Image
Kwa muda mrefu sana wanawake wamekuwa wakitumia parachichi kama nyenzo mojawapo ya urembo ima kwa kupaka kwenye uso au  nywele bila kuwa na uhakika kama kweli parachichi husaidia katika kurutubisha nywele na ngozi ya kwenye uso, swali ni je ni wangapi wanajua faida za parachichi kiafya, hususani faida ya kuukinga mwili dhidi ya kemikali hatari pamoja na kumfanya mtu kuonekana kijana?
 
Wanasayansi wa chuo kikuu cha Michoacana de San Nicolas de Hidalgo cha nchini Mexico wamesema ya kwamba parachichi husaidia katika kuukinga mwili dhidhi ya kemikali hatari (free radicals) na hivyo kuweka kinga dhidhi ya magonjwa mengi pamoja na kumfanya mtu kuonekana kijana (fight against ageing). Wanasayansi hao wamesema kwamba mafuta yanayopatikana katika parachichi yanauwezo wa kupenya hadi ndani ya injini inayotengeneza nishati mwilini inayopatikana katika seli inayojulikana kama mitochondria.
 
Free radicals ni kemikali zinazosababisha magonjwa mengi yakiwemo baadhi ya saratani, huharibu mishipa ya damu ya ateri (arteries), pamoja na kumfanya mtu kuzeeka haraka. Mafuta yanayopatikana katika baadhi ya mboga za majani, matunda na nyanya/tungule (tomatoes) yanauwezo wa kupambana na kemikali hizi hatari lakini mafuta haya hushindwa kuingia ndani ya mitochondria ambapo ndio kuna kemikali hizi hatari kwa wingi.
 
Mtafiti Christian Cortes-Rojo kutoka chuo kikuu hicho cha Mexico ambaye ndiye alifanya utafiti huu, alisema ‘’Anti-oxidants zinazopatikana katika mboga za majani na matunda mengi haziwezi kupenya ndani ya mitochondria na hivyo kushindwa kudhibiti kemikali hatari ndani ya mitochondria hizo. Hivyo kusababisha kemikali hizo hatari kuendelea kushambulia mitochondria na  kuziharibu, matokeo yake ni kuwa nishati haitolewi tena kutoka kwenye mitochondria na seli hushindwa kufanya kazi na kufa.”