Image

Fibroids; Chanzo, vipimo na matibabu yake

Fibroids ni moja ya matatizo yanayowasumbua wanawake wengi , kwa lugha ya kawaida, Fibroids maana yake ni uvimbe wa msuli wa kifuko cha uzazi. Uvimbe huu unaweza kuwa na ukubwa tofauti kuanzia kama punje ya harage mpaka ukubwa wa nazi. Wakati mwingine unaweza kudhani ni ujauzito!

Sio kila mwenye fibroids anakuwa na matatizo kiafya. Zinaweza kuwepo miaka mingi bila matatizo yoyote. Hata hivyo inashauriwa kila mwenye fibroids awe anapimwa na daktari angalau mara moja kwa mwaka ili kuona jinsi zinavyoendelea na kuhakikisha kuwa hazikui kwa kasi au kuhatarisha kuwa kansa.

Kwa wale zinaowaletea matatizo, fibroids husababisha kutokwa na damu nyingi za hedhi, maumivu ya tumbo, mimba kuharibika zikiwa changa, kuzaa watoto njiti na fibroid kukandamiza viungo vingine kama kibofu cha mkojo na kusababisha kukojoa mara kwa mara au matatizo ya haja kubwa.

Njia ya kugundua uwepo wa fibroid ni kupimwa na daktari na kufanyiwa ultrasound.

Matibabu yake yapo ya aina kuu tatu:

1. Kunywa dawa. Hata hivyo dawa zilizopo sasa hazina matokeo mazuri kuondoa fibroids ila husaidia kupunguza ukuaji wake.

2. Kuiondoa fibroid kwa operation. Ziko aina nyingi za operation kupitia kwenye tumbo au kupitia ndani ya kifuko cha uzazi. Aina ya operation hutegemea mahali ilipo fibroid.

3. Kuondoa kifuko cha uzazi. Njia hii huwafaa wale ambao hawana mpango wa kupata mtoto.

Kuna nadharia mbalimbali juu ya vitu vinavyosababisha fibroids lakini hakuna kitu kilichothibitika moja kwa moja kuwa chanzo cha fibroids. Kwa wale wenye uzito mkubwa inashauriwa kupunguza mwili kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata fibroids.


Zipo tafiti zinazoonyesha kuwa matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango vinapunguza uwezekano wa kupata fibroids.

Imesomwa mara 6734 Imehaririwa Alhamisi, 07 Novemba 2019 17:16
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.