Image

Ufahamu ugonjwa wa Tetekuwanga, Chanzo, Dalili na Tiba.

Ni ugonjwa unaowaathiri sana watoto mpaka kufananishwa kuwa ni moja ya hatua za ukuaji wa mtoto. Mgonjwa wa tetekuwanga hutokewa na vijipele vyenye majimaji mwili mzima. Vijipele hivi huwa vinawasha kitendo kinachomfanya mgonjwa wa tetekuwanga kutojisikia vizuri huku akishinda anajikuna mwili mzima. Tetekuwanga husababishwa na virusi kwa kitaalamu hujulikana kama Varicella Zoster (VZV).

Mara nyingi ugonjwa huu wa tetekuwanga huwa haujirudii, hii ndiyo sababu imezoeleka sana kwa wengi kusema kama haujawahi kuugua basi usikae karibu na mgonjwa wa tetekuwanga. Ikumbukwe kuwa, ugonjwa wa tetekuwanga unayo kinga ingawa hapa kwetu upatikanaji wake bado haujasambaa sehemu zote.

Dalili za ugonjwa wa tetekuwanga

Dalili kuu za ugonjwa wa tetekuwanga ni vijipele (kama malengelenge) vinavyowasha. Ugonjwa huu huchukua muda mpaka kuanza kujitokeza kwa dalili zake, mgonjwa wa tetekuwanga ataanza kuona dalili hizi baada ya siku 21 tangu virusi vya ugonjwa huu kuingia kwenye mwili wake (baada ya maambukizi). Ukiachana na vijipele vinavyowashwa, dalili nyingine za ugonjwa wa tetekuwanga ni kama;

  • Kuumwa kwa kichwa
  • Homa
  • Kupungukiwa kwa hamu ya kula

Hizi ni dalili za awali ambazo huanza kujitokeza kabla ya vipele kuanza kuchomoza, mara nyingi huchukua siku moja au mbili mara baada ya kuanza kusikia dalili hizi mpaka kuanza kujitokeza kwa vijipele. Vijipele vya tetekuwanga hupitia hatua kadhaa;

  • Vijipele vyekundu au pinki hujitokeza mwili mzima
  • Vijipele huiva na kuanza kutoa majimaji
  • Vijipele vinavywea na kuanza kukauka

Kumbuka, vijipele hivi havijitokezi kwa wakati mmmoja, hivyo wakati vingine vinapona, kuna vingine vitakuwa ndiyo vinatokeza.

Mgonjwa huendelea kujisikia vibaya mpaka vijipele vikauke, na hatua hii huweza kuchukua hadi wiki mbili mpaka kupotea kabisa.

Nini husababisha Tetekuwanga?

Kama tulivyoeleza hapo juu, tetekuwanga husababishwa na virusi ambavyo kwa kitaalamu hujulikana kama Varicella Zoster (VZV). Mara nyingi ugonjwa wa tetekuwanga huambukizwa kutokana na kugusana na mtu mwenye ugonjwa wa tetekuwanga. Virusi vya tetekuwanga huendelea kuwa na uwezo wa kuambukiza mpaka malengelenge (vijipele) viwe vimetumbuka na kukauka. Hivyo epuka makutano na mgonjwa wa tetekuwanga mpaka vipele vitakapokauka kabisa. Virusi hivi huweza kuambukizwa kwa njia zifuatazo;

  • Mate
  • Kukohoa
  • Kupiga chafya
  • Kugusa majimaji ya malengelenge ya tetekuwanga

Makundi yaliyo kwenye hatari ya kupata Tetekuwanga

Watu waliowahi kuumwa au kutumia kinga za tetekuwanga ni ngumu sana kupata maambukizi ya tetekuwanga. Pia, mtoto mchanga huweza kulindwa dhidi ya maambukizi ya tetekuwanga kutokana na kinga kutoka kwa mama yake ambayo huzaliwa nayo, lakini kinga hii huendelea kudumu kwa miezi mitatu tuu.

Mtu yoyote ambaye hajawahi kuumwa tetekuwanga, yupo kwenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu, lakini makundi yafuatayo yapo kwenye hatari kubwa zaidi;

  • Wanaoishi na wagonjwa wa tetekuwanga
  • Walio chini ya umri wa miaka 12
  • Wanaoishi na watoto
  • Wanaohudumia watoto kwenye vituo vya kulelea watoto au shule za watoto
  • Wenye upungufu wa kinga uliosababishwa na magonjwa au kuugua.

Uchunguzi wa Tetekuwanga

Inashauriwa uende hospitali mara moja baada ya kuona vijipele visivyoeleweka, haswa kama vijipele hivyo vitaambatana na baridi yabisi au homa.

Daktari atavichunguza vijipele, pia uchunguzi wa kimaabara utahitajika ili kuhakikisha kama ni kweli vijipele hivyo ni vya ugonjwa wa tetekuwanga.

 

Dalili mbaya za tetekuwanga

Nenda hospitali haraka iwezekanavyo kama utatokewa na moja ya dalili zifuatazo;

  • Vijipele vimetapakaa hadi machoni
  • Vijipele vimekuwa vyekundu sana, vinauma na vya ujoto (hii inaweza kumaanisha kuna mashambulizi ya bakteria)
  • Unajisikia kizunguzungu
  • Unapata shida kwenye kupumua

Mara nyingi makundi ambayo yapo kwenye hatari ya kupata madhara makubwa mpaka yakapelekea kutokea kwa dalili mbaya za tetekuwanga ni;

  • Watu wazima
  • Wazee
  • Watu wenye upungufu wa kinga
  • Wamama wajawazito

Ukiachana na Tetekuwanga, makundi haya, pia yapo kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa tetekuwanga ikaambatana na maambukizi ya VZV pneumonia au bakteria wanaoshamulia ngozi, maungio na mifupa.

Endapo mama mja mzito atashambuliwa na virusi vya tetekuwanga, basi kuna uwezekano wa kujifungua mtoto mwenye matatizo kama;

  • Kutokukua vizuri
  • Kichwa kidogo
  • Matatizo ya macho

Matibabu ya Tetekuwanga

 Mara nyingi watu walioambukizwa virusi vya tetekuwanga, hushauriwa kuanza kutumia dawa zitakazowasaidia kupunguza athari za tetekuwanga kama Homa, kuwaswha nk. Kwa watoto wenye afya bora, cha muhimu ni kudhibiti dalili, kwahiyo hutumia dawa za kupaka Calamine lotion ambayo hudhibiti vipele, na dawa ya kunywa antihistamines kama Cetrizine.

Kwa wagonjwa wenye upungufu wa kinga mwilini, hupewa dawa zifuatazo interferon alpha, acyclovir. Wazazi wanashauri wasiwapeleke watoto kwenye maeneo yenye mkusanyiko kama shule, sehemu za kuchezea nk ili kuepuka kuwaambukiza wengine. Kama ni mtu mzima, inashauriwa kutotoka nje mpaka utakapopona.

Daktari atakuandikia dawa zitakazokusaidia kukabiliana na dalili za ugonjwa huu na siyo kutibu ugonjwa, bali kupunguza makali yaletwayo na tetekuwanga. Kwa kupunguza makali kutakupelekea mfumo wa kinga kupona haraka. 

Jinsi ya kujikinga na Tetekuwanga

Mwaka 1995 mamlaka ya chakula na dawa ya Marekani ilipitisha matumizi ya Chanjo kwa ajili ya ugonjwa huu kwa watoto wenye afya bora na watu wazima wenye afya bora.

Matumizi ya kinga ya tetekuwanga yanaweza kusaidia kupunguza uwezekano wa kushambuliwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa huu. Kinga hii hutolewa kwa watoto wadogo kuanzia miezi 12 hadi 15 na baada ya miaka 4 au 6 inashauriwa kurudia ili kuimarisha nguvu Zaidi.

Kwa watu wazima ambao hawajawahi kuumbwa tetekuwanga na wala kupata kinga, wanashauriwa kuepuka kukutana na watu wanaoumwa tetekuwanga.

 

Picha kwa hisani ya http://kelly.worldconcern.org

Imesomwa mara 32694 Imehaririwa Jumatatu, 19 Septemba 2022 12:54
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.