Safari ya kila mtoto kuzaliwa ni ya kipekee sana, lakini safari zote huanzia kwenye muungano wa yai la mwanamke (ovum) na mbegu ya kiume (sperm). Mchakato huu unaendelea kwa miezi tisa ndani ya mwili wa mwanamke, na hatimaye kuzaliwa kwa mtoto. Katika makala hii, tutafuatilia kwa karibu hatua zote muhimu katika safari ya kupevushwa yai na mpaka kuzaliwa kwa mtoto.
Upevukaji wa Yai
Kwa kawaida, mtoto wa kike huzaliwa akiwa na mayai yanayokadiriwa milioni 1 hadi 2. Kwa wakati huu wa utotoni, mayai haya huwa yamesinzia (dormant) hadi kufika kipindi cha kubalehe (kuvunja ungo). Baada ya kubalehe, na endapo hakuna changamoto yoyote katika mfumo wa uzazi, basi kila mwezi mwili wa mwanamke huruhusu mayai kadhaa kepevuka ndani ya mfuko wa mayai (Ovary).
Kwa mazingira ya kawaida (isipokuwa mapacha wasiofanana) yai moja tu lililo bora zaidi kati ya mengi yaliyopevuka ndiyo huruhusiwa kutoka (Ovulation) na yale mengine yaliyopevuka na hayaruhusiwa kutoka huliwa na mwili. Yai hili lililotolewa linapotoka kwenye mfuko wa mayai hupita kwenye mirija ya fallopian na kisha kufika katika mji wa mimba (uterus) tayari kwa ajili ya uchavushwaji (fertilization), yai hili lina uhai wa masaa kati ya 12 hadi 24, na ndio wakati mzuri kwa mbegu ya kiume kuungana nalo ili kutunga ujauzito.
Uchavushaji:
Wakati wa tendo la ndoa, mamilioni ya mbegu za kiume(sperm) huingia kwenye uke wa mwanamke na mbegu hizi huogelea kwa msaada wa kimiminika kilichopo kwenye manii kupitia kizazi hadi kwenye mirija ya fallopian katika kutafuta yai. Kati ya mbegu nyingi zilizofanikiwa kufika kwenye yai, ni mbegu moja tu yenye ubora zaidi ndiyo itafanikiwa kuingia kwenye yai la kike na hapa ndipo uchavushaji (Fertilization) inakuwa imekamilika.
Baada ya mbegu moja kuingia, yai hujifunga na kutoruhusu tena mbegu za kiume kuingia kwenye yai kwa ajili ya uchavushaji. Mchanganyiko huu wa yai na mbegu huunda seli moja inayoitwa zygote. Seli hii ndio mwanzo wa maisha mapya na ina mchanganyiko wa DNA kutoka kwa wazazi wote wawili. Kisayansi, mtoto huchukua 50% ya DNA kutoka kwa kila mzazi. Nusu kutoka kwa baba na nusu kutoka kwa mama.
Ndani ya DNA kuna vitu vinaitwa chromosomes, na kila binadamu ana chromosomes 46 tu, 23 kutoka kwa baba na 23 kutoka kwa mama.Kati ya hizi chromosomes 23, 22 zinafanana kabisa lakini chromosomes ya 23 huitwa Sex chromosome na ndio itakayo amua jinsia ya mtoto.
Endapo kwa sababu zozote zile, hakutokuwa na yai lililochavunshwa, basi ukuta ulioundwa ndani ya uterus kwa ajili ya mapokeo ya zygote huvunjika na ndiyo sababu kila mwezi mwanamke ambaye bado hajakoma siku hupata hedhi.
Upachikanaji:
Zygote huanza kugawanyika na kuunda seli nyingi zaidi huku ikitafuta mahali pakujipachika katika mji wa mimba. Kujipandikiza huku hutokea ndani ya siku 6 hadi 12 baada ya fertilization. Baada ya hatua hii kumalizika kikamilifu Kondo (placenta) huundwa na ndiyo tunaweza kusema kuwa mwanamke ana ujauzito. Mwili wa mwanamke huanza kutengeneza hormone ya HCG (Human Chorionic Gonadotropin) ambayo itaanza kuleta dalili za mimba.
Ukuaji wa Mtoto
Baada ya kujipachika, seli zile huanza kugawanyika na kujipanga ili kuunda viungo vya mtoto.
Katika wiki za mwanzo, mtoto anaitwa embryo. Baada ya wiki ya nane, mtoto anaitwa fetus.Fetus huendelea kukua na kutengeneza viungo vyote vya muhimu. Ujauzito umeganyika katika vipindi vitatu tangu fertilization hadi kujifungua. Vipindi hivi huitwa trimesters.
Trimester ya Kwanza (Wiki 1-12):
- Wiki 1-2: Fertilization hufanyika, na zygote huanza kugawanyika na kufanya implantation.
- Wiki 3-8: Mtoto anaitwa embryo na viungo vyote muhimu huanza kuundwa. Moyo huanza kudunda, ubongo na mfumo wa fahamu huanza kuundwa. Wakati huu ni muhimu sana mama apate madini ya folic acid ili kuhakikisha mifumo hii inaundwa kwa usahihi.
- Wiki 9-12: Mtoto anaitwa fetus sasa. Viungo vyote muhimu vimeundwa, na mtoto anaanza kufanya harakati ndogo ndogo huku viungo vikiendelea kukomaa na kuimarika.
Trimester ya Pili (Wiki 13-27):
- Wiki 13-16: Mtoto anakua kwa kasi, na mama anaweza kuanza kuhisi mtoto akisogea au kucheza tumboni.
- Wiki 17-20: Ngozi ya mtoto inakuwa laini, na nywele za kichwa zinaanza kukua. Wakaiti huu kipimo cha ultrasound kinaweza kuonyesha jinsia ya mtoto.
- Wiki 21-24: Mapafu ya mtoto yanaanza kukomaa, lakini bado hayajakamilika na mtoto akizaliwa wakati huu, hataweza kupumua mwenyewe.
Trimester ya Tatu (Wiki 28-40):
- Wiki 28-32: Mtoto anaendelea kukua na kuongezeka uzito. Mafuta huanza kujilimbikiza chini ya ngozi, lakini bado hayupo tayari kwa maisha nje ya mji wa wimba.
- Wiki 33-37: Viungo vyote vya mtoto vimemaliza kukua. Mpaka wiki ya 34 kukamilika, mapafu nayo yanakua tayari yamekomaa na mtoto anaweza kuzaliwa wakati wowote baada ya hapo na akawa na uwezo mkubwa wa kuendelea kuishi nje ya tumbo la mama.
- Wiki 38-40: Mtoto anazingatiwa kuwa amekomaa kikamilifu na anaweza kuzaliwa wakati wowote. Mtoto akizidi kukaa tumboni zaidi ya hapo ni hatari, na uchungu usipoanza wenyewe, harakati za kuanzisha uchungu zinaweza kuanzishwa ili mama na mtoto wote waweze kuwa salama.
Kuzaliwa:
Baada ya miezi tisa, mtoto atakuwa tayari kuzaliwa. Mchakato wa kuzaliwa huanza na uchungu (contractions), ambao husaidia kufungua njia ya kizazi. Njia inapofika sentimita 10 mama huanza kusukuma na mtoto hutolewa. Kuna sababu kadhaa zinazoweza kuzuia mama kujifungua kwa njia hii na kuhitaji njia mbadala ambayo ni ya upasuaji (Cesarean section). Baada ya mtoto kutoka, kitovu (umbilical cord) hukatwa na kisha kondo kutolewa.
Hitimisho
Uzazi ni safari ya kipekee yenye kustaajabisha, Kutoka kwa mchanganyiko wa yai na mbegu hadi kuzaliwa kwa mtoto mpya, kila hatua ni muhimu katika kuunda maisha mapya. Kwa kuelewa mchakato huu, tunaweza kufahamu zaidi umuhimu wa afya ya uzazi na kuunga mkono wanawake wajawazito katika safari hii ya ujasiri.
Unaweza kutumia TanzMED App kwa ajili ya kufuatilia ujauzito au kupanga ujauzito wako.