Tatizo la kiakili la kujihisi mnene na kupoteza hamu ya kula au Anorexia nervosa ni tatizo linawaathiri watu wengi na kuwafanya kupoteza uzito zaidi ya ule unaokubalika kulingana na umri na urefu wa muhusika.
Watu wenye tatizo hili wana hali ya kuwa na hofu isiyo kifani ya kuongezeka uzito hata kama, kiukweli, wana uzito mdogo (wamekonda) kuliko kawaida. Wanaweza kujinyima au kupunguza kula makusudi (dieting), kufanya mazoezi ya kupunguza uzito kuliko kawaida au hata kufanya njia nyingine zozote ilimradi wapungue uzito.
Chanzo na vihatarishi vya tatizo hili
Chanzo halisi cha tatizo hili bado hakifahamiki rasmi. Hata hivyo, mambo kadhaa yanahusishwa na kutokea kwake. Mambo hayo yanajumuisha sababu za kinasaba (genetic factors) na vichocheo mwili (hormones). Aidha masuala ya kijamii yenye kuchochea wana jamii kama vile baadhi ya wasichana kupenda maumbo madogo (vimodo) nayo pia yanahusishwa.
Kipindi cha nyuma, masuala kama matatizo katika familia yalikuwa yakihusishwa na uwepo wa tatizo hili pamoja na matatizo mengine yanahusiana na ulaji wa muhusika ingawa kwa sasa uhusiano wake unaonekana kuwa si wa nguvu sana.
Vihatarishi vya anorexia nervosa vinajumuisha
- Kuwa na tabia ya kupenda kuwa sahihi (perfect) au kupenda kutilia mkazo kwenye taratibu fulafulani katika maisha ambazo wakati mwingine zinaonekana ndogo na zisizo na ulazima sana. Watu wenye kutaka vitu vifanyike kwa usahihi kabisa na ambao hawapo tayari kuruhusu makosa madogo madogo ya kibinadamu katika maisha wapo katika hatari ya kupata tatizo hili.
- Kuwa na hofu iliyopitiliza, au kutilia mkazo sana kuliko kawaida kuhusu uzito au muonekano wa umbo lako la mwili.
- Kuwa na matatizo ya ulaji kipindi cha uchanga au utotoni.
- Baadhi ya mila na desturi za jamii kuhusu afya na mambo urembo. Kwa mfano jamii inayoamini urembo wa msichana huongezeka anapokuwa mwembamba ina hatari ya kuzalisha wagonjwa wengi wa tatizo hili kuliko ile inayoamini tofauti
- Kuwa na picha hasi juu ya umbo lako kama vile kujiona kuwa hupendezi na wala huna mvuto
- Kuwa na tatizo la mhemko wakati wa utoto
Kundi gani hupatwa na tatizo hili zaidi?
Anorexia nervosa kwa kawaida huanza kipindi cha utoto kwenye miaka kati ya 10 mpaka 19 (teens) au miaka ya mwanzo ya ujana (miaka ya mwanzo ya ishirini). Kwa kawaida tatizo hili ni maarufu zaidi kwa wasichana/wanawake kuliko wavulana/wanaume. Wanawake wazungu hasa walio na elimu nzuri na wenye daraja la maisha ya kati au juu na wale wanaotoka katika familia bora wanaongoza kwa kupatwa na tatizo hili ukilinganisha na wanawake weusi au wa jamii za tabaka la chini kielimu na kimaisha.
Dalili zake ni zipi?
Ili kuweza kumtambua mtu mwenye tatizo hili, mgonjwa huwa na dalili zifuatazo:
- Hofu isiyo kifani ya kuogopa kuongezeka uzito au kuwa mnene, hata kama atakuwa amekonda
- Huwa na tabia ya kutotaka kuwa na uzito unaokubalika kuwa wa kawaida kulingana na urefu na umri wake (yaani huwa na uzito ulio 15% au zaidi chini ya uzito wa kawaida
- Huwa na hisia hasi juu ya mwili wake, daima hujihisi vibaya sana juu ya umbo lake na uzito wake, na hukataa kukubali kuwa amekonda na siku zote huamini kuwa yeye ni mnene na ameongezeka uzito
- Kwa wanawake, hukosa hedhi kwa kipindi cha miezi mitatu au zaidi (bila kuwa mjamzito)
Watu wenye tatizo hili huwa na tabia ya kujinyima kupita kiasi kula chakula, au hula na kisha hukimbilia chooni kujitapisha au kunywa dawa za kujilazimisha kuharisha. Tabia nyingine za tatizo hili ni pamoja na:
- Huwa na tabia ya kukata chakula katika vipande vidogo vidogo au kuchezea chezea chakula katika sahani badala ya kula
- Hupenda kufanya mazoezi ya mwili kila wakati, hata kama hali ya hewa si nzuri na hairuhusu kufanya hivyo, au hata kama wana majeraha, au ratiba zao haziwaruhusu
- Huwa na tabia ya kukimbilia chooni au bafuni mara baada ya kumaliza kula
- Hukataa kula mbele ya watu wengine hususani wageni
- Hupenda kutumia dawa za kuwafanya wakojoe sana (diuretics), au za kuwafanya kuharisha, kutapika au za kupunguza hamu ya kula
Dalili nyingine za tatizo hili ni
- Kuwa na ngozi kavu ya njano iliyokakamaa na yenye vinyweleo dhaifu kuliko kawaida
- Huwa na tabia za kuchanganyikiwa na uwezo mdogo wa kufikiri pamoja na ukosefu wa kumbukumbu au udhaifu katika kufanya maamuzi
- Kuwa na msongo wa mawazo
- Midomo huwa mikavu
- Hujihisi baridi kuliko kawaida (mara nyingi hupenda kuvaa nguo nyingi ili kuongeza joto mwilini)
- Mifupa huwa mifupi
- Hupungua uzito na kukonda sana (kwa sababu ya kupoteza kiasi kikubwa cha misuli na mfuta mwili)
Vipimo
Ili kufikia hitimisho la anorexia nervosa, ni vema kuchunguza na kuwa na hakika ya kutokuwepo kwa vyanzo vingine vya kupungua uzito na kupoteza misuli ya mwili kwa kufanya vipimo kadhaa. Pia vipimo hivi husaidia kufahamu athari iliyoletwa na kukonda kupita kiasi.
Baadhi ya magonjwa ambayo yana dalili zinazofanana na tatizo hili ni pamoja na ugonjwa wa Tezi za Adrenal (Addison's disease), ugonjwa wa utumbo mkubwa (celiac disease), na magonjwa ya mzio katika utumbo mkubwa (Inflammatory bowel diseases).Baadhi ya vipimo hivi inabidi virudiwe rudiwe kwa ajili ya kuratibu maendeleo ya mgonjwa.
Vipimo vya tatizo vinajumuisha
- Kipimo cha damu: Damu inaweza kusaidia kuchunguza vitu kama FBP (CBC), kiwango cha protein ya albumin, kiwango cha madini (electrolytes), na jumla ya protein (total protein)
- X ray ya mifupa husaidia kuchunguza uwepo wa mifupa membamba ambayo huashiria kiasi cha kulika kwa mifupa (osteoporosis). Aidha kipimo cha bone density test chaweza pia kusaidia kazi hii
- Vipimo vya utendaji kazi moyo (Electrocardiogram ECG au EKG na Echo)
- Kipimo cha utendaji kazi wa mafigo (renal function tests)
- Kipimo cha utendaji kazi wa Ini (Liver function tests)
- Vipimo vya utendaji kazi wa tezi ya thyroid (thyroid function tests)
- Kipimo cha mkojo (Urinalysis)
Matibabu
Changamoto kubwa sana katika matibabu ya tatizo hili ni kwanza kumfanya mgonjwa atambue na akubali kuwa ana tatizo. Wagonjwa wote wa anorexia nervosa hukataa kukubali kuwa wao ni wagonjwa. Hujiona kuwa wapo wazima na hata uzito walio nao ama ni mkubwa au wa kawaida kwao. Wengi wao pia hawakubali kama wana matatizo katika ulaji wao. Wagonjwa wa tatizo hili huanza matibabu pale tu hali zao zinapobadilika na kuwa mbaya sana, mahututi pengine karibu na kufa.
Malengo makuu katika matibabu ya wagonjwa wa tatizo hili ni kuhakisha wanarudisha uzito wao na kuwa na uzito wa kawaida unaokubalika na pia kuwarudishia hali ya kawaida ya ulaji.
Ongezeko la kati ya gram 500 mpaka kilo moja na nusu kwa wiki linakubalika kuwa ni ongezeko sahihi na salama kwa mgonjwa.
Ili kumuwezesha mgonjwa arudishe uzito wake katika hali yake ya kawaida pamoja na kuimarisha tabia yake ya ulaji, njia kadhaa zinaweza kutumika. Miongoni mwa njia hizo ni pamoja na:
- Kumsaidia kuongeza kujichanganya na jamii inayomzunguka
- Kumfanya apunguze mazoezi ya mwili au shughuli zozote zitakazoufanya mwili wake kupungua uzito zaidi
- Kuwa na ratiba maalum ya kula na kuhakikisha inafuatwa
Wagonjwa wengi huanza matibabu kwa kulazwa hospitali kwa muda mfupi kisha kuendelea na matibabu nyumbani.
Hata hivyo mgonjwa anaweza kulazwa hospitali na kuhitaji matibabu ya muda mrefu iwapo
- Amepoteza uzito kupitiliza (kwa maana nyingine ana uzito chini ya 70% ya uzito unaokubalika kulingana na umri na urefu wake). Kwa wale waliopata utapiamlo unaotishia maisha yao, mgonjwa anaweza kuhitaji kulishwa kwa kutumia mirija ya mishipa ya damu (I.V lines) au kwa kutumia mirija maalum yanayoingia hadi tumboni (stomach tube)
- Anaendelea kupoteza uzito ilihali anaendelea na matibabu
- Atapata magonjwa yaliyoletwa na kutokula kama vile matatizo ya moyo, kuchanganyikiwa au kuwa na kiwango kidogo cha madini ya potasium mwilini
- Ana msongo mkali wa mawazo au anafikiria kutaka kujiua
Nani anayehusika na matibabu wagonjwa wa tatizo hili?
Watoa huduma za afya wanaohusika na matibabu na huduma za wagonjwa wa tatizo la aina hii ni pamoja na:
- Wauguzi
- Madaktari
- Wataalamu wa lishe (Nutritionists au dietitians)
- Wataalamu wa afya ya akili
- Jamii na familia ya muhusika
Jamii na familia ya mgonjwa lazima itambue kuwa matibabu ya tatizo hili si jambo rahisi hivyo wanapaswa kufanya juhudi za makusudi kumsaidia mgonjwa. Wakati mwingine, aina kadhaa za matibabu zinaweza kuhitaji kutumika kabla mgonjwa hajapata nafuu inayotarajiwa.
Baadhi ya wagonjwa wanaweza kuamua kuacha matibabu iwapo hawatapewa maelezo ya kutosha wakidhani kuwa tiba ya dawa na chakula pekee ndiyo itakayowaponya.
Ukiacha tiba zilizotajwa hapo juu, wakati mwingine ni vizuri mgonjwa akakutanishwa na wagonjwa wenzake wenye tatizo kama lake ili wapate kusaidiana na kuelimishana juu ya tatizo linalowakabili. Hata hivyo usimamizi wa jambo hili ni muhimu kuepuka hali ya kupotoshana miongoni mwa wagonjwa.
Wagonjwa wenye matatizo ya akili na msongo wa mawazo wanaweza kupewa dawa kulingana na tatizo linalomkabili. Dawa hizi zinajumuisha antipsychotics na zile zenye kuondoa msongo wa mawazo na kuimarisha mood ya mgonjwa kama vile (antidepressants) ambazo pia husaidia sana kumfanya mgonjwa awe na hamu ya kula. Dawa hizo pia husaidia kuondoa mhemko.
Hata hivyo haishauriwi kutumia dawa hizi bila maelekezo ya daktari
Matarajio
Anorexia nervosa ni tatizo la hatari ambalo linaweza kusababisha kifo. Inakadiriwa kuwa karibu 10% ya wanaopata tatizo hili hufa ama hujiua. Mpango maalum wa matibabu unaweza kusaidia kuwarejesha wagonjwa katika hali zao za kawaida na kuendelea na maisha yao ya kila siku, ingawa ni jambo la kawaida kwa tatizo hili kujirudia siku za mbele.
Wanawake ambao hupatwa na tatizo hili katika umri mdogo wana nafasi kubwa ya kupona kabisa. Hata hivyo watu wengi waliopatwa na tatizo hili hupendelea kuwa na maumbo madogo hata baada ya matibabu na wengi wao huendelea kutilia mkazo katika aina ya vyakula walavyo.
Suala la uthibiti wa uzito kwa wagonjwa hawa linaweza kuwa gumu, hali ambayo inaweza kulazimu kuwepo kwa mipango ya muda mrefu ya matibabu ili kumfanya mgonjwa aweze kuwa na uzito unaokubalika.
Madhara ya Anorexia Nervosa
Madhara ya tatizo hili yanaweza kuwa ya hatari mpaka kusababisha kifo. Katika hali kama hiyo, mgonjwa analazimika kulazwa hospitali. Madhara ni pamoja na:
- Kuwa na hali ya kuvimba mwili kwa sababu ya upungufu wa protein mwilini, matatizo ya moyo, ini au hata ya mafigo
- Kuwa na mifupa dhaifu
- Kuwa na mlingano usio sawa wa madini mwilini (electrolyte imbalance hususani kiwango kidogo cha potassium)
- Mapigo ya hatari ya moyo yasiyo sawa (severe heart rhythms)
- Kupungua kwa chembe nyeupe za damu hali inayoongeza uwezekano wa mwili kushambuliwa na maradhi kwa sababu ya upungufu wa kinga ya mwili
- Mwili kuishiwa maji
- Utapiamlo mkali
- Degedege kwa sababu ya upungufu wa maji mwilini unaotokana na kujilazimisha kuharisha na kutapika
- Matatizo katika tezi ya thyroid hali inayosababisha kushindwa kuhimili baridi na kukosa choo
- Kuoza kwa meno
Jambo la kuzingatia
Zungumzia na daktari iwapo una ndugu au mtu wa karibu ambaye
- Ana hisia zisizo za kawaida kuhusu uzito wake
- Anafanya mazoezi kupita kiasi
- Anajiwekea kikomo kisicho cha kawaida katika kiwango cha ulaji wake
- Ana uzito wa chini kuliko kawaida
Kinga
Inawezekana sana kukinga kutokea kwa tatizo hili kwa baadhi ya watu. Njia za kufanya ni pamoja na kuhimiza watu kuwa na mawazo na tabia chanya juu ya uzito na ulaji wao. Hali kadhalika kuzungumzia tatizo hili kwa njia ya makundi pia husaidia kuepusha kutokea kwa tatizo.
Dr Fabian P. Mghanga
Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea
Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.