Image

Sababu na matibabu ya Kucheua Kwa Mtoto (Infant Reflux)

Kucheua kwa mtoto ni hali ya mtoto kutoa chakula kupitia mdomoni muda mfupi baada ya kula/kunyonya.Kucheua kwa mtoto hupungua kadri mtoto anavyokuwa mkubwa na ni nadra sana kutokea baada ya mtoto kufikisha umri wa miezi 18.

Kucheua pia kunaweza kuashiria tatizo kubwa zaidi kwa mtoto kama ugonjwa wa Gastro-esophageal Reflux Disease (GERD), mzio (allergy) au kuziba kwa mrija wa kupitishia chakula.

Nini husababisha mtoto kucheua baada ya kula? 

Maumbile ya asili ya misuli ya mtoto (lower oesophageal sphincter)-Kwa watoto wachanga, misuli inayounganisha mrija wa kupitisha chakula na tumbo yaani lower oesophageal sphincter, huwa haijakomaa (immature),hivyo kuruhusu chakula (maziwa) kurudi juu yaani kuelekea mdomoni badala ya kwenda kwenye tumbo moja kwa moja.Kazi maalum ya misuli hii ni kufungua njia kuruhusu chakula kuingia kwenye tumbo na kufunga kuzuia chakula kurudi kilikotoka yaani mdomoni.Hivyo, kutokukomaa kwa misuli hii huchangia kucheua kwa watoto

Maziwa ya watoto pia huchangia kutokea kwa hali hii kwani maziwa yapo kwenye majimaji hivyo ni rahisi kurudi juu na kutolewa tena mdomoni.

Kuwepo kwa hewa kwenye tumbo ambayo hutokana na mtoto kunyonya haraka sana/kunyonya sana au mama kutojuwa jinsi ya kumnyonyesha mtoto wake kwa njia sahihi huchangia kutokea kwa hali hii ya kucheua.

Kwa kawaida mtoto hucheua baada ya kunyonya lakini mara nyingine kucheua kwa mtoto hutokana na

 • Allergic gastroenteritis- Mzio (Allergy) wa protini inayopatikana kwenye maziwa ya ng’ombe
 • Gastroesophageal reflux disease (GERD)-Huu ni ugonjwa unaosababishwa na kucheua kwa tindikali inayotoka tumboni ambayo pia huharibu kuta za mrija wa kupitisha chakula (oesophagus).Kitu chochote kile kinachoongeza presha (Intra-abdominal pressure) chini ya lower oesophageal sphincter kama uzito ulopitiliza (obesity), kutopata choo kwa muda (constipation), baadhi ya vyakula, vinywaji na baadhi ya dawa husababisha GERD.
 • Eosinophilic oesophagitis- Hali inayotokana na kukusanyika kwa wingi kwa chembechembe za damu aina ya eosinophils na hivyo kuharibu kuta za mrija wa kupitisha chakula.
 • Mrija wa chakula kuwa mwembamba/kuziba hali inayojulikana kitaalamu kama oesophageal stricture au sehemu ya misuli kati ya tumbo na mrija wa chakula kuwa nyembamba au kuziba nayo hujulikana kwa kitaalamu  kama pyloric stenosis

Dalili za Infant Reflux

Kucheua kwa mtoto ni hali ya mabaki ya chakula kutolewa kupitia mdomoni baada tu ya mtoto kunyonya.Mtoto pia anaweza kutapika. Ikiwa mtoto wako ana afya njema, hana tatizo basi huna haja ya kuwa na wasiwasi kama akicheua au kutapika baada ya kunyonya ingawa kabla ya kupata hali hii mtoto anakuwa anasumbuka sana au kulia, akiashiria kupata taabu tumboni kwa sababu hajacheua/kutapika, hivyo wewe kama mama au baba hutakiwi kuwa na hofu.

Ni wakati gani wa kumpeleka mtoto kwa daktari?

Mpeleke mtoto kwa daktari kama

 • Haongezeki uzito 
 • Anacheua kwa nguvu mpaka macheuo au matapishi yakaruka nje kwa nguvu sana (projectile vomiting)
 • Anajikamua sana kabla ya kucheua/kutapika na kupata maumivu
 • Anacheua macheuo ya rangi ya kijani au ya njano
 • Anacheua macheuo yaliyochanganyika na damu au yenye rangi ya kahawia
 • Anakataa kunyonya
 • Anapata choo kilichoambatana na damu
 • Anapumua kwa shida
 • Anatapika baada ya kufikisha miezi sita
 • Anapata taabu ya kumeza chakula,kunguruma kwa sauti yake (hoarseness of voice),ana maumivu ya koo (sore throat), pua zimeziba kwa muda mrefu, maambukizi kwenye pua/masikio

Kama mzazi tambua ya kwamba

 • Baadhi ya watoto huanza kucheua wakati meno yanapoanza kuota, wakati wanaanza kutambaa,au wakati wanaanza kula vyakula vigumu (solid foods).
 • Baadhi ya watoto wakati wa kunyonya hutoa titi la mama ili waangalie mazingira yanayowazunguka/au wale wanaopenda kucheza na titi la mama wakati wa kunyonya,huingiza hewa ndani na hivyo kusababisha  kucheua
 • Kucheua hutokea baada tu ya mtoto kunyonya au saa 1-2 baada ya kunyonya
 • Watoto wachanga hadi kufikia umri wa miezi mitatu hucheua angalau mara moja kwa siku
 • Kucheua kwa watoto huongezeka mtoto anapofikisha umri wa miezi 2-4
 • Watoto wengi hupunguza kucheua wanapofikisha umri wa miezi 7-8 na
 • Huacha kabisa wanapofikisha umri wa mwaka mmoja

Vipimo vya Uchunguzi

Kama daktari wako atahisi mtoto wako ana tatizo zaidi kutokana na hali yake ya kucheua, baadhi ya vipimo ambavyo anaweza kumfanyia mtoto ni kama ifuatavyo

 • Ultrasound-Kipimo hiki kinaweza kuonyesha kuziba/kupungua kwa njia ya mrija wa chakula au kama mtoto ana pyloric stenosis kama nilivyoeleza hapo awali
 • Vipimo vya damu kama Complete blood Count ambacho huangalia wingi wa chembechembe za damu, maumbile yao, aina ya chembechembe hizo. Pia kipimo cha mkojo (urinalysis) ni muhimu kufanywa.
 • Eosophageal PH monitoring- Kipimo hiki husaidia kujua kama macheuo ya mtoto yana tindikali au la na hufanywa kwa daktari kuingiza mpira mwembamba kupitia pua au mdomo wa mtoto mojamoja kwenda kwenye mrija wa chakula, mbele ya mpira huu kuna kifaa maalum cha kupima PH ya mtoto wako kwa ndani.Kipimo hiki pia kitamsaidia mzazi kujua kama malalamiko, usingizi wa taabu anaopata mtoto (sleep disturbance) na mtoto kulia mara kwa mara (irritability) hutokana na tindikali au la.
 • X-rays za tumbo (Upper GI Series- Mtoto hupewa dawa kama chaki ya majimaji na kisha hupigwa picha za X-rays ambazo zitaonesha kama kwenye utumbo wa mtoto ana shida yoyote ile.
 • Upper endoscopy-Kipimo hiki ambacho hufanywa kwa kutumia mpira maalum wenye kamera kwa mbele ambao huingizwa kwenye mrija wa chakula (oesophagus) kupitia mdomoni mpaka kwenye sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo na kwenye tumbo, husaidia kujua kama mrija wa chakula umeziba/kuwa mwembamba au umepata mcharuko wa maambukizi (oesophagitis).Kipimo hiki kwa watoto hufanywa kwa mtoto kupewa dawa ya usingizi au nusu kaputi.

Matibabu ya kucheua

Mara nyingi kucheua kwa mtoto hakuna madhara yoyote yale na husaidiwa kwa;

 • Kumpa mtoto milo midogo midogo mara nyingi (small frequent feedings)
 • Kukatisha chakula na kumweka mtoto begani
 • Kumweka/Kumshika mtoto akiwa wima wakati wa kunyonya au baada ya kunyonya
 • Hakikisha unamlaza mtoto chali na si kulala kifudifudi
 • Tiba inaweza kuwa ya dawa kama ambazo zinazozuia tindikali au ya upasuaji (fundalplication procedure) kwa wale wenye pyloric stenosis.

 

 

 

 

Imesomwa mara 33959 Imehaririwa Jumanne, 15 Januari 2019 10:35
Dr. Paul J. Mwanyika

Dr. Paul J. Mwanyika ni Daktari  Bingwa waTiba na Uchunguzi wa Magonjwa ya Watoto (Pediatrics).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.