Image

Naweza kunywa pombe kama nina ugonjwa wa kisukari?

Naweza Kunywa Pombe kama nina Ugonjwa wa kisukari?

Wagonjwa wengi wa kisukari wameniuliza kuhusu swali hili.Aghalabu, hata wengine ambao wanasoma makala hii pia watakuwa na shauku ya kutaka kujua kama kweli wanaweza kunywa pombe ilihali wanaugua ugonjwa wa kisukari bila kupata madhara yoyote ya afya.Swali hili ni la msingi sana hasa unapokuwa kwenye matibabu ya ugonjwa wa kisukari.

Ugonjwa wa kisukari ni moja kati ya magonjwa mengi yasiyoambukiza (non-communicable diseases) ambayo yanongezeka kwa kasi na kusababisha vifo na ulemavu.

Taarifa ya International Diabetes Federation imesema watu millioni 463 duniani wanaishi na kisukari na millioni 19 ya hao wapo bara la Afrika pekee.

Shirika hili katika taarifa yake ya mwaka 2020 limesema kwamba uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari  nchini Tanzania ni kwa asilimia 3.7 huku idadi ya wagonjwa wa kisukari watu wazima imefika takribani watu 997,400.

Unywaji wa pombe uliopitiliza kwa watu wenye kisukari husababisha madhara makubwa ikiwemo kuongeza hatari ya kupata shinikizo la damu, magonjwa ya moyo,macho na kuharibika kwa mishipa ya fahamu.

Aidha Pombe au vileo vingi vina idadi kubwa ya wanga na sukari hivyo husababisha kupanda kwa haraka kwa sukari kwenye damu. Pia vina kalori nyingi hii upelekea kuwepo hatari ya kuongezeka uzito uliopitiliza ambapo hupunguza unyeti (sensitivity) na utolewaji wa kichocheo aina ya insulin  mwishowe husababisha ugumu wa kudhibiti sukari yako mwilini.

Sasa je naweza kunywa pombe kama ni ugonjwa wa kisukari?

jibu ni NDIO japo inabidi ujenge tabia ya kuwa na tahadhari pindi unapokunywa pombe.

Utatumia pombe pale tu ambapo sukari yako imedhibitiwa vizuri na kwa hali yoyote epuka unywaji pombe kupitiliza.

Najua kuna swali unaliwaza kuwa nisinywe kupitiliza unaamanisha nini?

Hili ni swali zuri na la msingi.Kulingana na shirika la ugonjwa wa kisukari la marekani (American Dabetes Association), imetoa vipimo vifuatavyo vya unywaji wa pombe kwa watu wenye kisukari.

Mwanamke mwenye kisukari asinywe zaidi ya chupa moja ya bia  sawa na 350mls, au 147 mls za wine na 44 mls za pombe kali kwa siku.

Kwa mwanamume, asinywe zaidi ya bia mbili sawa na 700mls, au 294 mls za wine au  88 mls za pombe kali.

USHAURI

Kabla ya kunywa pombe hebu jiulize masawali yafuatayo;

Je sukari yangu imedhibitiwa?

Je daktari wangu anakubali nitumie pombe au kilevi cha aina yoyote ile?

Je najua jinsi pombe inaweza kuniathiri mimi pamoja na sukari yangu?

Kama majibu yako yote ni ndio basi waweza kunywa pombe. Ila kumbuka pombe pia husababisha sukari kushuka. Ni vizuri kufahamu kiwango cha sukari yako mwilini kabla, wakati na baada ya kunywa pombe angalau kwa kipindi cha masaa 12.

Usikose kutembelea TanZMED kwa makala zaidi za afya kwa lugha ya kiswahili.

 

Imesomwa mara 2818 Imehaririwa Jumapili, 31 Januari 2021 20:45
Dr Hamphrey

Dr. Hamphrey S. Kabelinde MD ni mhitimu wa shahada ya Udaktari katika Chuo kikuu ya afya na sayansi shirikishi Muhimbili. Mwandishi na mhariri wa makala za afya Tanzmed.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.