Image

Watoto Wanaokunywa Juisi wapo Kwenye Hatari ya Kuugua Ugonjwa wa Pumu

  • Utafiti mpya unaonesha ya kwamba watoto wanaokunywa juisi au ambao mama zao walikunywa vitu vyenye sukari kipindi cha ujauzito wapo kwenye hatari kubwa ya kuugua ugonjwa wa Pumu
  • Wajawazito ambao walikunywa soda na vinywaji vyenye sukari (sugary beverages) wana asilimia 70 ya kuzaa watoto ambao baadae watapata ugonjwa wa Pumu

Matokeo ya utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani yameonyesha ya kwamba, watoto wanaokunywa vinywaji vyenye sukari au juisi (artificial juice) na ambao mama zao walikunywa soda kipindi cha ujauzito wao wapo kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa Pumu.

Watoto ambao waligundulika kuwa na kiwango kikubwa cha sukari aina ya fructose (ambayo hupatikana kwenye juisi au soda) kwenye milo yao kipindi cha ukuaji, walikuwa kwenye hatari ya asilimia 79 kupata ugonjwa wa Pumu ukilinganisha na watoto ambao hunywa vinywaji vyenye sukari kwa nadra au wale watoto ambao hawanywi kabisa vinywaji hivyo.

Kina mama ambao walitumia vinywaji vyenye sukari au soda kipindi cha ujauzito pia walikuwa kwenye hatari ya asilimia 70 kuzaa mtoto ambae baadae atagundulika kuwa na ugonjwa wa Pumu ikilinganishwa na kina mama ambao walitumia vinywaji vyenye sukari kwa nadra au ambao hawakutumia kabisa vinywaji hivyo kipindi cha ujauzito.

Matokeo ya utafiti huu yanazidi kuthibitisha ya kwamba sukari ina madhara mengi kwenye mwili wa binadamu, hivyo wataalamu na wanasayansi wanawaonya wanawake kuepuka vinywaji vyenye sukari kipindi cha ujauzito ili kuepuka ugonjwa wa kisukari kipindi cha ujauzito (gestational diabetes) pamoja na madhara mengine yanayotokana na sukari.

Wanasayansi hao kutoka Chuo Kikuu cha Harvard walifanya utafiti huu uliohusisha kina mama 1,000 pamoja na watoto wao, kwa kuchunguza jinsi wanavyokula miilo yao (eating habits), taarifa za afya za watoto (Health information) pamoja na kuangaliaa iwapo watoto hao walipata ugonjwa wa Pumu walipotimiza umri wa miaka saba hadi miaka tisa.Taarifa walizozipata walizichanganua kwa kuangalia kama kuna uhusiano wowote baina ya ugonjwa wa Pumu,soda na vinywaji vingine vyenye sukari kwa watoto.

Tafiti mbalimbali zilizopita zimewahi kuonyesha kuwepo kwa uhusiano kati ya vinywaji vyenye sukari na uzito uliopitiliza (obesity), pamoja na uhusiano kati ya ugonjwa wa Pumu na uzito uliopitiliza.

Utafiti huu uliofanywa na Chuo Kikuu cha Harvard pia ulionyesha ya kwamba sio tu watoto wenye uzito mkubwa (overweight) au uzito uliopitiliza (obesity) hupata ugonjwa wa pumu bali hata ulaji wao wa kiwango kikubwa cha sukari aina ya fructose unawaweka watoto hawa kwenye hatari ya asilimia 77 ya kupata ugonjwa wa Pumu.

Utafiti huu uliochapishwa kwenye jarida la The Annals of the American Thoracic Society ulionyesha kwamba, wanawake ambao hutumia vinywaji vingi venye sukari wanakuwa na uzito uliopitiliza, wenye  kipato na elimu duni ikilinganishwa na wanawake ambao huepuka vinywaji vyenye sukari au soda.Hata baada ya kuangalia vigezo hivyo hapo juu, bado watafiti waliweza kuona uwepo wa mahusiano kati ya vinywaji vyenye sukari, soda na ugonjwa wa Pumu.

Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha ya kwamba sio tu vinywaji venye sukari na sukari aina  ya fructose husababisha ugonjwa wa Pumu kupitia tatizo la uzito uliopitiliza, bali kuna mfumo wa ziada unaosababisha ugonjwa wa Pumu kupitia vinywaji vyenye sukari au soda. ’’Mpaka sasa hatukuweza kujua chanzo sahihi cha vinywaji hivi vyenye sukari na fructose kusababisha ugonjwa wa Pumu.Ingawa tunaamini ya kwamba vinywaji hivyo pamoja na fructose husababisha mcharuko (inflammation) kwenye mapafu ya watoto hivyo huchangia mtoto kupata ugonjwa wa Pumu’’ Alisema Rifas-Shiman, mtafiti aliyehusika kwenye utafiti huu.

Moja ya udhaifu wa utafiti huu ni kwa watafiti kutegemea sana kina mama kuwapa historia yao ya matumizi ya vinywaji vyenye sukari kipindi cha ujauzito pamoja na historia ya afya za watoto wao.

Ulaji mzuri wa milo yenye virutubisho sahihi ni muhimu sana kipindi cha ujauzito kwani husaidia katika ukuaji wa mtoto pamoja na kumkinga mtoto dhidhi ya magonjwa sugu kama ugonjwa wa Pumu.

Wanawake wajawazito wanashauriwa kula vyakula vyenye virutubisho vyote muhimu kama matunda,mbogamboga, vyakula vya wanga kama mikate na ngano, vyakula vyenye protini kama nyama nyeupe (kuku, aina mbalimbali za samaki), maziwa, maharage, mayai nk.

Ugonjwa wa pumu huambatana na viashiria vya kukohoa, kifua kubana, kuishiwa  pumzi, kutokwa na mlio wakati wa kuhema (wheezing sound).Ugonjwa huu unarithishwa kutoka kwa wazazi na pia huweza kusababishwa na visababishi angani (environmental factors) kama hewa chafu (air pollution) na visababishi vya mcharuko mwili  (allergens).Ugonjwa  wa Pumu hauna tiba

Ushauri kutoka TanzMED

Kitaalamu kila tafiti haikosi udhaifu wake hivyo ni vizuri kutambua ya kwamba udhaifu wa utafiti haufanyi au hauondoi umuhimu wa tafiti husika.Bado tafiti hii ni nzuri hasa ukizingatia imefanyika kwa kuhusisha watu wengi (1,000).Ni bora kwa wajawazito kuchukua tahadhari kwa kuepuka kunywa kwa wingi vinywaji vyenye sukari (sugary beverages), juisi na soda.

Kwa taarifa zaidi kuhusu ugonjwa wa Pumu soma makala yangu ya Ugonjwa wa Pumu kwenye tovuti yako ya TanzMED.

Imesomwa mara 5791 Imehaririwa Ijumaa, 27 Aprili 2018 14:25
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.