Image

Hatari za kubeba ujauzito kipindi ukiwa na shida ya kufunguka mlango wa kushoto wa moyo

Tatizo la kufunguka mlango wa kushoto wa moyo unaotenganisha chumba kidogo na kikubwa cha moyo na  kuzuia  kupita kwa damu ya kutosha kwenda kwenye mshipa mkubwa wa damu (Aorta) ambao huhusika kuzungusha damu ndani ya mwili hujulikana kama mitral stenosis

Visababishi

Tatizo hili la kufunguka mlango wa kushoto wa moyo unaotenganisha chumba kidogo na kikubwa husababishwa na;

  • Homa inayojulikana kama rheumatic fever
  • Mtu anaweza kuzaliwa na hali hii
  • Matibabu ya saratani za kifua kwa kutumia tiba ya mionzi
  • Mkusanyiko wa madini aina  calcium kwenye milango hiyo ya moyo

Kati ya hizi sababu hapo juu, inayosababisha kutokea kwa  tatizo hili kwa wakubwa ni homa ya rheumatic fever, ambayo hufuatia maambukizi ya vimelea vya bakteria aina ya  streptococci kwenye koo au ngozi ambayo hayakutibiwa kikamilifu

Mtu mwenye tatizo hili anaweza kutopata dalili au viashiria vyovyote vile mpaka pale  atakapotimiza  umri wa miaka 20 hadi 50. Hata hivyo wengine wanaweza kupata dalili na viashiria vya tatizo hili wakati wa kufanya mazoezi  au kazi yoyote ambayo inaongeza mapigo ya moyo, msongo mawazo na wakati wa kubeba ujauzito.

Dalili na viashiria vyake  ni

  • Kushindwa kupumua vizuri wakati wa kujishughulisha na shughuli yoyote ile na wakati mwingine kutopumua vizuri hata muda wa kupumzika kama tatizo limekuwa kubwa sana (severe mitral stenosis)
  • Kukohoa makohozi yaliochanganyika na damu kidogo (hemoptysis)
  • Kushindwa kupumua ukiwa umelala bila mto au kitanda kunyanyuliwa 
  • Kushtuka usiku na kubanwa pumzi
  • Kubanwa na pumzi wakati wa mazoezi
  • Uchovu (fatigue)
  • Kusikia au kuhisi mapigo yako ya moyo (palpitations)
  • Kuvimba Miguu (lower limb edema)

Muonekano wa ndani wa moyo

Ujauzito kuambatana na tatizo hili la kufunguka kwa mlango wa kushoto wa moyo unaotenganisha chumba kidogo na kikubwa

Tatizo hili la ujauzito kuambatana na kufunguka kwa mlango wa kushoto wa moyo unaotenganisha chumba kidogo na kikubwa limegawanyika  katika hatua tatu- Kali kiasi, wastani na kali zaidi, dalili na viashiria vya tatizo hili huwa mbaya zaidi pale mama mjamzito anapokuwa na tatizo la kufunguka kwa mlango wa kushoto wa moyo unaotenganisha chumba kidogo na kikubwa katika hatua ya wastani na kali zaidi, maana ujauzito pekee  uhitaji kuongezeka kwa ujazo wa damu hasa miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito na upungufu unaotokana na milango ya moyo kushindwa  kufunguka hufanya hatua ya kujifungua ya mama mjamzito kuwa ya hatari sana.

Hivyo ujauzito ulioambatana na tatizo hili husababisha

  • Moyo kushindwa kufanya kazi vizuri
  • Moyo kupiga bila mpangilio wake

Hatari kwa mtoto

  • Mtoto kuzaliwa kabla ya wakati (premature delivery)
  • Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo (low birth weight baby)
  • Mtoto kufa kwenye mfuko wa kizazi au baada ya kuzaliwa (Intrauterine fetal death or stillbirth)

 Vipimo muhimu vya kufanya

  1. Echocardiogram- Ambacho huonyesha tatizo hlii vizuri hadi hatua gani lilipofikia, ukubwa wa vyumba vya moyo na uwezo moyo kufanya kazi, na iwapo moyo kama haufanyi kazi yake vizuri
  2. ECG- Huonyesha kiwango cha mapigo ya moyo na vilevile kama moyo unapiga bila mpangilio

Vipimo hivi vyote ni salama kwa mama mjamzito

Matibabu

Ni muhimu kwa mgonjwa kuzingatia kuonana na daktari pamoja na kuandikiwa dawa ambazo hutumika kudhibiti dalili na viashiria vya tatizo hili ambazo ni dawa aina ya furosemide, spironalactone, na digoxin.

Kwa wajawazito walio kwenye hatua  ya wastani na kali zaidi ya tatizo hili  watahitaji tiba ya kuzibua mlango huo unaotenganisha vyumba vya kushoto vya moyo, kwa  kupitia mshipa wa damu wa kwenye paja mpaka kwenye moyo na kuweza kuzibua mlango huo (Percutaneous mitral balloon Valvuloplasty) , baada ya tiba hii wanaweza kujifungua kwa njia ya kawaida.

Baadhi ya wajawazito watahitaji  kufanyiwa upasuaji wa kuzalisha mtoto na hapo baadae  kurudi hospitali  kurekebishwa au kubadili huo mlango wa moyo mwenye tatizo la kutofunguka (mitral valve repair or replacement)

Imesomwa mara 7350 Imehaririwa Ijumaa, 26 Julai 2019 17:22
Dr.Mayala

Dr.Henry A Mayala ni daktari bingwa Wa Tiba ya moyo katika taasisi ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambaye kwasasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) ya Tiba ya Moyo katika Chuo Kikuu cha Tongji  nchini China.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Makala shabihana