Image

Maambukizi Katika Mfumo wa Uzazi wa Mwanamke (PID)

Maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke kwa kitaalamu Pelvic Inflamatory Diseases au kwa kifupi PID, ni moja ya matatizo ambayo huwaathiri sana wanawake. Kwa kawaida maambukizi haya huusisha shingo ya uzazi (cervix) hali ambayo hujulikana kama cervicitis, nyama ya mfuko wa uzazi (endometrium) ambayo kitaalamu huitwa endometritis, na mirija ya uzazi (fallopian tubes) hali ijulikanayo kitabibu kama salpingitis.

 PID husababishwa na nini? 

Pamoja na aina kadhaa za vimelea kuhusishwa na PID, vimelea vya jamii ya Neisseria Gonorrhoeae pamoja na Chlamydia trachomatis ndivyo vinavyoongoza kwa umaarufu zaidi katika kusababisha PID kwa akina mama.

Je mwanamke huambukizwaje PID?

Kuna njia kadhaa ambazo mwanamke anaweza kuambukizwa PID. Njia hizo ni pamoja na

  • Kufanya ngono isiyo salama
  • Maambukizi ya njia ya uzazi hasa kipindi mara baada ya kujifungua (au postpartum period)
  • Maambukizi ya njia ya uzazi mara baada ya kutoa mimba kwa njia zisizo salama (post abortion) au mara baada ya mimba kutoka (miscarriage)
  • Kutumia vipandikizi vya ndani ya mfuko wa uzazi (IUCD) kama njia mojawapo ya uzazi wa mpango, na
  • Kuambukizwa kupitia damu iliyo na vimelea vya PID.

Dalili za PID ni zipi?

Zipo dalili kadhaa za ugonjwa huu wa PID. Miongoni mwa dalili hizi ni

  • Mwanamke kuhisi maumivu ya tumbo hasa maeneo ya chini ya kitovu
  • Kupata maumivu ya mgongo
  • Mwanamke kupata utoko mchafu sehemu za siri. Utoko huu huambatana na harufu mbaya.
  • Kuhisi maumivu wakati wa kukojoa
  • Kupata maumivu wakati wa tendo la ndoa
  • Kutoka damu bila mpangilio wakati wa hedhi
  • Kupata homa
  • Wakati fulani kuhisi kichefuchefu na
  • Pia kutapika

Vipimo vya PID

Ili kuweza kutambua kama mwanamke ameambukizwa ugonjwa huu, tabibu anaweza kufanya vipimo kadhaa vikiwemo

  • Kuchunguza mkojo ili kufahamu kama mgonjwa ana mimba. Kipimo hiki ni muhimu hasa kwa mwanamke aliye katika umri wa kuzaa au mwenye uwezo wa kubeba mimba
  • Uchunguzi wa  mkojo kwenye darubini ili kutambua aina za vimelea vinavyomletea mgonjwa uambukizi. Aidha mkojo huweza kuoteshwa katika maabara kwa ajili ya kutambua aina nyingine za vimelea viletavyo uambukizi huo.
  • Kupima damu kwa ajili ya kuchunguza jinsi aina mbalimbali za chembe za damu zilivyoathiriwa na uambukizi huo au kama kuna mwingiliano na magonjwa mengine yaliyojificha. Kipimo hiki kwa kitaalamu huitwa Full Blood Picture.
  • Kuchukua utando unaozunguka shingo ya uzazi na kuuotesha kwa ajili ya utambuzi wa aina za vimelea viletavyo maambukizi hayo. Kipimo hiki huitwa cervical culture
  • Aidha ni muhimu pia kufanya vipimo vingine kwa ajili ya utambuzi wa magonjwa yaambukizwayo kwa njia ya kujamiiana, kama vile virusi vya ukimwi na kisonono.
  • Mgonjwa pia anaweza kufanyiwa ultrasound ya nyonga ili kuangalia kama kuna athari yeyote katika mfumo wake wa uzazi.

Matibabu

Mara mgonjwa anapogunduliwa kuwa ameathiriwa na ugonjwa huu, dawa za jamii ya antibayotiki huweza kutumika kwa ajili ya kuua vimelea vya ugonjwa. Hata hivyo ieleweke kuwa matumizi ya dawa hizi hufuata miongozo mbalimbali ambayo imewekwa na wizara au mamlaka za afya zinazohusika. Miongozo hii hutofautiana kati ya sehemu na sehemu au nchi na nchi, ingawa kiujumla Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo limeweka muongozo wake kwa ajili ya kufuatwa na nchi mbalimbali.

Miongoni mwa dawa hizo ni pamoja na Cefotetan na Doxycycline; Clindamycin pamoja na Gentamycin; Ampicillin na Sulbactam kwa pamoja na Doxycycline; na Ceftriaxone au Cefoxitin pamoja na Doxycycline.

Ieleweke pia haishauriwi kujinunulia na kutumia dawa hizi bila kupata ushauri ushauri wa mtaalamu wa afya. Aidha ili kuondoa maumivu na kushusha homa, dawa kama Paracetamol (Panadol) yaweza kutumika.

Jinsi ya kuzuia maambukizi katika mfumo wa uzazi

Kuna njia kadhaa za kuzuia maambukizi katika mfumo wa uzazi. Njia hizi ni pamoja na

  • Kufanya ngono salama kwa kutumia kondomu au kama ikiwezekana kujizuia kabisa kufanya ngono.
  • Kuwahi kuwaona wataalamu wa afya mara dalili za ugonjwa huu zinapoanza kujitokeza au pindi tu unapogundua kuwa mwenzi wako ana dalili za magonjwa ya zinaa
  • Kufanya vipimo mara kwa mara hasa vya mfumo wa uzazi, pamoja na vipimo vya maambukizi ya magonjwa yanayosambazwa kwa njia ya ngono (STI).
  • Kutofanya ngono mara baada ya kujifungua, mimba kutoka au mara baada ya kutoa mimba ili kuhakikisha njia ya shingo ya uzazi imefunga vema.

 

Imesomwa mara 33851 Imehaririwa Jumatatu, 18 Februari 2019 16:03
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.