha magonjwa ya zinaa. Maambukizi haya yanaweza kufika katika tezi dume moja kwa moja kupitia kwenye damu, au kutoka kwenye kiungo kilicho na maambukizi karibu na tezi dume au huweza kufika kwenye tezi dume kutokana na athari za kufanyiwa kipimo cha kuchukua nyama ya tezi dume kuipeleka  maabara kwa uangalizi zaidi au kwa lugha ya kitaalamu tunaita prostate biopsy. 

Dalili na viashiria vya maambukizi ya ghafla ya tezi dume

     - Homa

     - Kuhisi baridi

     - Kutetemeka kutokana na baridi

     - Maumivu chini ya mgongo 

     - Maumivu katika maeneo ya sehemu za siri

     - Kupata haja ndogo /kukojoa mara kwa mara

     - Kupata haja ndogo wakati wa usiku inayomfanya mtu kushindwa kuivumilia na hivyo kukimbia chooni

     - Maumivu/kichomi wakati wa kukojoa/haja ndogo

     - Maumivu ya mwili mzima

 Vipimo vya uchunguzi

- Complete blood count – Kipimo cha damu  kinachoonesha kuongezeka kwa kiwango cha chembechembe nyeupe za damu

- Kipimo cha damu ili kuangalia vimelea vya bakteria kwenye damu (blood cultures). Vimelea vya E-coli vina uwezo  wa kupenya kwenye tishu za tezi dume, hivyo dawa za kudhibiti E-coli  zinahitaji kutumiwa kama E-coli ndio watagunduliwa

- Urine for microscope- Kipimo cha kuangalia chembechembe nyeupe za damu na bakteria kwenye mkojo

- Kipimo cha damu kuangalia  kiwango  cha Prostate Specific Antigen (PSA). Mara nyingi  kiwango cha PSA  huongezeka lakini ni kwa muda tu.

- Kipimo cha prostate biopsy mara nyingi hakifanywi kutokana na dalili na viashiria vya maambukizi haya kuonyesha kuwa ni maambukizi ghafla ya tezi dume, lakini wakati wa kipimo hiki, chembechembe nyeupe aina ya neutrophils huonekana kwenye tezi dume.

- DRE- Kuchunguza Tezi Dume kupitia njia ya haja kubwa au Digital Rectal Examination (DRE): Hiki ni kipimo cha kwanza kabisa ambacho mgonjwa hufanyiwa na daktari wake. Ni kipimo kinachoweza kumpa daktari picha ya tatizo na kufahamu kuhusu ukubwa na hali ya tezi dume. Daktari akiwa amevaa glovu huingiza kidole chake cha shahada katika njia ya haja kubwa au puru (rectum) ya mgonjwa kisha kuzungusha zungusha ili kufahamu kama tezi limevimba ama la na pia hali yake kama ni ngumu kuliko kawaida ama lina utando na nyama laini. Katika maambukizi haya ya prostatitis,tezi dume huwa limevimba, lenye maumivu linapoguswa, lililokakamaa (firm), lenye jotojoto (warm) na kinga ambazo hazieleweki.

- Kipimo cha damu kuangalia aina ya protini inayojulikana kama C-Reactive protein ambayo huwa huongezeka kiwango chake pale panakuwa na maambukizi.

- Vipimo vya X-ray, Ultrasound na CT Scan vinaweza kutumika kulingana na hali ya mgonjwa itakavyokuwa au kama daktari anahisi  chanzo cha maambukizi katika tezi dume kinatokana na maambukizi katika viungo vilivyokaribu na tezi dume au kuangalia viungo vilivyokaribu na tezi dume kama viko katika hali yake ya kawaida au la. 

Matibabu

Matibabu ya aina hii ya prostatitis yanahusisha matumizi ya dawa aina za antibiotiki ambazo huponya maambukizi haya kwa haraka sana. Aina nyingine za dawa hizi huwa haziwezi kupenya hadi ndani ya tezi dume (mfano ciprofloxacilin) hivyo kufanya matibabu kuwa ya shida sana. Dawa za antiobiotiki zinazoweza kupenya kwa urahisi katika tezi dume ni dawa jamii ya co-trimoxazole, tetracyclins nk. 

Wagonjwa ambao wana upungufu wa kinga mwilini au wale wenye magonjwa sugu watahitaji kulazwa hospitali  ili wawe chini ya uangalizi wa karibu wa daktari. 

Dawa za maumivu na za kulainisha choo pia hutolewa kwa mgonjwa mwenye maumivu au ambaye anapata choo kigumu. 

Mgonjwa ambaye amepata madhara ya maambukizi haya ya ghafla katika tezi dume kama kutoweza kupata haja ndogo/mkojo, atahitaji kuwekewa mpira wa kupitisha mkojo sehemu ya chini ya kitovu  ili kumpunguzia maumivu  na kurahisisha  mkojo kutoka nje. 

Mgonjwa ambaye amepata matibabu ya antiobiotiki na hali yake haibadiliki kuwa nzuri atahitaji kufanyiwa kipimo cha Trans-urethral ultrasound ili kuangalia kama ana jipu ndani au la.

Male anatomy

 

Kinga ya maambukizi haya ni:

- Kuongeza hali ya usafi katika maeneo yako ya siri

- Hakikisha choo (toilet) chako ni kisafi hasa wale wanotumia vyoo vya kukaa

- Kutumia dawa za antiobiotiki kulingana na maelekezo ya daktari kwani dawa nyingine hupunguza kinga yako ya mwili kwa muda na hivyo kusababisha kupata maambukizi ya bakteria.

- Kama chanzo ni ugonjwa wa zinaa, ni vizuri kumueleza mwenza wako ukweli na kwenda hospitali ili kupata ushauri nasaha pamoja na tiba. 

Maambukizi sugu ya tezi dume (Chronic bacterial prostatitis)

Aina hii ya prostatitis huonekana chini ya silimia 5 ya wagonjwa wote wa  maambukizi ya tezi dume ambayo hayasababishwi na tatizo la uvimbe katika tezi dume. Maambukizi sugu ya tezi dume  ni nadra sana kutokea na husababishwa na  bakteria aina ya E-coli. Maambukizi haya hayana dalili wala viashiria vyovyote isipokuwa tu pale ambapo kutakuwa na kuenea kwa maambukizi kwenye kibofu cha mkojo. 

Vipimo vya uchunguzi

     - Kipimo cha kuangalia vimelea vya bakteria katika mkojo (urine for culture and sensitivity)

    - Kipimo cha kuangalia vimelea vya bakteria kutoka katika majimaji yanayotoka kwenye tezi dume (Expressed Prostatic Secretions au EPS).Majimaji haya hupatikana wakati wa kufanya kipimo cha DRE ambapo daktari atagandamiza kidole chake kwenye tezi dume ili majimaji haya yatoke.Pia majimaji haya yanaweza kupatikana baada ya daktari kufanya kipimo hiki cha DRE kama hapo awali  daktari alishindwa kuyapata haya majimaji.

    - Kipimo cha kuangalia kiwango cha PSA kwenye damu kama nilivyoeleza hapo awali.Kawaida kiwango cha PSA huwa juu.

    - Semen analysis - Kipimo cha kuangalia shahawa za mwanamume.Katika kipimo hiki chembechembe za usaha (pus cells) zitaonekana kwa wingi kuliko kiwango cha shahawa, chembechembe za shahawa zinazoonekana hapa hazina uwezo  (non motile semen) wa kusafiri kwenda sehemu nyingine yoyote.Pia seli aina ya epithelial  huonekana hapa. 

Matibabu

     - Matumizi ya dawa za antibiotiki kwa muda mrefu (wiki 4-8).

     - Matumizi ya dawa aina za alpha blockers husaidia kwa wenye maambukizi sugu ambayo hayaishi

    - Maambukizi ya mara kwa mara ya aina hii ya prostatitis huweza kusababishwa na kutoweza kukojoa mkojo wote wakati wa kutoa haja ndogo kutokana na sababu mbalimbali kama uvimbe kwenye tezi dume, neurogenic bladder nk Matatizo ya vijiwe kwenye tezi dume na maumbile yanayohifadhi vimelea vya bakteria pia ni chanzo cha kujirudia kwa maambukizi haya sugu mara kwa mara.

 

Usikose sehemu ya pili na ya mwisho ya makala hii.

Imesomwa mara 12487 Imehaririwa Jumatatu, 25 Juni 2018 11:06
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.