Usonji ni tatizo linalojitokeza mapema utotoni, ambapo mtoto huwa na mapungufu kwa kupenda kujitenga na kutotaka kuwa karibu na watu (Impaired social interaction), hupata matatizo ya lugha na shida ya mawasiliano (impaired language and communication skills) na huwa na tabia ya kurudia rudia kitu anachokifanya mara nyingi (restrictive repetitive behaviour).
Mara nyingi wazazi hugundua watoto wao wana tatizo hili katika kipindi cha miaka miwili ya umri wa mtoto.Chanzo halisi cha tatizo hili la usonji hakijulikani ingawa matatizo ya kijenetiki (Neurodevelopmental disorder) ndio uhusishwa na tatizo la usonji.Maaambukizi ya Rubella au matumizi ya pombe na madawa ya kulevya aina ya coccaine wakati wa ujauzito na hata sababu za kimazingira, yote haya uhusishwa na tatizo hili la usonji.
Watoto wa kiume huathirika sana ikilinganishwa na watoto wa kike. Kwa kila watoto watatu wa kiume wenye kupata usonji ni mtoto mmoja tu wa kike anaepata usonji.
Jarida la The Lancent la mwaka 2013, linasema watu wapatao milioni 21.7 wameathirika kwa tatizo hili la usonji ulimwenguni kote 1. Tabia za kujirudia rudia kwa mtoto aliyeathirika na tatizo la usonji zimegawanyika katika makundi yafuatayo;
- Tabia zilizozoeleka - Kama kupiga piga mikono, kutikisa tikisa kichwa mara kwa mara na kujibiringisha mwili
- Tabia ambazo huchukua sana muda kama za kupanga panga vitu kwa mpangilio maalum au kuosha mikono mara kwa mara
- Tabia ya kung’ang’ania vitu visihamishwe kwa mfano viti au kutokubali kukatizwa katizwa
Ugunduzi (Diagnosis)
Ugunduzi wa tatizo hili la usonji hufanyika kwa
- Daktari wa watoto (Pediatrician) kumpima vipimo vya kawaida pamoja na kuchukua historia ya ukuaji wa mtoto husika (Developmental milestones)
- Daktari bingwa wa watoto aliyebobea kwenye matatizo ya kisaikolojia ya watoto (Pediatric neuropsychologists) kumpima ili kuangalia tabia za mtoto huyu na uwezo wake wa kiakili (Cognitive skills)
- Vipimo vya kijenitikia (genetics testing) kama high-resolution chromosome and fragile X testing. Hufanyika baada ya kugundulika kwamba chanzo cha tatizo la usonji ni matatizo ya kijenetiki
Kadri mtoto anavyoendelea kukuwa ndio usonji unavyoweza kutambulika kwa urahisi zaidi kwani madhara yake yanaonekana kwa urahisi wakati wa ukuaji wa kiakili wa mtoto.
Uchunguzi
Mchunguze mtoto wako kwa viashiria vya tatizo la usonji mapema zaidi kwani kumchelewesha mtoto mwenye usonji kupimwa na kupewa tiba mapema huchangia tatizo hili kuwa kubwa zaidi na hivyo kuathiri matokeo ya matibabu ya tatizo hili. Nusu ya wazazi hugundua watoto wao wana tabia zisizo za kawaida ndani ya miezi 18 ya umri wa mtoto, na moja ya tano ya wazazi hugundua ya kwamba watoto wao wana tabia zisizo za kawaida ndani ya kipindi cha miezi 24 ya umri wa mtoto 2.Tabia hizi ambazo si za kawaida katika ukuaji wa mtoto ni;
- Kutotamka maneno ya kitoto (no babbling) mpaka anapotimiza umri wa mwaka mmoja
- Kushindwa kuotesha kidole au kumpungia (waving, gesturing etc) mzazi/mtu yoyote mkono mpaka anapotimiza umri wa miezi 12
- Kushindwa kutamka neno lolote mpaka anapotimiza umri wa miezi 16
- Kutotamka maneno mawili kwa pamoja au sentensi mpaka umri wa miezi 24
- Kupoteza uwezo wa kuongea au kutokuwa na tabia ya kutangamana/kuchanganyikana na watu wengine wakati wowote ule katika umri wa mtoto
Matibabu
Familia yenye mtoto mwenye tatizo la usonji huhitaji kuelemishwa jinsi ya kuishi na mtoto huyo pamoja na kusaidiwa katika malezi yake. Kwa kuwa tatizo hili halitibiki ni muhimu mtoto kupata:
- Tiba ya Tabia
- Uchambuzi wa tabia (ABA): Kutumia utaalamu wa kisaikolojia kufundishia na kuwahusisha na jamii, kuboresha mawasiliano, na usimamizi wa kitabia
- Matibabu na elimu ya usonji kwa kuboresha mawasiliano kwa watoto wenye ulemavu (TEACCH)
- Tiba nyingine muhimu ni kuelimisha jamii kuhusu watoto wenye usonji , jinsi ya kuishi nao na kuwaanzishia watoto wenye usonji matibabu mapema.
Marejeo
- Global Burden of Disease Study 2013 Collaborators (2015)."Global, regional, and national incidence, prevalence, and years lived with disability for 301 acute and chronic diseases and injuries in 188 countries, 1990–2013: a systematic analysis for the Global Burden of Disease Study 2013.". Lancet. 386: 743–800. doi:1016/S0140-6736(15)60692-4. PMC 4561509. PMID 26063472.
- Landa RJ (2008). "Diagnosis of autism spectrum disorders in the first 3 years of life". Nat Clin Pract Neurol. 4 (3): 138–47. doi:10.1038/ncpneuro0731. PMID 18253102