Image

Tundu Katika Kuta za Chini za Moyo (Ventricular Septal Defect)

Makala ya leo ni muendelezo wa magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, na ugonjwa wa leo hujulikana kama Tundu katika moyo, au Tundu katika kuta za ventrikali za moyo, ni ugonjwa ambao hutokea mara nyingi zaidi.

Watoto wenye tundu dogo katika moyo, huweza kukua bila matatizo yoyote, wakati wale wenye tundu kubwa huanza kuonesha dalili mapema

Vifuatavyo ni vihatarishi ambavyo vinaweza kupelekea kupata tundu katika kuta za chini za moyo

  • Maambukizi ya Rubella katika kipindi cha ujauzito
  • Ugonjwa wa kisukari ambao haujadhibitiwa kwa mama mjamzito
  • Matumizi ya pombe au madawa ya kulevya na baadhi ya dawa za hospitali katika kipindi cha ujauzito

Dalili

  • Rangi ya ngozi, midomo na kucha hubadilika na kuwa bluu
  • Kunyonya au kula kwa shida sana, na ukuaji wa shida
  • Kupumua kwa shida
  • Kuchoka haraka
  • Kujaa miguu na kuvimba tumbo
  • Mapigo ya moyo ya haraka
  • Kwa mtaalamu anaweza kusikia ishara ya ongezeko la sauti ya ziada ya mapigo ya moyo ya mtoto hali ambayo wataalamu huiita holosystolic murmur kwa kutumia kifaa kitaalamu stethoscope

Tundu kwenye kuta za chini za moyo

Madhara ambayo yanaweza kutokana na Tundu katika kuta za chini za moyo

  • Eisenmenger syndrome: Ni hali inayotokea wakati shanti ya damu kutoka kushoto kwenda kulia inayotokana na tundu katika kuta za moyo huongeza mtiririko wa damu katika mishipa ya kwenye mapafu na kusababisha shinikizo la damu katika mapafu. Hali hii husababisha kuongezeka kwa shinikizo katika upande wa kulia wa moyo, na kusababisha kubadilika kwa shanti kutoka kulia kwenda kushoto. Matokeo yake ni kuwa damu isiyo na oksijeni ambayo ilitakiwa kwenda kwenye mapafu kwa ajili ya kusafishwa, huchanganyika na damu yenye oksijeni iliyoko upande wa kushoto na kusambaa mwilini.
  • Kiharusi
  • Maambukizi katika kuta za ndani za moyo (endocarditis)
  • Moyo kushindwa kufanya kazi vizuri

Ujauzito na Tundu katika kuta za chini za moyo

Kwa akina mama ambao wamezaliwa na tatizo hili, ambao walitibiwa bila madhara yoyote wanaweza kushika ujauzito bila kupata madhara yoyote kipindi cha ujauzito. Isipokuwa, wale ambao hawakutibiwa au ambao wameshapata madhara, hushauriwa kutoshika ujauzito kwa sababu ya hatari zinazoweza kutokea kipindi cha ujauzito.

Vilevile kwa akina mama waliozaliwa na tatizo hili, uwezekano wa watoto wao kuzaliwa na tatizo hili huwa mkubwa. Kwa mujibu wa taarifa za taasisi ya moyo ya Marekani hatari ya kupata tatizo hili kwa mtoto huongezeka kwa kati ya asilimia 2 hadi 20 iwapo atazaliwa na mama mwenye ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao.

Vipimo

  • X-ray ya Kifua
  • ECG
  • Echocardiogram
  • Cardiac catheterization
  • Pulse Oximetry

Matibabu

  • Wengi wa wagonjwa wa tatizo hili huwa hawahitaji matibabu ya aina yeyote ile kwa vile tatizo hili hujirekebisha katika miaka ya mwanzo ya maisha yao. Hata hivyo kwa wale ambao watahitaji matibabu, hutibiwa kwa tiba au upasuaji kutegemea na ukubwa wa tatizo lenyewe.
  • Tiba huhusisha dawa zifuatazo:
    • ACEI’s ambazo hupunguza kazi ya moyo
    • Cardiac glycosides ambayo huongeza nguvu ya mapigo ya moyo
    • Diuretics ambazo pia hupunguza kazi ya moyo kwa kupunguza maji mwilini
  • Utaratibu wa kuziba tundu umegawanyika katika sehemu mbili, na hufanyika iwapo tundu ni kubwa sana, au tundu halikujirekebisha lenyewe wakati mtoto anapokua, au dawa alizopewa mgonjwa hazikusaidia.
    • Upasuaji - ambapo kifua hufunguliwa kuziba tundu
    • Catheter - ambapo mrija hupitishwa katika mshipa wa damu kufikia sehemu tatizo lilipo kwenye moyo na kuliziba kwa kutumia kifaa maalumu. Katika njia hii, huwa hakuna haja ya kufanya upasuaji wa kufungua kifua cha mgonjwa.
Imesomwa mara 7929 Imehaririwa Ijumaa, 22 Machi 2019 08:15
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.