Kupungua kwa ufyonzaji wa maji hutokana na
- Kufanyiwa upasuaji kipindi cha siku za nyuma katika eneo la kinena, au operesheni ya upandikizaji figo ambazo zinaweza kuathiri mfumo wa lymph na vena na hivyo kupunguza ufyonzaji wa maji kutoka kwenye mapumbu.
- Kuwahi kufanyiwa tiba ya mionzi kipindi cha nyuma nayo uhusishwa na kutokea kwa mabusha.
Kwa hapa kwetu Tanzania, kung’atwa na mbu aina ya Culex anayeeneza vimelea vya filaria kunaelezwa kuwa sababu kuu mojawapo inayopelekea kuwepo kwa tatizo la mabusha na matende hususani maeneo ya Pwani na mwambao.
Dalili za Mabusha
Katika hatua za awali, mabusha hayana dalili zozote (asymptomatic).
Hata hivyo, baada ya muda fulani, mapumbu hujaa na uvimbe huweza kuonekana hata kwa nje. Kwa kadiri uvimbe unavyozidi kuongezeka, dalili zifuatazo zaweza kujitokeza pia;
- Muhusika kujihisi hali ya uzito na kuvuta sehemu za siri kutokana na kujaa na kuongezeka kwa uzito wa mapumbu.
- Mgonjwa huweza kujihisi hali ya usumbufu na kutojisikia vizuri maeneo ya kinena mpaka mgongoni.
- Kwa kawaida mabusha hayana maumivu yeyote. Hata hivyo, iwapo mgonjwa ataanza kujihisi maumivu, hiyo ni dalili ya kuwepo kwa uambukizi katika mshipa wa epididymis (acute epididymitis)
- Uvimbe huwa na tabia ya kupungua iwapo mgonjwa atakaa kitako na huongezeka pindi anaposimama.
- Iwapo mgonjwa atajisikia homa, kichefuchefu na kutapika, hizo ni dalili za kuwepo kwa uambukizi katika mabusha.
- Kwa kawaida mabusha hayana muingiliano na uwezo na ufanisi wa utendaji wa ngono. Hata hivyo kuna taarifa tofauti za kitafiti kutoka bara Asia na Afrika Magharibi kuwa mabusha yanaweza kuathiri ufanisi wa ngono na kwa kiasi fulani kusababisha mhemko au msongo wa mawazo kwa muathirika.
Uchunguzi na Vipimo
Uchunguzi mzuri wa kitabibu (physical examination) huwezesha kugundua uwepo wa mabusha kwa kiasi kikubwa bila hata kuhitaji vipimo vya ziada. Vipimo uhitajika tu kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha mabusha, madhara yaliyoletwa na mabusha au kujua hali ya korodani.
Vipimo ni pamoja na
- Kupima damu (Full Blood Count) na mkojo (Urine Analysis) kuchunguza uwepo wa maambukizi kama vile vimelea wa filaria na mengineyo.
- Ultrasound ya kinena pamoja na mapumbu: Aina hii ya kipimo hufanywa ili kuchunguza uwepo wa matatizo mengine tofauti na mabusha. Matatizo hayo ni kama vile ngiri, uvimbe, kujinyonga kwa korodani (testicular torsion), majeraha katika korodani, damu kuvuja kwenye kwenye korodani (traumatic hemorrhage) au maambukizi.
Matibabu ya Mabusha
Kwa watoto wadogo, kwa kawaida mabusha hupotea yenyewe ndani ya mwaka mmoja. Iwapo hayajapotea, mtoto uhitaji kufanyiwa upasuaji kama tiba.
Kwa wanaume watu wazima, mabusha pia huweza kupona yenyewe bila kuhitaji tiba. Iwapo mabusha hayajapotea na yanamletea mgonjwa usumbufu (discomfort) au hali mbaya ya kiumbo (disfigurement) hayana budi kufanyiwa upasuaji ili kuyaondoa.
Njia za tiba ni
- Upasuaji: Upasuaji wa mabusha huweza kufanyika bila ya mgonjwa kuhitaji kulazwa (outpatient). Madhara yanayoweza kutokea wakati wa upasuaji wa mabusha ni pamoja na damu kuganda (blood clots), maambukizi au majeraha kwenye korodani. Hii ndiyo njia maarufu zaidi na ya kuaminika ya matibabu ya mabusha duniani kote.
- Kunyonya maji kwa kutumia sindano maalum (Needle aspiration): Njia nyingine inayotumika kutibu mabusha ni kuyanyonya maji kwa kutumia sindano maalum (needle aspiration). Hata hivyo njia hii haitumiki sana sehemu nyingi duniani kwa sasa kwa sababu maji ya mabusha huwa yana tabia ya kujirudia baada ya muda mfupi hata kama yatanyonywa.
Baadhi ya matabibu hupendelea kudunga dawa maalum za kuzuia maji yasijae tena (sclerosing agents) mara baada ya kunyonya na kuyaondoa maji yote.
Njia hii ya kunyonya maji ya mabusha, hufaa zaidi kwa wagonjwa wasioweza kuhimili upasuaji. Madhara yanayoweza kusababishwa na tiba ya namna hii ni pamoja na maambukizi na maumivu kwenye korodani.
Hata hivyo wakati mwingine, bila kujali ni tiba gani imetumika, mabusha huweza kujirudia baada ya matibabu.
Madhara ya Mabusha
Kwa kawaida mabusha hayana madhara yeyote. Aidha mabusha hayawezi kuathiri uwezo wa mtu kuzaa. Hata hivyo mabusha yanaweza kuleta madhara iwapo tu kama yakiambatana na magonjwa mengine kwenye korodani.
Kwa mfano, kama mabusha yataambatana na maambukizi (testicular infection) au uvimbe kwenye korodani (testicular tumor), yanaweza kusababisha kupungua kwa uzalishaji na utendaji kazi wa mbegu za kiume (sperms) na kupelekea tatizo la ugumba kwa wanaume.
Hali kadhalika, iwapo sehemu ya utumbo mkubwa au mdogo imebanwa katika upenyo fulani kwenye sehemu ya ukuta wa tumbo, huweza kusababisha ngiri (strangulated hernia), hali ambayo ni hatari kama isipotibiwa haraka.