Kipindi cha ujauzito ni wakati muhimu sana kwa afya ya mama na mtoto. Ili kuhakikisha mama anajifungua salama na mtoto anazaliwa akiwa na afyanjema, ni muhimu kuhudhuria kliniki mara kwa mara kama inavyoshauriwa na Watoa huduma. Kampeni nyingi zimeanzishwa ili kuhamasisha akina mama wajawazito wanaanza kuhudhuria kliniki mapema, pia kwenye App kama TanzMED kuna feature maalumu ambayo inakuongoza na kukukumbusha kuhudhuria kliniki, lakini je, unajua kwa umuhimu wa kuhudhuria kliniki ya ujauito?
Kuzuia Matatizo ya Afya kwa Mama na Mtoto Aliye Tumboni
Wakati wa kliniki, mama mjamzito hupatiwa dawa, vipimo na chanjo mbalimbali ambazo husaidia kumlinda yeye na mtoto wake kutokana na magonjwa hatari. Baadhi ya dawa hizi ni:
A: Dawa za Kuongeza Damu (FEFO)
Dawa za kuongeza damu ni muhimu sana kwa mama mjamzito. Fefo ina madini ya chuma na folic acid ambayo husaidia kuzuia upungufu wa damu unaosababishwa na matumizi ya ziada wakati wa ujauzito. Madini ya chuma humlinda mama dhidi ya upungufu wa damu, na folic acid husaidia ukuaji wa mtoto, hasa katika wiki za mwanzoni, kabla ya kuunda uti wa mgongo na mfumo wa mishipa ya fahamu. Matumizi ya folic acid pia yanasaidia kuzuia kasoro kama mgongo wazi na tatizo la kichwa kikubwa. Unzaweza kusoma kuhusu vichwa vikubwa hapa Fahamu ukweli, hatari na matibabu ya Vichwa vikubwa
FIG 1: Mtoto mwenye kichwa kikubwa FIG 2: Mtoto mwenye mgongo wazi
B: Dawa za Kuzuia Malaria
Malaria ni hatari sana kwa mama mjamzito kwani vimelea vya malaria vinaweza kuathiri kondo la nyuma na kusababisha matatizo makubwa kwa mtoto na mama, ikiwemo kifo. Mama wajawazito hupewa dawa za kuzuia malaria pamoja na vyandarua vilivyowekwa dawa.
C: Dawa za Minyoo
Minyoo inaweza kudhoofisha hali ya afya ya mama kwa kunyonya virutubisho muhimu vinavyotakiwa kwa ukuaji wa mtoto. Pia, minyoo inaweza kusababisha upungufu wa damu, hivyo ni muhimu kwa mama wajawazito kupatiwa dawa za kuzuia minyoo.
D: Chanjo ya Tetenasi
Mama wajawazito pia hupewa chanjo ya tetenasi ambayo husaidia kumkinga dhidi ya ugonjwa huo hatari ambao unaweza kuathiri afya ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Kutambua Magonjwa ya Mama na Mtoto Mapema
Mahudhurio ya kliniki pia husaidia kugundua matatizo au magonjwa ambayo mama anaweza kuwa nayo kabla au wakati wa ujauzito. Magonjwa kama vile shinikizo la damu, kisukari, upungufu wa damu, magonjwa ya zinaa, na virusi vya ukimwi vinaweza kuathiri mama na mtoto. Kwa kugundua matatizo haya mapema, mama anaweza kupatiwa matibabu sahihi ili kuepusha athari mbaya kwa mtoto kama vile ulemavu wa akili, kifafa cha mimba, au kifo.
Elimu ya Afya na Ujauzito
Kliniki hutoa nafasi kwa mama mjamzito (na wenza wao) kupata elimu kuhusu jinsi ya kutunza ujauzito. Elimu hii inahusisha lishe bora, tabia hatarishi zinazopaswa kuepukwa, na dalili za hatari zinazohitaji matibabu ya haraka. Kupata elimu hii ni muhimu ili kuhakikisha mama anajua namna ya kujilinda yeye na mtoto wake wakati wote wa ujauzito.
Kujua Maendeleo ya Ujauzito
Kupitia mahudhurio ya kliniki, mama anaweza kufuatilia maendeleo ya mtoto aliye tumboni. Hii inahusisha mambo kama kubaini umri wa ujauzito, kutambua kama mimba ipo katika nafasi sahihi (ili kugundua mimba zilizotunga nje ya mji wa mimba), kuangalia kiasi cha maji ya uzazi, na kuchunguza jinsi mtoto alivyolala ili kupanga njia sahihi ya kujifungua.
Elimu ya Uzazi wa Mpango
Baada ya kujifungua, ni muhimu kwa mama kufahamu mbinu za uzazi wa mpango ili kuhakikisha mwili wake unapata muda wa kupona vizuri kabla ya kupata ujauzito mwingine. Hii inasaidia kulinda afya ya mama na mtoto wake ajaye.
Hitimisho
Mwanamke anatakiwa kuanza mahudurio ya kliniki hata kabla hajabeba ujauzito. Lakini hata kama ukigundua tayari umeshabeba ujauzito ni muhimu kunza mahudhurio ya kliniki mapema. Jilinde na umlinde mwanao kwa kuhakikisha unahudhuria kliniki kila mwezi mara tu baada ya kujua umebebe ujauzito!! Pia, unaweza kutumia App ya TanzMED kufuatilia ujauzito wako.