Image

Maambukizi katika kuta za ndani za moyo (Infective Endocarditis)

Hutokea pale vimelea (bakteria) wanapovamia kuta za ndani za moyo (endocardium), zikiwepo valve na kusababisha maambukizi.

Hakuna mishipa ya damu ambayo ni mahususi kwa ajili ya kupeleka damu safi moja kwa moja kwenye valve za moyo, hivyo chembe chembe nyeupe za damu (ambazo ni mahususi kwa ajili ya kinga ya maambukizi) hufika kwa shida sana kwenye valve za moyo. Hali hii husababisha chembe chembe nyeupe kuwa butu  pale vimelea (bakteria) wanapotengeneza uoto (vegetations) kwenye valve za moyo. Na kwa sababu ya hakuna mishipa ya damu ambayo ni mahususi kwa ajili ya kupeleka damu moja kwa moja kwenye valve za moyo, matibabu yake husumbua sana kwakuwa ni vigumu dawa kufika kwenye eneo husika.

Maambukizi katika kuta za ndani za moyo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili kutokana na  jinsi ugonjwa ulivyo-anza (onset):

Maambukizi ya kuta za ndani za moyo ya papo kwa hapo kitaalamu acute bacteria endocarditis 

huanza kati ya siku kadhaa hadi wiki kadhaa, na mgonjwa huwa maututi; na maambukizi katika kuta za ndani za moyo ndogo ya papo kwa hapo kitaalamu sub acute bacteria endocarditis- huanza kati ya wiki kadhaa hadi miezi kadhaa, na dalili hutokea pole pole

Na vile vile maambukizi haya yanaweza kugawanywa kama ifuatavyo

  • Maambukizi katika kuta za ndani za moyo ya Valve asili au kitaalamu native valve endocarditis
  • Maambukizi katika kuta za ndani za moyo ya Valve za bandia au kitaalamu prosthetic valve endocarditis
  • Maambukizi katika kuta za ndani za moyo kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya kwa njia ya mshipa kitaalamu intravenous drug abuse endocarditis

Je ni vimelea gani husababisha Maambukizi katika kuta za ndani za moyo?

Vimelea vifuatavyo vinaongoza kwa kusababisha maambukizi katika kuta za ndani za moyo

  • Staphylococcus aureus
  • Streptococcus viridians
  • Streptococcus intermedius
  • Group B streptococci
  • Pseudomonas aeruginosa
  • enterococci
  • vimelea wa bakteria walio katika kundi lijulikanalo kama HACEK
  • Fangasi wa aina mbalimbali

Ni watu gani wapo kwenye hatari ya kupata Maambukizi katika kuta za ndani za moyo?

  • Ambao walishaugua tatizo hili awali
  • Wenye kisukari
  • Wajawazito
  • Wenye matatizo mengine ya valve za moyo (Rheumatic valvular heart disease)
  • Kung’oa jino au meno
  • Waliofanyiwa upasuaji mdogo kuwekewa kifaa cha kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker)
  • Kutokuwa na vihatarishi hivyo haimanishi huwezi kuugua tatizo hili.

Dalili zake zikoje?

  • Homa
  • Uchovu na viungo kuuma
  • Maumivu ya kichwa
  • Kikohozi
  • Kupumua kwa shida
  • Maumivu ya kifua
  • Petechial rash

Vipimo vya infective endocarditis

  • Blood culture and sensitivity - kuotesha damu kuangalia ni vimelea gani vilivyohusika, na dawa gani inaweza kuua vimelea husika
  • Complete blood count - kuangalia wingi wa damu, wingi wa chembe nyeupe ambayo ni kiashiria cha maambukizi
  • Echocardiogram - ultrasound ya moyo kuonyesha kuta za ndani za moyo na valve na ufanyaji    kazi wa moyo, na kama kuna uoto-vegetations
  • CT scan ya ubongo (Brain CT - scan) hasa kwa wale wanaoonesha dalili za matatizo ya mishipa ya fahamu kuangalia kama vimelea au uoto umepelekwa na damu kwenye mishipa ya damu ya ubongo
    Kipimo cha mkojo - kuangalia kama kuna protini au chembe chembe nyekundu za damu kwenye hadubini

Matibabu

Baada ya seti tatu hadi tano za damu kuchukuliwa, ni muhimu kuanza na Antibaotiki (Nafcillin + Gentamycin) au (Vancomycin +Gentamycin) au Levofloxacillin ndani ya saa moja hadi saa moja na nusu na kuendelea na antibaotiki husika baada ya majibu ya damu. Na inabidi kutumia dozi kubwa ya antibaotiki kwa kipindi cha wiki sita.
Dawa ya Paracetamol kwa ajili ya kushusha homa na kupunguza maumivu.
Huduma ya uuguzi kwa karibu zaidi

Ni viashiria vipi husababisha mgonjwa afanyiwe upasuaji?

  • Moyo kushindwa kufanya kazi na kutotibika na dawa kirahisi
  • Maambukizi ya Fangasi (histoplasma capsulatum) katika kuta za ndani za moyo na valve
  • Maambukizi kuwa makali na hali ya mgonjwa kuendelea kuzorota baada masaa 72 ya kutumia antibaotiki
  • Kupasuka kwa aneurysm ya Sinus ya Valsalva
  • Matatizo katika mtiririko wa mfumo wa umeme kwenye moyo unaosababishwa na kuwepo kwa usaha katika mirija ya bawabu za moyo
  • Maambukizi yanayotokana na kugusana kwa kuta za valvu za anterior mitral leaflet kwa wagonjwa wenye infective endocarditis kwenye valvu ya aorta (aortic valve)

Jinsi ya kuzia maambukizi

  • Maelekezo ya kuzuia maambukizi ya kuta za ndani za moyo na valve kutoka chama cha madaktari wa moyo cha marekani kwa vimelea vinavyoweza kuuliwa na antibaotiki
  • Kuua vimelea chochote kilichopo kwenye damu kabla hakijafika kwenye valve
  • Zuia kimelea kisishikamane na valve au kusababisha damu kuganda na kutenegeneza kitu kinachoitwa kitaalamu - thrombus
  • Kuteketeza vimelea au kimelea chochote kilichojishikiza katika damu iliyoganda na kutengeneza -thrombus

Ni vyema kujikinga kwa kutumia antibaotiki hasa kwa wafuatao

  • Wenye valve za bandia
  • Waliougua tatizo hili awali
  • Waliofanyiwa upasuaji wa kuwekewa moyo mpya
  • Wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo
  • Waliotoa jino
  • Upasuaji wowote katika mfumo wa upumuaji
  • Upasuaji wowote unahusu maambukizi katika ngozi, misuli au mifupa (incision and drainage of an abscess)

     
Imesomwa mara 9179 Imehaririwa Jumatatu, 15 Mai 2017 11:55
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana