Image

Tatizo la Kuharisha kwa Watoto

Utangulizi

Kuharisha kwa watoto ni tatizo linaloshika nafasi ya pili duniani kwa kusababisha vifo miongoni mwa watoto chini ya miaka mitano. Inakadiriwa kwamba kwa kila watoto 5 wanaofariki , 1 hufa kwa sababu ya kuharisha. Watoto milioni 1.5 kila mwaka hufa kutokana na kuharisha.

Leo hii, inakadiriwa asilimia 39 tu ya watoto wanaoharisha katika nchi zinazoendelea hupata matibabu sahihi.Hata hivyo, mwenendo wa kitakwimu unaonesha kwamba kumekuwa na mafanikio kidogo tangu mwaka 2000.

Kuharisha huelezwa kuwa ni upotevu wa maji na madini muhimu kwa mwili wa binadamu (electrolytes) kupitia kinyesi na kupelekea upungufu wa maji mwilini. Katika hali ya kawaida, watoto wachanga hutoa kiasi cha gramu 5 za kinyesi kwa kila kilo ya mtoto (5g/ kg) kwa siku, wakati mtu mzima hutoa wastani wa gramu 200 kwa siku. 

Sababu za Kuharisha kwa watoto

Kuharisha kunaweza kusababishwa na aina mbalimbali za vimelea ingawa pia kunaweza kusitokane na maambukizi ya vimelea (non-infectious causes). Vimelea vinavyosababisha kuharisha ni

  • Virusi: Virusi vinaongoza katika kusababisha tatizo la kuharisha kwa watoto katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
  • Bakteria: Wanasababisha kuharisha kwa asilimia chache 2-10%. Kuharisha kunakosababishwa na bacteria husababisha upotevu mdogo wa maji ukilinganishwa na virusi. Mfano wa bakteria wanaoweza kusababisha tatizo hili ni Campylobacter, Salmonella, Shigella, na Escherichia coli
  • Parasite pia husababisha kuhara, lakini aina hii ya kuhara huwa ni sugu zaidi (chronic diarrhea) kwa ujumla na mara nyingi haiambatani na homa, kutapika, na upungufu wa maji mwilini. Giardia lamblia na Cryptosporidium parvum ni moja ya aina hii za parasire wanaosababisha kuhara.

Sababu ambazo hazihusiani na maambukizi ya vimelea yaani noninfectious causes ni pamoja na kula chakula kilichochanganywa na sumu au kumeza sumu, matatizo katika sehemu ya utumbo mwembamba na mnene, na matatizo ya usagaji chakula (metabolic abnormalities).

Kwa vile sababu kuu ya kuharisha ni kutokana na virusi, tutazungumzia aina kuu ya virusi wanaosababisha kuhara.

Kuna aina takribani 4 wanaojulikana ambavyo ni Rotavirus, Adenovirus, astrovirus na norovirus. Kati ya hivi jamii ya Rotavirus ndio wanaongoza duniani kote katika kueneza na kusababisha kuharisha kwa watoto wachanga na wadogo . Katika nchi zinazoendelea, Rotavirus ndiyo chanzo kikuu cha vifo vinavyotokana na kuhara miongoni mwa watoto chini ya umri wa miaka 5.

Rotavirus huathiri wavulana na wasichana kwa uwiano sawa. Hatari zaidi ni kwa wale walio na uzito wa kuzaliwa chini ya gramu 1500 vilevile uzito kati ya gramu 1500-2499. Ukali wa ugonjwa ni mkubwa zaidi kwa watoto wenye umri wa miezi 3-24. Watoto wachanga chini ya miezi 3 wanapata sehemu ya kinga (antibodies) kutoka kwa mama anayenyonyesha na vilevile kinga mtoto aipatayo kupitia kondo la nyuma (placenta) kabla ya kuzaliwa. Kwa maana hiyo basi shambulizi la awali baada ya miezi 3 lina uwezekano wa kusababisha ugonjwa mkali zaidi.

Jamii hii ya Virusi wana uwezo wa kuenea kwa urahisi sana toka kwa mtoto mmoja kwenda kwa mwingine. Kimsingi wanaenea kwa njia ya kinyesi. Ni rahisi mtoto kupata uambukizi wa rotavirus iwapo atakula chembechembe za kinyesi zenye vimelea hivi. Mtu mwenye vimelea hivi anaweza kuambukiza mtu mwingine hata kabla ya dalili hazijaanza kujionesha kwake au hata siku kadhaa baada ya dalili kujionesha.

Mtu aliyeambukizwa anaweza kutoa idadi kubwa ya vimelea hivi kiasi cha virion 1-10 kwa kila mililita ya kinyesi. Ili kuambukizwa kinahitajika kiasi kidogo tu cha hawa vimelea, takribani miligramu 0.000001. Hivyo ni rahisi kuambukizwa kwa kugusana au kwa kushika au kutumia vifaa vyenye maambukizi ya rotavirus. Aidha, rotavirus wamegunduliwa kuwepo katika majimaji ya kwenye kinywa na koo (oropharngeal secretions), ingawa bado haijathibitishwa kama kuna uwezekano wa maambukizi kwa njia ya hewa.

Muonekano wa mgonjwa

Watoto wanaohara kwa sababu ya rotavirusi huwa na dalili kuu tatu ambazo ni homa, kutapika na kuharisha. Kawaida choo kinakuwa cha majimaji sana. Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 63 ya watoto wanaolazwa hospitalini kwa tatizo hili wanaonyesha dalili zote 3, asilimia 25 wanakuwa na dalili 2 tu.

Wakati mwingine kuharisha kunaweza kujitokeza baadaye baada ya kutapika au homa. Joto la mtoto huwa si kali sana ingawa baadhi ya watoto wanaweza kuwa na joto kali linalozidi nyuzi joto 39 za sentigradi.

Kutapika kunaweza kusiwe zaidi ya masaa 24. Vilevile wanaweza kuwa na kuchefuchefu, maumivu ya tumbo (abdominal cramping), kulia pasipo kutulia akibembelezwa (irritability) na uchovu.

Vifo husababishwa na upungufu wa maji mwilini. Upungufu wa maji waweza kuambatana na upungufu na kukosekana uwiano wa madini mwilini (electrolyte imbalance). Aidha kunaweza kusababisha madhara katika figo (ischemic injury to the kidneys) na katika mfumo wa neva (central nervous system) na kusababisha na mtoto kupoteza fahamu (shock).

Inashauriwa kuchunguza kiasi cha maji kilichopotea. Iwapo uzito wa mtoto utakuwa umepungua kwa zaidi ya asilimia 10, mtoto anaweza kuwa na dalili kama

  • kupoteza fahamu
  • kuwa na mapigo ya moyo ya kasi
  • kushindwa kula na kunywa
  • kuwa na macho yaliyolegea kulegea na kuingia ndani sana (severe sunken eyes)
  • kushindwa kutoa mkojo kabisa
  • kutotoa machozi na mdomo kuwa mkavu sana.

Upungufu wa kati ya asilimia 5-10 ya maji mwilini, husababisha

  • macho ya mtoto huingia ndani (sunken eyes)
  • ngozi kurudi taratibu pindi inapovutwa (loss of skin turgor)
  • mapigo ya moyo kuwa kasi
  • kuwa na ubonyeo katika sehemu ya mbele ya kichwa (depressed anterior frontanele)
  • uchovu
  • kiu na kunywa maji kwa haraka
  • mtoto kutoa machozi kidogo sana pindi anapolia
  • midomo kuwa mikavu na
  • kupumua kwa haraka kuliko kawaida

Chini ya asilimia 5 mtoto huwa na

  • kiu
  • ngozi inayorudi taratibu pindi ikivutwa
  • macho yanaweza kuingia ndani na
  • uchovu.

Unapoona dalili hizi wakati mtoto wako anaharisha unapaswa kumpeleka haraka kituo cha afya ili kupata ushauri wa wataalamu wa afya.

Uchunguzi 

  • Kipimo cha choo: hujumuisha pia uchunguzi wa vimelea.
  • Kipimo cha antigeni cha Rotavirusi (Rotavirus antigen tests) ingawa asilimia 50 ya majibu yanaweza kuwa si sahihi (false-negative) hasa pale panapokuwa na damu kwenye choo.
  • Kupima kiwango cha sukari mwilini (blood glucose level)
  • Chembechembe nyeupe za damu kutambua maambukizi ya bakteria.
  • Kupimo cha figo (Renal function Test and electrolytes)
  • Vipimo vingine kutegemea na hali ya mgonjwa.

Matibabu

Ingawa yawezekana mtoto kupona bila hata matibabu lakini ni jambo muhimu kuchunguza madhara yanayoweza kusababishwa na upungufu wa maji mwilini. Ieleweke kuwa watoto wapo katika hatari kubwa zaidi ya ya kupungukiwa na maji mwilini kutokana na kuharisha, hivyo basi msingi wa matibabu ni kurudisha kiasi cha maji kilichopotea.

Hali kadhalika, matumizi ya madini ya zinc yamehusishwa na kupungua kwa makali ya ugonjwa na kupunguza muda wa kuharisha.

ORS ambayo ni mchanganyiko wenye uwiano mzuri wa chumvi na sukari ni aina ya tiba inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya matibabu. Uwiano uliopo katika ORS huwezesha utumbo wa mtoto kufyonza vizuri maji na madini mengine.

Matibabu ya kuharisha kwa watoto yanaweza kugawanywa katika awamu kuu mbili

  • Kurudisha maji yaliyopotea (rehydration)
  • Kuendelea kuupa mwili maji kwa ajili ya mahitaji ya kila siku (Maintenance)

Mlezi hushauriwa namna ya kutengeneza mchanganyiko huu ORS kulingana na hali ya mtoto. Kwa mama wanaonyonyesha, wanashauriwa kuendelea kumnyonyesha mtoto mgonjwa huku akimpa mlo wa kawaida wa kila siku. Ikiwezekana, ni vema pia kuendelea kumpa mtoto maji ya ziada. Kama mtoto akitapika, mzazi/mlezi anashauriwa kusubiri kwa angalau dakika 5-10 kabla ya kuendelea tena kumnywesha kidogo kidogo (kwa mfano, kijiko kila baada ya dakika 2-3).

Watoto walio na hali mbaya na wale waliopoteza zaidi ya asilimia 10 hawana budi kupewa maji kwa njia ya mishipa ya damu yaani intravenous fluids.

Kwa vile chanzo kikuu cha kuhara kwa watoto ni maambukizi ya virusi, haishauriwi kutumia antibiotics kama sehemu ya matibabu. Hata hivyo antibiotics zinaweza kutumika tu pale ambapo itathibitika kuwa kuharisha kumesababishwa na bakteria.

Dawa za kuzuia kuharisha kama vile Loperamide hazishauriwi kwavile athari zake ni mbaya zaidi kwa mtoto kuliko faida.

Namna ya kuzuia maambukizi

  • Kuzingatia usafi wa chakula (kupika na kuhifadhi).
  • Kunawa mikono kila baada ya kutoka chooni, kabla ya kushika chakula na wakati wa kula
  • Kuwa makini na watoto wanaoharisha ikiwezekana kuwatenga na wenzao
  • Matumizi ya Chanjo: Usalama wa chanjo ya Rotavirus bado haujathibitishwa rasmi hasa kwa watoto chini ya wiki 6. Aidha chanjo hii imekuwa ikihusishwa na kutokea kwa matatizo katika utumbo mkubwa na mdogo.
Imesomwa mara 31360 Imehaririwa Jumatatu, 05 Novemba 2018 09:32
Dr. Paul J. Mwanyika

Dr. Paul J. Mwanyika ni Daktari  Bingwa waTiba na Uchunguzi wa Magonjwa ya Watoto (Pediatrics).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.