Image

Sababu, dalili na aina za Dege dege kwa watoto (Seizures)

Utangulizi

Degedege ni mojawapo ya matatizo hatari sana kwa watoto na huogopesha sana wazazi na walezi wengi. Katika hili kuna dhana tofauti tofauti zilizojengeka miongoni mwa wanajamii, ambapo baadhi huamini degedege ina uhusiano na mambo ya ushirikina na kwamba huweza kutibiwa kwa njia za namna hiyo.
Wazazi na walezi wenye imani za namna hii hukataa kuwapeleka watoto wao hospitali wakiamini kuwa watakufa iwapo wataachwa wapate matibabu ya hospitali. Dhana nyingine iliyojengeka ni ile ya kuwa degedege ni tatizo linalotokea mara moja tu maishani mwa mtoto kitu ambacho si kweli. Aidha wapo pia baadhi ya wanajamii wanaohusisha degedege na ugonjwa wa Malaria pekee.

Ukweli ni kwamba karibu asilimia 3 ya watoto chini ya miaka 15 hupata degedege, nusu ya hawa hupata degedege linalosababishwa na homa kali. Kwa maana hiyo basi, degedege pia linaweza kumpata mtoto asiye na homa kama kifafa. Inakadiriwa kuwa mtoto 1 kati ya 100 hupata degedege la kifafa.

Degedege ni nini?

Degedege ni dalili inayoonesha mvurugano katika ufanyaji kazi wa seli za ubongo. Kwa kawaida, seli za ubongo ambazo kwa kitaalamu huitwa neurons huwasiliana kwa njia ya mtiririko wa umeme (electrical impulses). Ni mtiririko huu wa mawasiliano ya umeme kati ya seli za ubongo ndiyo unaofanya mwili uweze kufanya kazi ipasavyo. Iwapo basi itatokea kuwepo sababu yeyote ile itakayosababisha mawasiliano kati ya seli za ubongo kutokuwa katika mtiririko sahihi mfano kuwepo msisimko wa mawasiliano, hali hiyo husababisha degedege.

Degedege husababishwa na nini?

Zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha degedege. Moja ya mambo yanayoweza kusababisha degedege ni kuwepo kwa jeraha katika ubongo (brain injury) ambalo linaweza kuwa kwa sababu yeyote ile ikiwemo jeraha analopata mtoto wakati wa kuzaliwa (brain ischemia).

Lakini pia kuna baadhi ya familia ambazo zinakuwa na matatizo ya kimaumbile katika ubongo zinazorithiwa toka kizazi hadi kizazi (mfano kifafa). Familia za namna hii huwa na watoto ambao hupatwa na degedege kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko familia ambazo hazina matatizo haya.

Vilevile degedege inaweza kuhusishwa na hali ya mabadiliko ya muda mfupi katika ubongo kama vile joto kali, matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine, amphetamine, viwango visivyo vya kawaida vya sukari na sodium katika damu (electrolytes imbalance) na uwepo wa uvimbe katika ubongo (brain tumor).

Sababu nyingine zinazoweza kusababisha degedege 

  • saratani ya ubongo,
  • matatizo ya kimaumbile katika ubongo ya kuzaliwa nayo (congenital brain defects),
  • mashambulizi ya vimelea vya bakteria, virusi, fangasi katika ubongo kama vile ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis).

Aidha matatizo katika ini na figo pia yanaweza kusababisha degedege. Pia kuna matatizo ya kimetaboliki (metabolic diseases) kama vile ugonjwa wa kukojoa kiwango kikubwa kuliko kawaida cha aina fulani ya tindikali ya amino ujulikanao kama Phenylketonuria (PKU) hasa kwa watoto chini ya mwaka mmoja.

Aina za Degedege

Degedege la homa (Febrile Seizures)

Hii ni aina ya degedege ambayo hutokea mara nyingi zaidi kwa watoto kuliko aina nyingine za degedege. Kwa ujumla hutibika na kupona kwa urahisi kuliko aina nyingine za degedege. Hata hata hivyo aina hii ya degedege inaweza kuashiria kuwepo kwa tatizo hatari la maambukizi ya bakteria katika mwili (sepsis) au katika ubongo wa mtoto (bacteria meningitis).

Degedege la homa linaweza pia kusababishwa na magonjwa kama malaria, mashambulizi ya vimelea katika njia ya hewa (Respiratory tract infection), uambukizi katika njia ya chakula (Gastroenteritis) na uambukizi katika njia ya mkojo (UTI). Kwa hiyo ni vema kumchunguza kwa kina kila mtoto anayepata degedege la homa ili kufahamu chanzo na kukipatia matibabu muafaka.

Kwa kawaida degedege la homa hutokea kwa watoto wenye umri kati ya miezi 6 mpaka miaka 5, ingawa kundi la watoto walio na umri wa miezi 14 mpaka 18 ndilo linaloongoza kwa kuathirika zaidi. Tafiti bado zinaendelea kujaribu kufahamu uhusiano kati ya homa kali na kutokea kwa degedege ingawa baadhi ya wanasayansi wanahusisha zaidi na sababu za kijenetiki (genetical reasons).

Kuna aina 2 za degedege la homa

  • Degedege la homa rahisi (A simple febrile Seizure) ni aina ya degedege ambalo linaambatana na kupanda ghafla kwa joto la mwili kufikia nyuzi joto 39 za sentigredi au zaidi, linadumu chini ya dakika 15, linahusisha mwili mzima likifuatiwa na kipindi kifupi cha kama kizunguzungu kwa mtoto (drowsiness) na linatokea mara 1 katika kipindi cha masaa 24. Aina hii ya degedege haisababishi jeraha la kudumu katika ubongo na ni asilimia chache huendelea mpaka kufikia hatua ya kuwa tatizo la kifafa.
  • Degedege la homa lisilo rahisi (A complex febrile Seizures) ni aina ya degedege ambalo hudumu zaidi ya dakika 15 au linalohusisha sehemu fulani ya mwili wa mtoto (siyo mwili mzima) na kutokea zaidi ya mara 1 katika kipindi cha masaa 24. Aina hii ina uwezekano mkubwa wa kusababisha kifafa hapo siku za baadaye.

Degedege lisilo na homa (Unprovoked Seizures)

Ni aina ya degedege ambalo haliambatani na homa. Mara nyingi aina hii inaashiria uwepo wa tatizo katika ubongo inayosababisha mtiririko wa mawasiliano kati ya seli za ubongo wakati mwingine kuwa wa kasi kupita kiasi. Degedege la namna hii huwa na tabia ya kujirudia rudia katika takribani nusu ya idadi ya watoto wanaopatwa nalo. Hapa inahitajika kupata historia ya mtoto na familia yake kwa umakini ili kuweza kujua kama kuna historia ya kifafa katika familia/ukoo au tatizo la degedege la homa kabla na matatizo katika seli za neva. Vilevile ni muhimu kupima viwango cha madini mwilini hasa sodium, sukari, au sumu katika damu. Iwapo litatokea mara 2 zaidi ya masaa 24 hapo inaashiria tatizo la kifafa.

Degedege linalotokea upande mmoja wa mwili (Partial Seizures)

Katika hili, sehemu mojawapo ya ubongo huhusika na matokeo yake ni sehemu tu ya mwili inayoonesha dalili za degedege. Aina hii ya degedege hutokea kwa namna mbili tofauti. Mtoto anaweza kupoteza fahamu kwahiyo asijue linalotokea (a complex partial seizure) au degedege linaweza kumpata mtoto pasipo kupoteza fahamu (a simple partial seizure). Wakati mwingine inaweza kukuwia vigumu kutambua aina hii ya degedege (simple partial seizure) kwa sababu kwa kawaida huchukua muda mfupi sana kama sekunde 10 mpaka 20 hivi na wakati mwingine mtoto anaweza akawa na uwezo wa kuongea wakati degedege likiwa linaendelea.

Kwa kawaida degedege la namna hii uhusisha kucheza kwa misuli sehemu za uso, shingo au sehemu fulani za mikono. Mzazi au mlezi anaweza kufikiri labda mtoto anaonesha mojawapo ya sehemu ya kawaida ya michezo ya watoto. Ili kuweza kutofautisha na michezo mingine, ni kwamba degedege likianza mtoto hawezi kulizuia mpaka limalizike hata kama mzazi utamwambia aache kufanya anayofanya wakati kama ni mojawapo ya michezo yake ni rahisi kuzuia.

Degedege linalohusisha mwili mzima (Generalized Seizures)

Hapa sehemu kubwa ya ubongo huathirika na matokeo yake ni mwili wote kuonesha dalili za degedege ikiwemo kupoteza fahamu.Aina hii vilevile inaweza kuelezewa kwa namna mbili yaani

  • degedege potevu (Absence seizure)
  • Generalized Tonic Clonic Seizure.

Degedege potevu (Absence seizure) ni aina ya degedege ambalo ni nadra kutokea kwa mtoto chini ya miaka 5, na mara nyingi linawahusisha sana watoto wa kike. Degedege la namna hii mara nyingi sana hudumu si zaidi ya dakika 1. Uhusisha kupoteza fahamu na kuduwaa pasipo fanya kitu chochote kwa sekunde kadhaa kabla ya mtoto kurudiwa na fahamu na kuendelea na shughuli zake za awali.

Inaweza kumtokea mtoto mara nyingi kwa siku. Pamoja na kupoteza fahamu lakini nguvu ya misuli haipotei, kwa hiyo kama mtoto alikuwa amekaa atabakia kuwa amekaa badala ya kudondoka chini. Kuna hadithi moja ya mtoto ambaye amewahi kukumbwa na tatizo hili wakati akivuka barabara, na akasimama ghafla barabarani bila kujielewa.

Degedege la kifafa (Generalized Tonic Clonic Seizure) ni aina ya degedege ambalo pia mara nyingi huwapata watoto. Aina hii ya degedege inakuwa na kiashiria muda mfupi kabla ya degedege. Viashiria hivi vinatofautiana kati ya mtoto na mtoto, inaweza kuwa kuhisi kama vitu kutembea mwilini, kuhisi kichefuchefu, harufu, kichwa kuuma, tumbo kuuma, kuhisi uoga, mabadiliko ya ladha tofauti mdomoni nk.

Watoto ambao wana tatizo hili la degedege kwa muda mrefu wanajua pindi pale viashiria vinavyowapata na inakuwa rahisi kwake kukimbilia sehemu ambayo anaona ni salama kabla ya degedege kuanza. Mtoto hupoteza fahamu, wengine hutoa sauti, hugeuza macho au kuyachezesha na misuli ya mwili mzima kukamaa au kuchezacheza.

Wakati wa degedege mtoto anaweza kuung’ata ulimi wake, kukojoa na hata wakati mwingine kupata haja kubwa. Baada ya degedege ambalo linaweza kudumu kwa dakika kadhaa, mtoto anabakia katika hali ya usingizi kwa takribani nusu saa au hata kwa zaidi ya saa 1.

Degedege la watoto wachanga (Neonatal seizure)

Hili huwapata watoto wachanga wenye umri chini ya siku 28 kwa sababu mbalimbali kama vile maambukizi ya vimelea viletavyo magonjwa, matatizo ya kimaumbile ya kuzaliwa nayo (Congenital structural abnormalities), sumu nk. Jinsi au namna wanavyopata degedege ni tofauti sana na watoto wengine kwa sababu degedege linalohusisha misuli ya mwili mzima halitokei kwa watoto wachanga.

Mara nyingi wanakuwa kama wanatafuna kitu, wakati mwingine macho kuyaelekeza upande mmoja bila ya kuyachezesha huku wakiwa wamekakamaa, pia wanaweza kuchezesha miguu kama wanaendesha baiskeli, lakini vilevile degedege linaweza kujionyesha kwa kubadilika rangi, au kutopumua kwa muda (apnea).

Degedege linalodumu kwa muda mrefu (Status Epilepticus)

Aina hii ya degedege ambayo ni ya hatari zaidi hutokea pale ambapo mtoto anapata degedege zaidi ya dakika 30 na zaidi pasipo kurudi katika hali yake ya ufahamu.

Dalili za degedege

Kulingana na sehemu ya ubongo iliyohusika, dalili za degedege huonekana katika sehemu tofauti tofauti za mwili. Inaweza kuhusisha sehemu moja ya mwili (localized) ambapo unaweza kuona misuli ya upande mmoja wa mwili wa mtoto ikicheza na kukakamaa au inaweza kuhusisha mwili wote (generalized).

Degedege linaweza kuambatana pia na upotevu wa fahamu kwa mtoto. Kuna baadhi ya degedege inawia vigumu kutambua pale inapotokea. Degedege hutofautiana kutegemea na umri wa mtoto. Degedege linalowapata watoto wachanga ni tofauti na la watoto wa umri mwingine.

Zifuatazo ni dalili mbalimbali za degedege zinazoweza kutokea kwa mtoto wa umri wowote

  • Mabadiliko katika mfumo wa fahamu ambapo mtoto hupoteza fahamu
  • Mabadiliko katika hisia kama vile kuwa na woga, hofu isiyoelezeka, furaha iliyopitiliza au kicheko kisicho na maelezo
  • Mabadiliko katika hisia ya ngozi kama mtoto kujihisi kutambaliwa na mdudu kwenye mkono, mguu, mgongoni (tactile hallucinations) n.k
  • Mabadiliko katika macho kama vile kuona vitu vya ajabu ambavyo havipo (visual hallucinations), kuona mwanga ikiwaka na kuzima (flashing lights)
  • Upungufu wa nguvu ya misuli hali inayoambatana na kudondoka chini ghafla
  • Misuli kukakamaa au misuli kucheza ambapo inaweza kuwa sehemu moja ya mwili au kuhusisha mwili wote
  • Mabadiliko katika hisia ya ulimi ambapo mtoto hujihisi hali ya uchungu mdomoni

Katika hizi dalili, inawezekana kabisa mtoto akaonesha dalili mojawapo tu au akawa na dalili zaidi ya moja. Dalili hizi zinaweza kudumu kwa muda mchache sana toka sekunde mpaka dakika chache au kuwepo kwa muda mrefu zaidi ya dakika 30.

Vipimo

Ni muhimu kwa watoto wote kufanyiwa mahojiano na uchunguzi wa kina ili kugundua tatizo. Kabla ya vipimo ni muhimu kupata taarifa ya mtoto kutoka kwa mzazi/mlezi kuhusu historia ya kuzaliwa, ugonjwa wowote kwa wakati huo au siku za karibuni, matumizi ya dawa au kemikali yoyote.
  • Kipimo cha damu si lazima kwa watoto wenye simple febrile seizuires. Uchunguzi wa kimaabara hufanyika kulingana na historia ya mtoto na hali yake kwa ujumla.
  • Kipimo cha mkojo
  • Kipimo cha maji ya uti wa mgongo (Lumbar Puncture)
  • Imaging Kipimo hiki CT Scan kinafanyika pale tunapohisi kuwa na hitilafu katika mfumo wa neva
  • Electroencephalography (EEG)
  • Chromosome na DNA
  • TORCH antibodies studies

Matibabu

Matibabu kwa watoto wadogo ni tofauti na watu wazima. Isipokuwa kwa sababu maalum na baada ya uchunguzi, watoto hawatakiwi kupata dawa pale wanapopata degedege kwa mara ya kwanza. Sababu ya kutowapa dawa mara ya kwanza wanapokwenda hospitalini ni

  • Madaktari wengi wanakuwa hawana uhakika kama lililotokea ni degedege au la
  • Dawa nyingi zina madhara makubwa kwa mtoto
  • Mara nyingi watoto wengi wanapata degdege mara moja

Kama dawa itatolewa, daktari atatoa dawa sahihi katika ngazi husika kulingana na majibu ya uchunguzi uliofanyika na vilevile kumfuatilia mtoto ili kujua kama kuna madhara yeyote baada ya kutumia dawa. Mara nyingi huchukua wiki na zaidi au miezi kuizoea dawa na wakati mwingine inahitajika dawa zaidi ya moja kuweza kulikabili tatizo.

Imesomwa mara 42222 Imehaririwa Jumatatu, 18 Februari 2019 16:07
Dr. Paul J. Mwanyika

Dr. Paul J. Mwanyika ni Daktari  Bingwa waTiba na Uchunguzi wa Magonjwa ya Watoto (Pediatrics).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.